STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
8.3.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefungua Hoteli ya Park Hayatt yenye hadhi na
Nyota Tano na kusema kuwa Serikali itaendelea kulinda hali ya amani na utulivu,
jambo ambalo limeipatia sifa kubwa Zanzibar na kuendelea kuwavutia wageni
kutoka pande zote za dunia.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa Hoteli mpya ya Nyota Tano ya Park Hayatt, huko
Mambo Msiige katika eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Katika hotuba
yake aliyoitoa katika ufunguzi wa Hoteli hiyo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali
itaendelea kuwalinda watalii, wawekezaji pamoja na mali na rasilimali zao
zilizopo nchini.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa Serikali itaendelea na jitihada zake za kuimarisha miundombinu ya
viwanja vya ndege ambapo hivi karibuni ujenzi wa Jengo la Abiria katika kiwanja
cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume Zanzibar unatarajiwa utakamilika
huku ikiwa tayari sehemu ya bandari kwa ajili ya abiria umekamilika kwa
mashirikiano na Mfanyabiashara maarufu Bwana Said Bakhresa.
Dk. Shein
aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kujenga bandari kubwa ya kisasa katika
eneo la Mpiga Duri Mjini Zanzibar ambapo hatua za awali za michoro
imeshakamilika na hatua inayofuata hivi sasa ni kutafuta fedha kwa ajili ya
ujenzi wa bandari hiyo.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alitoa shukurani na pongezi
kwa uongozi wa Kampuni y
a ASB Holdings,
hasa Sheikh Saeed Juma Al-Bawardy kwa kuchagua kuijenga hoteli hiyo hapa
Zanzibar.
Dk. Shein
aliuhakikishia uongozi wa Kampuni hiyo kuwa uamuzi wao wa kuichagua Zanzibar ni
sahihi na unakwenda sambamba na mipango ya Serikali ya kuimarisha utaluii na
uchumi wa Zanzibar.
Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya Ujenzi ya ‘China Railways Jianchang
Engineering Co Ltd’ (CRJE) kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa ustadi wao wa kujenga
jengo jipya la hoteli hiyo linalokidhi viwango vya Mji Mkongwe wa Kimataifa.
Katika hatua za
kuimatrisha sekta ya utalii hapa nchini, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali
ilitunga Sheria Nam. 9 ya kuimarisha utalii mwaka 1996 ambayo iliipa nguvu
Kamiosheni ya Utalii iliyoanzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kuisimamia sekta ya
uatlii ambapo idadi ya watalii ilizidi kuongezeka hapo mwaka 2007 jumla ya
watalii 143,282 walitembelea Zanzibar.
Dk. Shein
alieleza juhudi nyengine zilizochukuliwa na Serikal;i katika kuimarisha sekta
ya Utalii ikiwa ni pamoja na kutangaza rasmi dhana ya Utalii kwa Wote hapo
tarehe 16 Oktoba, 2011 ambapo lengo kuu ni kuhakikisha kila mwananchi
ananufaika na matunda ya utalii na anashiriki katika kuuendeleza.
Aliipongeza
Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) kwa bidii inayochukua katika
kuzifanikisha shughuli za uwekezaji katika miradi mikubwa kama hiyo.
Sambamba na hayo
Dk. Shein hakuchelea kuelezea changamoto kadhaa na mitihani mbali mbali
iliyojitokeza katikamchakato wa awali katika ujenzi wa hoteli hiyo na kueleza jinsi alivyosimama kidete katika
kuhakikisha ujenzi wa Hoteli hiyo unafanikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu
za nchi sambamba na kuheshimu maamuzi ya Serikali huku akitoa pongezi kwa Rais
mstaafu wa Awamu ya Sita Mhe. Dk. Amani Abeid Karume ambapo mchakato wa ujenzi
wa Hoteli hiyo ulianza katika awamu yake.
Pia, Dk. Shein
aliihimiza Wizara ya Ardhi, Maji na Nishati kuendelea kusimamia kwa karibu
shughuli zote za ujenzi, ukarabati na usanifu wa Mji Mkongwe kwa lengo la
kuhakikisha kuwa majengo yanayojengwa yanakidhi viwango na hadi ya kuwa ni
sehemu ya Mji Mkongwe kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Serikali na vigezo
vya UNESCO.
Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kuliagiza Baraza la Maji la Zanzibar kuongeza kasi ya usafi
katika wakati huu ambapo limepata vifaa mbali mbali vya kisasa kwa ajili ya
kuendeshea shughjuli zao.
Aidha, Dk. Shein
aliihimiza Wizara ya Habari, Utamaduni,Utalii na Michezo kuendelea kushirikiana
na Wawekezaji walioekeza hapa nchini katika kuvitangaza vivutio viliopo vya
utalii vipya na vya zamani pamoja na huduma bora zinazopatikana katika hoteli
za Zanzibar.
Dk. Shein pia,
alieleza mipango inayokamilishwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kufungua
Ofisi ya Uwakala wa Utalii mjini Mumbai-
India kwa lengo la kuitangaza Zanzibar hasa Mashariki ya Kati na Mashariki ya
Mbali ikiwemo China na India.
Nae Waziri wa Dk.
Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora ambaye
pia ni Kaimu Waziri wa Fedha alieleza kuwa
takwimu zinaonesha kuwa sekta ndogo ya Hoteli na mikahawa imeweza
kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nje kuliko sekta nyengine hapa nchini.
Alisema kuwa
hatua hiyo inatokana na juhudi za pamoja baina ya Sekta binafsi na Serikali
katika kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji hapa nchini huku akieleza azma ya
Serikali kulenga katika kushajiisha uwekezaji wa Daraja la juu, ambapo hoteli
hiyo ya Park Hyatt ni aina ya uwekezaji unaohitajika hivi sasa hapa nchini.
Mapema Kaimu
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Bwana Vuai
Lada alisema kuwa Mradi wa Zamani Palace chini ya Kampuni ya SB Holdings Ltd
unamilikiwa na Bwana Ali Saeed Juma Albawardy ambaye ni raia wa Falme za
Kiarabu (UAE), ulithibitishwa na ZIPA mwezi Oktoba mwaka 2010 ukiwa na mtaji wa
makisio wa Dola za Kimarekani milioni 30.
Lada alisema kuwa
Mradi huo ambao utafanya biashara zake kwa jina la Park Hyatt Zanzibar, mpaka
sasa umeshahawekeza zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 25 na unatarajiwa
kufikia zaidi ya Dola milioni 30 mpaka kumalizika kwake.
Alisema kuwa
hoteli hiyo ina jumla ya vumba 67, viwili ni ‘ Presidencial suites’, vitatu ni
‘executive suites’ na sita ‘Junior suites na 57 ni vya kawaida. Aidha alieleza
kuwa hoteli hiyo hadi sasa imeshaajiri wafanyakazi 150 na nafasi 10
zinashikiliwa na wageni na 140 zinashikiliwa na wenyeji.
Kaimu huyo
Mkurugenzi alisema kuwa hoteli hiyo itainua daraja la utalii hapa Zanzibar kwa
kuwa na watalii wa daraja la juu pamoja na kupanua soko la utalii kwa nchi za
Ghuba na Mashariki ya Mbali sambamba na kushawishi sekta nyengine kama vile
kilimo, uvuvi na biashara ndogondogo.
Nao Wawakilishi
wa Mwekezaji wa Hoteli hiyo Bwana Pablo
Graf na Bwana Philip D’Abo walitoa pongezi kwa wananchi wa Zanzibar na viongozi
wa Serikali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ukarimu wao mkubwa na kueleza
kwa nyakati tofauti kuwa ujenzi wa hoteli hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa
kukuza soko la ajira hapa nchini sambamba na kuinua utalii wa Zanzibar huku
wakieleza mafanikio na maendeleo ya miradi kama hiyo kwenye nchi za Ulaya,
Marekani na Falme za Kiarabu ambapo wameekeza.
Viongozi mbali
mbali pamoja na wageni waalikwa walihudhuria katika ufunguzi huo akiwemo Rais
Mstaafu wa Awamu ya Sita Mhe. Dk. Amani Abeid Karume, Makamu wa Pili wa Rais
Balozi Seif Ali Idd, Mama Shadya Karume, Mmiliki wa Hoteli ya Park Hyatt
Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya ASB Bwana Saeed Juma Albawardy, Mawaziri pamoja
na viongozi mbali mbali. Huku hafla hiyo ikipambwa na tenzi pamoja na taarab
asilia.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment