Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiizindua rasmi Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja { JMMK }hapo katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Mjumbe wa Kamati tendaji ya Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud akitoa muhtasari wa majukumu ya Jumuiya hiyo kabla ya kufanyika kwa uzinduzi rasmi.
Mwenyekiti wa Mkutano wa Tano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Haji Omar Kheir akijiandaa kumkaribisha Mgeni rasmi Balozi Seif kuizindua Jumuiya hiyo Hapo Bwawani Mjini Zanzibar.
Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja wakifuatilia Hotuba ya Mgeni rasmi kuizindua Jumuiya hiyo Balozi Seif hayupo pichani hapo Bwawani.
Baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja wakifuatilia Hotuba ya Mgeni rasmi kuizindua Jumuiya hiyo Balozi Seif hayupo pichani hapo Bwawani.
Balozi Seif akiagwa rasmi na Viongozi wa { JMMK } nje ya ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar mara baada ya Kuizindua rasmi Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Picha na –OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba njia pekee ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoukabili Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwemo kushuka kwa kiwango cha elimu, ukosefu wa ajira kwa Vijana pamoja na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Watoto na Wanawake ni nguvu za pamoja kati ya Viongozi na Wananchi wenyewe wa Mkoa huo.
Alisema Jamii yoyote ile isipokutana na kupanga jinsi ya kuendesha mambo yanayowagusa kamwe jamii hiyo haitaweza kupata mafanikio kwa jambo lolote lile mfano Elimu, afya au hata Kilimo.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiizindua rasmi Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja { JMMK } hapo katika Ukumbi wa Mikutano wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar.
Alisema Takwimu zinaonyesha wazi kwamba Mkoa wa Kaskazini Unguja unaongoza kwa kushuka kwa kiwango cha Elimu, vitendo vya udhalilishaji, uchafuzi wa mazingira na mpasuko wa Umoja unaosababishwa na tofauti za Kidini na Kisiasa ambazo zimepelekea kudidimia kwa hadhi na heshima ya Mkoa huo katika uso wa Zanzibar.
“ Mkoa wetu hivi sasa umevamiwa na watu ambao wanatumia dini na siasa kwa lengo la kuwagawa wananchi mambo ambayo kama hawakuwa makini watu hao wanaweza kuwaweka mahali pabaya Wananchi wa Mkoa huo ”. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kuwa kwa kipindi kirefu sasa Skuli za Mkoa wa Kaskazini Unguja hazifanyi vyema katika Mitihani yao ya Kitaifa hali inayotishia maendeleo ya Mkoa huo pamoja na Taifa kwa ujumla.
Balozi Seif aliitaka Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja { JMMK } kujipanga vizuri kimpango na Kimkakati kwa upande wa suala la kukuza kiwango cha Elimu ili Mkoa huo ujenge hadhi ya kuongoza kielimu Tanzania nzima.
Alisema ili malengo hayo yafanikiwe vyema Jumuiya hiyo inahitaji kuwa na mashirikiano ya hali ya juu na karibu zaidi kati ya Viongozi wake, skuli zote zilizomo ndani ya Mkoa, wazazi, Taasisi za Kijamii pamoja na wanafunzi wenyewe.
Balozi Seif alisema baadhi ya mambo ambayo Jumuiya hiyo inaweza kufikiria kuyatekeleza ili kukuza kiwango cha elimu ni pamoja na kuzifanyia kazi tafiti mbali mbali zilizoonyesha mapungufu ya kielimu pamoja na kushajiisha vijana wa Mkoa huo wenye Elimu ya juu kutenga muda wao wa Jumamosi na Jumapili kwa ajili ya kuwasaidia Vijana wenzao.
Akigusia suala la ajira hasa kwa Vijana wanaomaliza masomo yao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa Jumuiya hiyo kushajiisha watu wenye mitaji kufungua vituo vya kazi za Amali Mkoani huo ili kusaidia kupunguza wimbi kubwa la ajira katika eneo hilo.
Alifahamisha kwamba Vituo hivyo vya kazi za amali { Job Centre } vijengewe uwezo mkubwa wa utoaji wa mafunzo yatakayotoa fursa pana kwa vijana wanaojifunza kuwa na uwezo mpana wa kuajirika.
Alieleza kwamba Mkoa wa Kaskazini Unguja umebarikiwa kuwa na Miradi mingi ya Hoteli za Kitalii ambazo iwapo utakuwepo utaratibu mzuri wa mawasiliano kati ya Uongozi wa Jumuiya hiyo, Mkoa na wamiliki wa Hoteli hizo uwezekano wa kupata ajira kwa vijana watakaomaliza mafunzo ya vituo hivyo utakuwa mkubwa sana.
Hata hivyo Balozi Seif aliwanasihi na kuwaomba Vijana wanaomaliza masomo yao kuacha tabia ya kuchagua kazi kwani huu si wakati wa kufanya hivyo kutokana na tatizo hilo kubwa kwa hivi sasa limekuwa likiyakumba na kuyaathiri mataifa mbali mbali Ulimwenguni yakiwemo pia yale yaliyoendelea kiviwanda.
Kwa upande wa Dini na Siasa sehemu zinazoonekana kutumiwa vibaya wakati huu na hatimae kuleta mtafaruku ndani ya Jamii Balozi Seif aliwanasihi wanakaskazini wote kuendelea kuilinda hadhi ya Mkoa wao unaooneka kuyumba kutokana na mavamizi ya watu wanaopenda kugawa wananchi.
Alisema siasa na Dini sio mambo mageni ndani ya Mkoa huo yaliyoonekana kutoa nafasi pana kwa kizazi kilichopita kushiriki kikamilifu katika masuala yote mawili na kamwe hawakuwa tayari hata kidogo kuvunja umoja wao.
Alisema kizazi cha nyuma kiliishi na kupendana sambamba na kushirikiana katika mambo yao yote ya kijamii na hakukuwa na ndoa zilizovunjwa kwa sababu ya kisiasa kama jamii inavyoshuhudia kufanyika kwa vitendo hicho vibaya hivi sasa vinavyokwenda kinyume na Utamaduni pamoja na maadili ya Dini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi Mzima wa Wana wa Kaskazini Unguja kwa wazo lao la kuunda Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wao kitendo kitakachosaidia chachu ya kupatikana kwa maendeleo ya haraka ndani ya Mkoa huo.
Alisema Mikutano inayofanywa na kupatikana ndani ya jumuiya zinazoundwa na watu kutoka upande mmoja wa nchi kwa lengo la kujadili na kupanga mambo yatayosaidia kutatua changamoto zinazowakabili ni muhimu sana kwa maendeleo yao pamoja na hata kwa Taifa.
Akitoa muhtasari wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja Mjumbe wa Kamati Tendaji ya muda ya Jumuiya hiyo ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B” Ndugu Ayoub Moh’d Mahmoud Jecha alisema wazo la kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo limepata Baraka kutoka kwa Viongozi wakuu wa Kitaifa wenye asili na uzawa wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Nd. Ayoub alisema Kamati tendaji ya muda ililazimika kuunda kamati nyengine ndogo ndogo za Uchumi na Ustawi wa Jamii , Kamati ya Ustawi wa Jamii na ile ya Mkakati kwa dhamira ya kuurejeshea heshima yake Mkoa huo wa Kaskazini Unguja.
Mapema Mwenyekiti wa Mkutano huo wa Tano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Wanakaskazini Unguja Mh. Haji Omar Kheir alisisitiza umuhimu wa wanajumuiya hiyo kujitolea kwa nguvu zao zote ili lengo lililokusudiwa la kuundwa kwake lifanikiwe vyema.
Akizitaja baadhi ya changamoto zinazoendelea kuukumba Mkoa Huo Mh. Haji alisema kupotea kwa mila , silka na Utamaduni ndani ya jamii za wanakaskazini Unguja ndio chimbuko la kubuniwa kwa Jumuiya hiyo ya Maendeleo ya Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unaguja.
Mkutano huo wa Tano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ulifuatiwa na mada ya Uchumi na Ustawi wa jamii iliyotolewa na Mjumbe wa Kamati Tendaji wa Jumuiya hiyo Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud na kujadiliwa na walishiriki zaidi ya 980 kutoka Matawi yote 98 yaliyomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja { JMMK } imeshateua Wajumbe Watano waliounda Bodi ya wadhamini ambao ni Dr. Salmin Amour,Balozi Seif Ali Iddi, Bibi Fatma Bakari Moh’d, Mzee Ali Ameir Mohammed pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein aliyetunukiwa heshima hiyo na kukubali kuwa mwanachama wa Jumuiya.
No comments:
Post a Comment