6/recent/ticker-posts

Waziri wa Fedha na Mipango afanya mazungumzo na watendaji wa Benki Kuu ya Tanzania Ofisi ya Zanzibar




Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema nchi inategemea kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato ya ndani hususan yatokanayo na kodi, ambayo hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkk Juma Malik Akil, aliyasema hayo wakati akizungumza na watendaji wa Benki Kuu ya Tanzania Ofisi ya Zanzibar mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea makao makuu ndogo Kinazini.
Alisema mapato hayo ni mhimili muhimu katika uendeshaji wa shughuli za serikali na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Dkt. Juma alisema tafiti zilizofanywa na wataalamu kutoka Tume ya Mipango zimebaini kuwa Zanzibar inapoteza zaidi ya asilimia 83 ya mapato ambayo ingeweza kuyakusanya endapo kungekuwa na mifumo imara na ya kisasa ya ukusanyaji wa mapato.
Alibainisha kuwa upungufu huo unatokana na kutokuwepo kwa mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato, hali inayosababisha serikali kukusanya takribani asilimia 17 tu ya uwezo wake halisi.
Aidha alisema endapo mifumo ya kidijitali itatumika kikamilifu, kuna uwezekano mkubwa wa kufikia asilimia 100 ya makusanyo, hivyo kuziba pengo la upotevu wa mapato unaofikia asilimia 83 ambayo kwa sasa nchi inashindwa kuyakusanya na nchi inapoteza mapato yake.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa uchumi wa kidijitali, alisema ni lazima sekta ya fedha ihakikishe kila senti inayopaswa kukusanywa inakusanywa ipasavyo na kuelekezwa katika malengo yaliyokusudiwa, yakiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida ya serikali ili kuleta tija kwa wananchi wanaoitegemea serikali yao.
Alibainisha kuwa matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali yataiwezesha nchi kujenga miradi mikubwa ya maendeleo bila kutegemea kwa kiasi kikubwa mikopo.
Dkt. Juma alisisitiza kuwa ni lazima nchi iendelee kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo hususan ile ya kimkakati, akibainisha kuwa mapato ya ndani yakikusanywa ipasavyo yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi kwa ujumla.

 

Post a Comment

0 Comments