6/recent/ticker-posts

OMO aongoza Kikao cha Kamati Kuu ACT Wazalendo Dar




Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Mhe. Othman Masoud Othman, amesisitiza kuwa chama hicho hakipo kwa ajili ya kushiriki chaguzi pekee, bali ni chombo cha ukombozi, mageuzi, na maendeleo ya Taifa kwa maslahi ya wananchi wote.
Mhe. Othman ameyasema hayo leo, Januari 18, 2026, wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, kinachofanyika katika Ukumbi wa Hakainde Hichilema, uliopo katika Jengo la Maalim Seif, Makao Makuu ya ACT-Wazalendo Magomeni jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia ushiriki wao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Mhe. Othman amebainisha kuwa ACT-Wazalendo iliingia uwanjani ili kuidhihirishia dunia juu ya ukosefu wa utayari wa kidemokrasia nchini.
"Tunajua viongozi wenzetu hawajawa na dhamira njema ya kuongoza nchi, hii imeonesha vyema kuna kiwango kikubwa cha kukosa demokrasia, kiwango kikubwa cha kukosa Viongozi bora na namna taasisi zetu za kusimamia uendeshaji wa nchi zilivyofikishwa na nchi yenyewe ilipofika, haya tumeyaona baada ya kushiriki Uchaguzi huu". Ameeleza huku akisisitiza dhamira yao.
"Kwetu sisi, hatuwezi kukaa kimya; ni lazima tuingie katika mapambano ya kuitafuta haki ya watu wetu, na tayari zipo hatua mbali mbali tunazoendelea kuzichukua," alisema Mwenyekiti huyo.
Aliongeza kuwa miongoni mwa hatua hizo ni kuhakikisha chama kinaendelea kuwa hai na imara, huku kikijielekeza katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za haki za binadamu na kusimamia kuheshimiwa kwa maamuzi ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Othman ametoa pole kwa wanachama na Watanzania kwa ujumla kufuatia changamoto zilizojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, zikiwemo vifo na vitendo vya manyanyaso dhidi ya raia.
Amewataka wajumbe wa Kamati Kuu kuwa watulivu na makini katika kujadili ajenda zilizopo ili kutengeneza njia na mustakabali bora wa Taifa, akisisitiza kuwa ACT-Wazalendo ndilo tumaini lililobaki kwa Watanzania.
Kikao hiki cha Kamati Kuu ni cha kwanza kufanyika tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, na kimebeba ajenda nzito zikiwemo, Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, Taarifa ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na Tathmini ya kina ya hali ya kisiasa nchini.
Aidha, kikao hicho kinatarajiwa kutoa maazimio na msimamo rasmi wa chama kufuatia mwenendo wa sasa wa kisiasa nchini. Viongozi mbalimbali wamehudhuria kikao hicho, akiwemo Kiongozi wa Chama, Bi. Dorothy Semu.


 

Post a Comment

0 Comments