Habari za Punde

Kutoka baraza la Wawakilishi: Kuongezeka kwa Baa ni tamaa za wamiliki wa maeneo bila ya kujua athari zake


Na Abdulla Ali na Rahma Khamis Maelezo

Kuongezeka kwa biashara ya vilevi (Baa) katika mji wa Zanzibar kunatokana na tamaa za wamiliki wa maeneo kwa kuuza kiholela bila ya kujua lengo la mnunuzi na athari zinazoweza kujitokeza katika jamii.

Haya yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji Omari Kheri katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Mhe. Jaku Hashim Ayoub alipotaka kujua kuwa Serekali imewaambia nini  wananchi wa  Jimbo la Kiembe Samaki kuhusiana na tatizo hilo.

Aidha amesema biashara ya vileo nchini Zanzibar inaendeshwa kwa kufuata Sheria ya Vileo ya 1928, ambayo ndiyo iliyoweka utaratibu wa ukataji wa leseni na adhabu kwa wanaokwenda kinyume na taratibu za leseni hizo.

Amesema kila Mwaka kabla ya kutolewa leseni mpya kwa vilabu vya vilevi (Baa) hutolewa matangazo ili wale wenye pingamizi za kuwepo kwa Baa kupeleka pingamizi zao katika mamlaka ya utoaji wa leseni na hatimaye hutakiwa kufika katika vikao vya majadiliano na wajumbe wa mahakama ya vileo.

Hata hivyo  Waziri huyo amesema pamoja na kuwepo Sheria hiyo kwa muda mrefu na kufanya kazi hadi leo bila ya kua na matatizo makubwa, hivyo niwazi kuwa inahitaji marekebisho ili iendane na hali halisi ya sasa.

Waziri Kheri ameeleza kuwa Ofisi yake imewasiliana na Tume ya Kurekebisha Sheria ili kuifanyia mapitio na kuipendekeza sheria mpya itakayowasilishwa barazani hapo kwa ajili ya kujadiliwa na hatimae kuweza kutumika kama sheria iliyo kamili mara baada ya kupitishwa na wajumbe wa Baraza hilo.

“Nashukuru Tume imeshakamilisha kazi hiyo na kutupa Rasimu ya Sheria mpya baada ya kushauriana na wahusika wengine na Ofisi yangu inaifanyia kazi na muda si mrefu Mswada wa Sheria hiyo utaletwa katika Baraza lako tukufu.”Waziri amesema.

Akifafanua kuhusiana na Baa amefahamisha kuwa Jimbo la Kiembe Samaki kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo Baa kumi na moja (11) ambazo zote hizo zimepewa leseni kwa mujibu wa taratibu za kisheria, na Ofisi hiyo haina taarifa za kuwepo kwa Baa ambazo hazina leseni na zinazofanya kazi ndani ya Jimbo la hilo.

Ametanabahisha kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo adhabu ya kuendesha biashara hiyo bila ya leseni ni faini au kifungo au vyote 2 kisichozidi miezi 12 na Mahakama imepewa uwezo wa kisheria wa kufilisi vinywaji vyote vitakavyokutwa ndani ya Baa isiyo na leseni.

Waziri  Kheri amewataka wananchi pamoja na kuwaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutumia utaratibu uliowekwa kisheria kwa ajili ya kutoa malalamiko yao ili yapatiwe ufumbuzi kwa wakati na hatimae kuweza kuondokana na kero ndogondogo zinzowakabili wananchi katika makaazi yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.