STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 8.2.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa
licha ya mafanikio yaliopatikana katika sekta ya kiuchumi, kijamii na kisiasa
kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya ustawi wa wanawake bado jitihada za pamoja
zinahitajika katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake hao.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inatambua mchango wa wanawake katika kuijenga Zanzibar
kabla na baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 na ndio maana katika
kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi hayo miongoni mwa waliotunukiwa nishani
walikuwa ni wanawake ambao wamefanya mambo makubwa ya kukumbukwa katika
historia ya maendeleo ya Zanzibar.
Aliyasema hayo katika hotuba yake
iliyosomwa kwa niaba na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo
Mhe. Bi Hindi Hamad Khamis katika madhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
yaliofanyika katika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani Zanzibar yalioenda
sambamba na Usiku wa Taasisi ya Bibi Siti Binti Saad.
Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema
kuwa mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika mapambano dhidi ya unyanyasaji
wa kijinsia, maradhi thakili yanayowasibu wanawake, kuongeza jitihada katika
kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi, kupunguza mimba za utotoni pamoja na
kuimarisha upatikanaji wa fursa na haki mbali mbali.
Dk. Shein alisema kuwa hatua ya maendeleo
iliyofikiwa hivi sasa ni matokeo ya jitihada kubwa zinazofanyika kwa pamoja,
bila ya kujali jinsia, kupanga na kutekeleza mambo mbali mbali huku akitumia
fursa hiyo kuipongeza Taasisi ya Siti Binti Saad kuona umuhimu na mchango wa
wanawake katika jamii na kuamua kuwapa tunzo katika hafla hiyo.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inatambua
kuwa itakuwa bora zaidi katika kupanga na kutekeleza mipango yetu ya maendeleo
ikiwa kila mwananchi atapewa fursa na haki sawa ya kushiriki katika kupanga na
kutekeleza mipango hiyo ya maendeleo”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa katika
kipaindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imetekeleza mambo mbali mbali katika sekta za kiuchumi na kijamii kwa lengo la
kuimarisha maendeleo na ustawi wa wanawake pamoja na watoto.
Dk. Shein alisema kuwa katika jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi,
Serikali imeziimarisha fursa za upatikanaji wa mikopo kwa wanawake kupitia
mifuko mbalimbali ya uwezeshaji iliyokuwepo kabla na iliyoanzishwa hivi
karibuni.
Kadhalika Dk. Shein alisema kuwa usawa wa
kijinsia katika uteuzi na uchaguzi wa nafasi katika ngazi mbali mbali
unazingatiwa na kueleza kuwa hadi
kufikia tarehe 13 Agosti mwaka jana alipolivunja Baraza la Wawakilishi lilikuwa
na wajumbe 81 kati ya hao wajumbe wanawake walikuwa ni 27 sawa na asilimia 33
kiwango ambacho hakijafikiwa na nchi nyingi duniani.
Akieleza mafanikio mengine ya wanawake
Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake kuona kwa mara ya kwanza, Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imepata Makamu wa Rais mwanamke Mhe. Samia Suluhu Hassan
ambapo pia, wagombea wawili kati ya watatu waliopitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM
kugombea nafasi ya Urais kwa tiketi ya CCM walikuwa wanawake.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Dk. Shein alisema
kuwa Serikali imeimarisha fursa za elimu ya juu kwa wanawake sambamba na
kuimarisha utoaji wa mafunzo katika Skuli ya Sekondari ya Wawanwake, BenBella
na Utaani, ambazo zimeimarishwa zikiwa na lengo la kuwasaidia wanafunzi wa kike
waweze kufaulu kwa wingi na kuweza kujiunga katika vyuo vikuu vya ndani na nje
ya nchi.
Dk. Shein akieleza kuhusu sekta ya afya,
alisema kuwa kwa upande sekta hiyo, Serikali imeimarisha huduma za wanwake na
watoto katika vituo vya afya na katika hospitali zote za Zanzibar huku akitilia
mkazo agizo alilolitoa mwezi Mei 2012 kwamba wanwake wote wanaojifungulia
hospitalini wapatiwe huduma za uzazi bila ya malipo yoyote.
Katika jitihada za kupambana na
udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, Dk. Shein alisema kuwa
Serikali ilianzisha Kampeni dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia tarehe 6, Disemba,
mwaka 2014, kampeni ambayo imesaidia sana katika kutoa mwamko wa kupambana na
vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto.
Nao uongozi wa Taasisi ya Bibi Siti Binti
Saad ukiongozwa na Mwenyekiti wake Bi Nasra Mohammed Hilal ulieleza mafanikio
ya Taasisi hiyo sambamba na kueleza kujuhudi zilizochukuliwa na akina mama
katika kuiletea maendeleo Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla.
Hafla hiyo ya kuadhimisha siku ya wanwake
duniani iliyoenda sambamba na usiku wa Taasisi ya Bibi Siti Binti Saad tumbuzo
mbali mbali zilitumbuiza katika usiku huo ikiwa ni pamoja na ngoma za asili ikiwemo ngoma ya Rubamba na taarab ya
kikundi cha Raahat Zamaan.
Katika kikundi cha taarab cha Raahat
Zamaan ambacho kiliupamba usiku huo, kirembwe cha Bibi Siti Binti Saad akiwa na
wasanii wenziwe waliburudisha na kuwakumbusha nyimbo za mkongwe huyo ambazo
zilitia fora wakati wa uhai wake hadi hii leo bado zinaendelea kungara.
Sambamba na hayo, akina mama mbali mbali
walikabidhiwa zawadi kutokana na ushiriki wao katika kuiletea maendeleo
Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla, zawadi zilizotolewa na Taasisi hiyo
akiwemo Mama Fatma Karume, Bibi Siti Binti Saad, Bibi Johari Yussuf Akida, Bi
Mtumwa Fikirini, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mhe. Asha Rose Migiro, Mhe. Anna
Makinda, Mhe.Khadija Aboud, Zainab Himid, Bi Fatma Aloo, Bi Rufea Juma Mbarouk,
Mhe. Amina Salum Ali, Bi Jogha Mohammed, Tatu Ali na wengineo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment