Habari za Punde

KONGAMANO LA UNESCO NA WIZARA YA ELIMU LAMALIZIKA, VIPAUMBELE VYA ESDP VYAPATIKANA

1
Mkuu wa Ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues akisisitiza jambo wakati wa kongamano la kujadili vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu (ESDP) lililofanyika katika ukumbi wa NACTE, jijini Dar es Salaam.(Picha na Philemon Solomon wa Fullshwangwe)
Na Rabi Hume, Modewjiblog
Kongamano lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi limemalizika jana jijini Dar es Salaam baada ya kupitisha vipaumbele ambavyo vitatumika katika Mpango wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu (ESDP) kwa miaka mitano kuanzia 2017 – 2021.
Akizungumza na Mo Dewji Blog, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Elimu, Clifford Tandari alisema kupitia kongamano hilo wamethibitisha vipaumbele ambavyo vitatumika ili kuifanya elimu ya Tanzania kuwa bora na yenye manufaa kwa miaka ya mbeleni.
Alisema kupitia kongamano hilo wamethibitisha ili kuwapo na elimu bora nchini kunahitajika kuwa na walimu wenye sifa na ubora unaohitajika, mashuleni kutumika vitabu vya ziada na kiada, kuimarisha huduma ya ukaguzi mashuleni, watoto wote wenye umri wa kwenda shule wapelekwe shuleni na kuwajengea uwezo wa stadi za kazi wahitimu ili hata wanapomaliza masomo waweze kujiajiri.
“Tumethibitisha yale maeneo muhimu ya sekta ya elimu ambayo tumegundua kwamba ili tuweze kusonga mbele lazima tuimarishe ubora wa elimu yetu kama ni walimu wasome vizuri wawe na ubora, tuwe na vitabu wanafunzi wapate maarifa kutoka kwenye vitabu, kudhibiti ubora wa elimu na watoto waende shule kwa shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi na elimu ya juu,” alisema Tandari.
Aidha Tandari alieleza kuwa awali walikuwa wakishindwa kuwa na mipango ya aina hiyo kutokana na kutokuwepo kwa fedha lakini kwa sasa wataweza kugharamia mpango huo wa elimu kutokana na serikali kuwa tayari kusimamia mpango huo wa kuboresha elimu ya serikali.
Aliongeza kuwa wao kama Wizara ya Elimu wanaamini kuwa mfumo wa elimu kwa sasa utakwenda vizuri kutokana na kasi aliyonayo rais wa awamu ya tano, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ameamua kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi sekondari na kutokana na kasi yake ya utendaji kazi wanataraji utafanyika kama jinsi unavyopangwa.
2
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Elimu, Clifford Tandari akiwaelezea washiriki wa kongamano hilo (hawapo pichani) kuhusu Mpango wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu (ESDP) ambao utafanyiwa kazi kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017 – 2021.

Naye Mkuu wa Ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikiaa Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues alisema kuwa kongamano hilo limekuwa zuri kutokana na makubaliano ambayo washiriki wameyafikia katika kusaidia elimu ya Tanzania kukua kwa kipindi cha miaka mitano ijayo na hiyo ni hatua ya awali ambayo wameanza nayo na hadi kufikia mwezi Mei watakuwa wameshakamilisha hatua zote zikiwepo bajeti na jinsi utekelezaji huo utakavyofanyika.
Awali Zulmira alieleza kuwa UNESCO ndiyo shirika la Umoja wa Mataifa ambalo linasimamia elimu na wao ndiyo wameandaa mpango huo wa ESDP na wataendelea kusaidia kukua kwa elimu nchini na hiyo ni moja kati ya kazi wanazozifanya katika kusaidia ukuaji wa elimu na kuifanya kuwa bora katika nchi mbalimbali ambazo shirika hilo wanafanya kazi.
3
Mkuu wa Ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikiaa Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues akielezea jambo katika kongamano la kujadili vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu (ESDP).
4
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo akizugumza kuhusu Mpango wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu (ESDP), Katikati ni Mkuu wa Ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikiaa Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues na kushoto ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Elimu, Clifford Tandari.
5
Mmoja wa wanakikundi akiwaelezea wanakikundi wenzake kuhusu kipaumbele ambacho walikuwa wamechaguliwa kukijadili na baadae kuwasilisha mbele ya washiriki wote jinsi kipaumbele hicho kitakavyotumika pamoja na faida zake.
7
Mkuu wa kitengo cha Ushirikiano wa Kiufundi kutoka Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kutoka Ufaransa, Anton De Grauwe akimuelekeza jambo mwana kikundi mwenzake wakati wa kongamano la kujadili vipaumbele vitakavyotumika katika Mpango wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu (ESDP).
8
Baadhi ya wanakikundi wakiwa makini kufuatilia kila jambo ambalo linaendelea katika kongamano hilo la siku mbili ili kupata vipaumbele ambavyo vitatumika katika Mpango wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu (ESDP).
9
10
11
Picha ya pamoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.