Habari za Punde

Zanzibar Kuanzisha Kituo cha Mtandao wa Maeneo Yake Kusaidia Upotoshaji wa Taarifa.



Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar.
Idara ya Mipango miji na Vijiji Zanzibar kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Zanzibar wanatarajia kuanzisha Kituo cha Mtandao wa Taarifa za Maeneo na mazingira ya Zanzibar ambapo Wananchi watalazimika kupata taarifa kupitia kituo hicho.

Taarifa hizo zitawekwa katika mfumo wa kidigitali na kuwekwa katika Mtandao huo ili kuepusha upotoshaji wa taarifa na pia zipatikane kwa wakati bila ya usumbufu.

Mkurugenzi wa Mipango miji na Vijiji Zanzibar Dkt. Mohammed Juma ameyasema hayo wakati wa warsha ya kuandaa utaratibu wa kuanzisha kituo hicho cha Mtandao Shangani mjini Zanzibar.

Amefahamisha kuwa kutokana na kuwepo kwa Vyanzo vingi vya Taarifa zinazohusu Maeneo ya Zanzibar kunapelekea baadhi ya Taarifa hizo kutokuwa sahihi na kupelekea mkanyiko katika jamii.

“Kwa sasa kuna Vyanzo vingi vya kujua maeneo na mazingira ya Zanzibar..kwa mfano ukienda kutaka taarifa juu ya eneo fulani inawezekana taarifa hiyo ikatofautiana na Vyanzo vingine lakini tutakapokuwa na Chanzo kimoja taarifa zitakuwa moja na sahihi”Alisema Dkt Mohamed.

Ametaja faida zitakazopatikana kupitia Mtandao huo kuwa nipamoja na kuwarahisishia Wananchi kupata taarifa popote walipo na kwa wakati kinyume na ilivyo sasa ambapo hulazimka kwenda katika Taaisi husika jambo ambalo huwaletea usumbufu.

Aidha amesema pia itakuwa ni sehemu ya uwazi kwa Serikali kupitia Taasisi zake ambapo kila kitu kitawekwa wazi na kupatikana kirahisi kupitia Mtandao huo.

“Mtandao huo utaweka wazi maeneo yote yakiwemo,Makaazi,maeneo ya uwekezaji..isipokuwa yale yakiusalama ili kumrahisishia mwananchi kuweza kupata Taarifa bila kuhangaishwa huku na kule” alibainisha Dkt Mohammed.

Aidha amebainisha kuwa katika Warsha ya kuandaa Mtandao huo Taasisi nane zimeshiriki ili kuwa na sauti moja juu ya maeneo na mazingira ya Zanzibar.

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Mamlaka ya usimamizi wa ardhi, Idara ya Mazingira, Idara ya Misitu na maliasili zisizorejesheka na idara ya maendeleo ya uvuvi.

Taasisi zingine ni pamoja na Idara ya Rasilimali za baharini, Chuo kikuu cha taifa SUZA na Mamlaka ya Mazingira Zanzibar (ZEMA) ambazo zote zimeshiriki katika Mpango huo wa kuandaa Taarifa za pamoja.

Jumla ya shilingi Milion 140 zitatumika kuanzisha Kituo hicho cha Mtandao ambazo ni msaada kutoka Serikali ya Finland.

Kwa upande wake Mwezeshaji wa mafunzo kutoka Taasisi ya Mazingira ya Finland Bi Riihz Teinirants amesema Taasisi watendaji wa Taasisi hizo walioshiriki mafunzo wanajukumu la kuwafahamisha wenzao ili kutimiza lengo lililokusudiwa.

Aidha bi Riihz amesema mbali na kutoa mafunzo ya kuanzisha Kituo hicho cha Mtandao wataisaidia Zanzibar kutafuta taarifa za maeneo yake na kuziweka katika Kituo hicho hasa zile za mwambao wa bahari ili kuleta ufanisi unaohitajika.

Kunzishwa kwa kituo hicho cha Mtandao wa Taarifa za maeneo ya Zanzibar ni matokeo ya kukamilika kwa Mradi wa kutunza mazingira Zanzibar (SMOLE) uliofadhiliwa na Serikali ya Finland katika kuisaidia Zanzibar ambapo Mradi huo ulipata mafanikio makubwa.

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.