Habari za Punde

Makabidhiano ya Taasisi za Elimu Zanzibar

suza

CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mnamo tarehe 16 Oktoba, 2016 Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliidhinisha kuunganishwa kwa baadhi ya Taasisi za Elimu Zanzibar kuwa chini ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kwa kusaini Sheria namba 7 ya mwaka 2016 iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Chini ya Sheria hiyo, Taasisi ya Uongozi wa Fedha Zanzibar (ZIFA), Chuo cha Taaluma za Afya (CHS), na Taasisi ya Maendeleo ya Utalii Zanzibar (ZIToD) zote kwa pamoja zinaunganishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na kufuta Sheria zilizoanzisha taasisi hizo. 
Aidha Sheria hiyo imeifanyia marekebisho Sheria Namba 11 ya mwaka 2009 ambayo nayo iliirekebisha Sheria Namba 8 ya 1999 ambayo ndio ilianzisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar.
Kufuatia kuidhinishwa kwa Sheria hii na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Jumatatu ya tarehe 16 Januari, 2017 mnamo saa 4.00 za asubuhi huko katika Kampasi ya SUZA ya Tunguu, Mkoa wa Kusini, Unguja kutakuwa na makabidhiano rasmi ya taasisi zilizotajwa kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar. 
Makabidhiano hayo yatafanywa na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara za Elimu na Mafunzo ya Amali; Fedha na Mipango; Afya; na Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo. Taasisi zinazounganishwa zilikuwa chini ya Wizara zinazoongozwa na Mawaziri hao.
Taasisi hizo zikiwa chini ya mwamvuli wa SUZA zitaendesha shughuli zake kama kawaida lakini zikiwa na majina mengine ambapo iliyokuwa ZIFA sasa itakuwa ni Skuli ya Biashara, CHS itakuwa chini ya Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba ambapo ZIToD itakuwa ni Taasisi ya Maendelo ya Utalii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.