Habari za Punde

ZAECA yapiga kambi: Upotevu wa mapato Bandari ya Mkoani

Na Mwandishi wetu.

Mdhamini wa Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu wa uchumi Zanzibar (Zanzibar Anti-Corruption And Economic Crimes Authority - ZAECA) afisi ya Pemba Bw: Suleiman Ame Juma amewatoa hofu wananchi kisiwani Pemba wale wanaotumia usafiri wa majini kua mamlaka hiyo kuwepo katika bandari ya Mkoani sio kwa lengo la kuwazuia abiria wasisafiri kama inavyodaiwa na baadhi ya watu na badala yake wapo kwaajili ya kudhibiti vitendo vya rushwa, ulanguzi wa tiketi na upotevu wa mapato ya serekali unaonekana kukithiri bandarini hapo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi afisini kwake huko Chakechake mkoa wa kusini Pemba mdhamini huyo amesema kua, kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) kifungu cha “13" kinatoa ruhsa kwa mamlaka hiyo popote pale kunapokua na mwanya wa Rushwa au Uhujumu wa Uchumi kwenda kudhibiti hali hiyo kwa lengo la kuokoa hasara zitokanazo na matendo hayo maovu.

Amesema kutokana na taarifa ilizozitapa ya hali mbaya ya ulanguzi wa tiketi, upotevu wa mapato pamoja na baadhi ya abiria kupandishwa katika meli bila ya kuwa na tiketi Mamlaka ndipo ilipoamua kwenda kufunga kambi katika bandari hiyo ili kuhakikisha kua serekali haipotezi mapato yake na kuzuia ulanguzi wa tiketi

“hali ilikua mbaya sana bandarini hapo, utaona watu wanakuja bila ya tiketi ukimuuliza anakwambia ameambiwa aje atalipia pesa bandarini hapo na kuingia ndani ya meli, kuna baadhi ya watendaji wasio waaminifu wanaingiza watu ndani ya meli bila ya kua na tiketi, hili si jambo la kustahamiliwa kwa sababu licha ya kuikosesha serekali mapato lakini pia hupelekea meli kuingizwa abiria waliozidi idadi ya uwezo wa meli husika na kusababisha hatari kwa wanao safiri” alisema mdhamini huyo.

Akizungumza kwa masikitiko Juma amesema kua, katika hali ya kuhuzunisha kumekua na baadhi ya watendaji wasiokua waaminifu hutumia nafasi zao vibaya kupitisha abiria jambo ambalo ni kosa sheria.

Akizungumzia suala la uuzaji wa tiketi amesema, kisheria tiketi zinatakiwa kuuzwa na wahusika tu walioajiriwa na kampuni au shirika linalomiliki meli au boti na si kinyume na hivyo na itakua ni kwenda kinyume na sheria iwapo kutajitokeza watu watakaouza tiketi hali ya kua si wahusika halali, hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“baada ya kufanya tafiti tumegundua kua kuna mtu anazinunua tiketi mapema sana, abiria akifika afisini anaambiwa zimemalizika apo apo anafatwa na mtu anauziwa tiketi ile ile kwa bei ya juu hali hii haikubaliki, maana kufanya hivi ni ulanguzi na kunawanyima haki wananchi wa kawaida au abiria wakiingizwa ndani ya meli bila ya tiketi na kulipia pesa mkononi, kwa msingi huo abiria wakilipia pesa mkononi ZRB na Mamlaka ya Usafiri Baharini itashindwa kukusanya kodi kwa sababu taasisi hizo hukusanya kodi kwa kupitia vishina vya Tiketi .

Aidha mdhamini amewataaka wananchi wa kisiwa cha Pemba kuepuka tabia ya kutaka kusafiri kupitia ahadi za mtendaji au yeyote alieahidi kumsaidia kumpandisha bure kwenye meli bandarini hapo akisema kua hivyo ni kinyume na utaratibu , kila mmoja anatakiwa kununua tiketi iliyohalali ili kusafiri pasi na usumbufu wowote.

Amesema tokea 04/01/2017 wapo bandarini hapo na wataendelea kuwepo mpaka pale hali itakapotengemaa huku akitilia mkazo zaidi kwa abiria waache kununua tiketi kwa wasiokua wahusika ili kuepusha kufanyiwa ulanguzi na kuepuka usumbufu wakati wa kusafiri, pia amewaomba wananchi wakienda kununua tiketi waende na vitambulisho ili jina liende sambamba kama lilivyojitokeza katika kitambulisho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.