Habari za Punde

Mama Mwanamwema Shein, Amewataka Kinamama Kutembea Kifua Mbele Kuyatangaza Mafanikio Yaliopatikana Zanzibar.

MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein amewataka akinama na viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kutembea kifua mbele kwa lengo la kuyatangaza mafanikio yaliopatikana hapa nchini hasa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Mama Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Ofisi za CCM Mkoa wa Amani Kichama  zilizopo mjini Unguja, wakati akizungumza na akinamama, viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) wa Mkoa wa Mjini Kichama kwa lengo la kuwasalimia na kuwashukuru kwa kuendelea kuiunga mkono CCM, na hatimae kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliopita.

Katika hotuba yake, Mama Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mambo mengi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wake ambapo miongoni mwa hayo ni suala zima la elimu bila ya malipo, utoaji wa pencheni jamii kwa wazee kuanzia miaka 70 na kuendelea, kuondosha malipo kwa akinamama wanaojifungua katika hospitali za Serikali.

Mengine ni pamoja na kulipia ada ya mitihani wanafunzi wa Sekondari pamoja na uimarishaji wa huduma ya afya ya  Mama na Mtoto ambapo Dk. Shein hivi karibuni aliyafungua majengo mapya huko katika hospitali ya Mnazi Mmoja ambayo yamesheheni vifaa vya kisasa na lengo likiwa ni kutoa huduma bora za afya.

Kwa mnasaba huo, Mama Shein pamoja na ujumbe wake aliofuatana nao wakiwemo wake wa viongozi na Wabunge na Wawakilishi walitoa pongezi zao za dhati kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri, viongozi wa Chama na Serikali pamoja na watendaji wote kwa kutekeleza mipango na shughuli zilizomo katika Ilani ya CCM.

Aidha, Mama Shein alieleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kueleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la upungufu wa maji safi na salama katika maeneo ya mjini.

Hivyo, Mama Shein alitoa wito kwa viongozi na wananchi kuendelea kuwa na subira  na kushirikiana na serikali yao katika kufanikisha  mipango ya maendeleo.

Mama Shein, ambaye katika ziara yake hiyo amefuatana na viongozi mbali mbali wakiwemo Wabunge na Wawakilishi wa Viti maalum pamoja na wake wa Wabunge na Wawakilishi, alitumia fursa hiyo kusisitiza suala zima la amani  

Pia, Mama Shein alitoa nasaha zake kwa viongozi, akinamama na wanajumuiya ya UWT na kuwataka kushirikiana  na vyombo vinavyohusika kuwaripoti watu wanaobaimika kufanya vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.

Wakati huo huo, Mama Shein aliwakabidhi kadi za Jumuiya ya UWT wanachama wapya 42 waliojiunga na Jumuiya hiyo.

Mapema Mama Asha Balozi, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka viongozi wa UWT kupenda kukosolewa na kuwataka kuzidisha mashirikiano na kusikiliza mawazo ya watu waliochini yao kwani huo ndio uongozi. Aidha, Mama Asha, alipingana na wale wote wanaosema kuwa hakuna maendeleo.

Pamoja na hayo, Mama Asha aliwataka akinamama hao kujipanga vizuri katika suala zima la kuwalea watoto wao sambamba na kutambua nyendo zao hasa nyakati za usiku huku akiwasisitiza haja ya kuzidisha mapenzi miongoni mwao.  

Nae, Mama Fatma Karume alitumia fursa hiyo kutoa historia ya kudai uhuru wa Zanzibar na jinsi wanawake walivyoshiriki katika mapambano hayo.

Aidha, Mama Fatma Karume  aliishauri Serikali kuwawekea watoto wadogo muda maalum wa kutembea nyakati za usiku kutokana na kuepuka vitendo viovu ambavyo wanaweza kufanyiwa.   

Katika risala yao UWT Mkoa wa Mjini, walimpongeza Dk. Shein kwa kuwateua akinamama wengi katika Serikali anayoiongoza na kutoa shukurani kwa wanajumuiya ya UWT Mkoa wa Mjini kwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi Mkuu wa marudio. 

Akinamama hao, walimpongeza Dk. Shein kwa kutia saini hadharani Mswada wa Sheria ya utafiti na uchimbaji wa Mafuta na Gesi Zanzibar, na kumpongeza kwa kitendo chake hicho cha kishujaa huku wakisisitiza haja ya kuendeleza ushirikiano ndani ya chama chao ili kizidi kuleta mafanikio zaidi. Aidha, viongozi hao walijinasibu kwa mashirikiano na maendeleo waliyonayo.


Mama Shein alianza ziara hizo za shukrani katika Mikoa ya Pemba mnamo Novemba 5 hadi 8 mwaka huu na kuendelea katika Mikoa ya Unguja kuanzia Novemba  21 na kumalizia hii leo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.