Habari za Punde

Balozi Seif atoa msaada kwa Kikundi cha Ushirika cha Msitupumbaze, Mangapwani

 Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi mchango wa Shilingi Milioni 1,000,000/- kwa Mshika Fedha wa Kikundi cha Ushirika cha Msitupumbaze cha Mtaa wa Kiduka Njaa Mangapwani Bibi Asha Muhsin Hassan zitakazosaidia kukamilisha jengo lao la ufugaji wa mbuzi wa maziwa.

Anayepiga kofi kati kati ni Katibu wa Kikundi hicho Bwana Haji Hoja Haji, aliyeko nyuma yake kushoto aliyevaa fulana manjano Mlezi wa Kikundi hicho Bwana Hassan Ibrahim Khamis na nyuma ya Katibu huyo kulia yake aliyevaa kofia ya kiua ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Nd. Issa Juma.
Mlezi wa Kikundi cha Ushirika cha Msutupumbaze aliyevaa fulana rangi ya manjano Bwana Hassan Ibrahim Khamis akimueleza Balozi Seif  mfumo wa Kitaalamu utakaotumika katika kuendelez mradi wa ufugaji Mbuzi wa Maziwa hapo Mangapwani Wilaya ya Kaskazini B Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Picha na - OMPR – ZNZ. 

Na Othman Khamis, OMPR

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba uwamuzi wa Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini wa kuanzisha vikundi vya ujasiri amali  ni wa busara na hekima kwa vile unasaidia nguvu za Wananchi hao katika muelekeo wa kupunguza au kuondosha kabisa umaskini.

Alisema uamuzi huo wa miradi ya uzalishaji unaoongeza pia kipato chao cha kila siku umekuwa ukihimizwa ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi { CCM } ya Mwaka 2015 – 2020  iliyonadiwa mwaka 2015 na kupata ridhaa ya Wananchi katika kuongoza Dola ya Tanzania. 

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza hayo wakati akikabidhi mchango wa Milioni 1,000,000/- Taslim kwa Kikundi cha Ushirika cha Msitupumbaze cha Mtaa wa Kiduka Njaa katika Kijiji cha Mangapwani kinachoendelea na maandalizi ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa Mbuzi wa Maziwa.

Akihamasishwa na ari ya Wananchi hao ya kuanzisha mradi huo muhimu kiuchumi Balozi Seif  akawaahidi wanakikundi hao mchango mwengine wa Shilingi Milioni Moja mapema Wiki ijayo, Mifuko 10 ya Saruji pamoja na Gari moja ya Kokoto.

Mwakilishi huyo wa Jimbo  la Mahonda aliwapongeza wanaushirika hao mchanganyiko kwa juhudi walizochukuwa za kupambana na umaskini na kuwaeleza kwamba atafanya jitihada za ziada kwa kushawishi Wataalamu wa Sekta ya Mifugo ili kuwapatia mafunzo yatakayowasaidia kufuga kitaalam na kupata faida zaidi.

Mapema Mlezi wa Kikundi hicho cha Ushirika cha Msitupumbaze Mangapwani Bwana Hassan Ibrahim Khamis alisema mradi huo wa ufugaji Mbuzi wa Maziwa  ni wa pili Barani Afrika ukitanguliwa na ulionzishwa Nchini Rwanda na kupata ufadhili wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo { IFAD } chini ya usimamizi wa Shirika la Huduma za Kilimo la Kimataifa {ASP }.

Bwana Ibrahim alisema kila familia ililengwa kupata mbuzi wawili katika harakati za awali za mwanzo wa mradi huo ambapo baadae ikaamuliwa uendeshwe kwa mpango wa ushirika.

Alisema inakuwa rahisi kwa wataalamu wa Mifugo kutenga muda maalum wa kutoa mafunzo ya pamoja kwenye vikundi vya ushirika  badala ya mtu mmoja mmoja sambamba na kuimarisha huduma za chanjo na tiba ya mifugo.

Mlezi huyo wa Msitupumbaze alifahamisha zaidi kwamba mbuzi  watakaozaliwa ndani ya mradi huo katika kipindi cha miaka Mitano  chini ya usimamizi wa wataalamu wa Mifugo watagaiwa kwa vikundi vyengine vitakavyoanzishwa hapo baadaye.

 Mapema akitoa Taarifa fupi ya Historia ya Kikundi hicho cha Ushirika cha Msitupumbaze  Mangapwani Katibu wa Kikundi hicho Ndugu Haji Hoja Haji alisema wanaushirika hao hivi sasa wanaendelea na harakati za kukamilisha jengo la kuhifadhia mifugo hiyo.

Nd. Hoja alisema mzao wa kwanza wa Mbuzi hao wa Maziwa 48 wanakaopewa kutoka  Shirika la Kimataifa la Huduma za Kilimo { ASP } utagaiwa kwa Wanakijiji kwa lengo la kujiendeleza Kimifugo.

Kikundi cha Ushirika cha Msitupumbaze cha Mtaa wa Kiduka Njaa katika Kijiji cha Mangapwani umeasisiwa mnamo Tarehe 25 mwezi Agosti mwaka 2008 ukiwa na wanachama 20 mchanganyiko.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.