Habari za Punde

Wadau Watakiwa Kusimamia Kwa Kina Kujadili Sera ya Uvuvi wa Bahari Kuu Tanzania.

Na Abdi Shamnah
WASHIRIKI wa mkutano unaojadili rasimu ya Sera ya Taifa ya usimamizi wa uvuvi wa bahari kuu Tanzania, wametakiwa kujadili rasimu hiyo kwa kina, ili kufanikisha dhamira za serikali, za kuwa na sera madhubuti itakayoweza kusimamia vyema uvuvi wa bahari kuu.
Changamoto hiyo imetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu (anaeshugulikia mifugo na uvuvi), Dk. Islam Seif, katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa uvuvi, unaojadili rasimu ya sera ya Taifa ya usimamiziwa  uvuvi wa bahari kuu, uliofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ulioko Fumba.
Mkutano huo umewahusisha wadau  na wataalamu wa sera na watafiti kutoka taasisi za serikali na asasi za kiraia, ikiwemo idara ya Uvuvi, Mazingira,vyama vya mabaharia, ZMA, SUMATRA, TPA, ZPC,  wamiliki wa viwanda vya kusindika samaki, vyuo vya uvuvi na NGO mbali mbali.
Alisema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, zina matarajio makubwa kuwa mkutano huo utatoka na sera madhubuti itakayoweza kusimamia vyema uvuvi wa bahari kuu, ili kuleta tija ya kijamii na kiuchumi kwa taifa na wananchi wake.
Alisema ni jukumu la wadau hao kujadili kwa kina rasimu hiyo ili kufikia malengo ya kuanzishwa  Mamlaka hiyo yenye azma ya kukuza, kusimamia na udhibiti uvuvi  wa bahari kuu.
Aidha aliwataka wadau hao  kuzingatia mambo ya msingi yatakayoipa sifa sera hiyo, ikiwemo uimarishaji uwezo wa kifedha, miundombinu na uhifadhi wa mazingira ya ukanda wa kiuchumi.
‘‘Sera inapaswa kuzingatia utekelezaji wa mipango ya usimamizi wa uvuvi, leseni ziendane na rasilimali zinazovunwa pamoja na kuhakikisha kunakuwepo ushirikishwaji wa wazawa katika uvuvi wa bahari kuu’’, alisema.
Dk. Islam alibainisha kuwa katka kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda, kuna haja ya kuzingatia upatikanaji wa ajira kupitia viwanda na masoko.
‘’ Lakini pia sera iainishe fursa zilizopo katika uanzishaji wa aina nyengine za uvuvi, sambamba na namna ya kujenga mawasiliano na kumarisha  mashirikiano na sekta nyengine za kiuchumi’’, alisema.  
Nae, Mshauri mwelekezi Dk. Indu, ambae anashirkiana na serikali kuandaa  sera hiyo, aliishukuru Serikali kwa mashirikiano yake yenye lengo la kukamilisha sera hiyo.
Alisema kukamilika kwa sera hiyo, kutaiwezesha mamlaka  kusimamia na kudhibiti vyema uvuvi katika ukanda huo wa kiuchumi, hivyo kukidhi mahitaji ya wananchi kijamii na kiuchumi.
Aidha alisema itafanikisha malengo ya serikali ya kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025, sambamba na dira ya kupambana na umasikini.
Mamlaka ya Usimamizi wa uvuvi wa bahari kuu, ilianzishwa mnamo 2010 na tangu hapo bado haijawa na sera yake.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.