STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 15.05.2017
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewatembelea
na kuwapa pole wananchi wa maeneo mbali mbali kisiwani Pemba kufuatia maafa
yaliotokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha ambazo zimeathiri baadhi
ya makaazi ya wananchi, mazao pamoja na
miundomninu ya barabara na madaraja kisiwani humo.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika ziara yake aliyoifanya katika maeneo mbali mbali Kisiwani Pemba
ambayo yameathirika na mvua hizo za masika zinazoendelea kunyesha na kutumia fursa hiyo kuwafariji
wananchi hao pamoja na kuwapongeza kwa moyo mkubwa waliouonesha wa kusaidiana
na kustiriana katika kipindi hicho kigumu.
Miongoni mwa maeneo aliyoyatembelea Dk. Shein katika
ziara yake hiyo ni Mchanga wa Kwale, Chamanangwe, Bugujiko, kuungoni, Gando na
Pujini kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na Mgagadu Kiwani, Chonga, Kipapo,
Changaweni Mkoani, Ghala la karafuu la ZSTC Mkoani pamoja na Makombeni kwa
upande wa Mkoa wa Kusini Pemba.
Katika ziara yake Dk.
Shein alieleza kusikitishwa na kuhuzunishwa na athari hizo zilizotokea lakini
hata hivyo alitoa pongezi zake kwa wananchi kwa mashirikiano waliyoyaonesha
katika kipindi hicho, uongozi wa Mkoa na Wilaya zote za Pemba, uongozi na
wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi , Mawasiliano na Usafirishaji pamoja
na vikosi vya SMZ vilivyosaidia katika juhudi za kupambana na athari hizo.
Dk. Shein katika ziara
yake hiyo aliwaeleza wananchi kuwa Serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar iko
pakoja na wao na itaendelea kuwapa kila msaada unaohitajika na kuwataka
kuendelea kwua na uvumilivu na subira na kutomlaumu mtu ama kuhamaki kwa tukio
hilo ambalo ni shani ya Mwenyezi Mungu.
Dk. Shein alipata fursa
ya kuiona familia ambayo nyumba yao iliangukiwa na mbuyu ambayo ndani mlikuwa
na familia ya watu wanane wakati wa usiku lakini wote walikuwa salama huko
katika maeneo ya Gando Kilimajuu na kuifariji na kuahidi kuwa Serikali itatoa
msaada wake mkubwa ikiwa ni pamoja na kuijenga nyumba hiyo ambapo familia iyo
ilimpongeza Dk. Shein kwa hatua yake ya kwenda kuwaona.
Akiwa katika eneo la
Bugujiko akizungumza na wananchi waliathirika baada ya nyumba zao kuingia maji
katika eneo hilo Dk. Shein alisema kuwa tatizo hilo linamnasaba na mvua hivyo
aliwaahidi wananchi kuwa Serikali itajenga msingi wa maji katika eneo hilo ili
kuondosha kabisa athari kama hizo wakati wa mvua kwani uwezo huo upo.
Aidha, Dk. Shein akiwa
Kipapo kwenye barabara ya Kipapo Mgelema ambapo miundombinu ya barabara na
daraja imeathirika, Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa eneo hilo kuwa azma ya
Serikali ya kuijenga barabara hiyo pamoja na barabara nyengine alizoahidi
ambazo hutoa mazao kwa wingi likiwemo zao la karafuu, azma hiyo ipo na barabara
hizo zitaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami pamoja na madaraja yake yote ili
kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Aliwapa pole wananchi wa
eneo hilo na kuwathibitishia kuwa Serikali ipo pamoja nao huku akiwakubalia
ombi lao la kujengewa skuli ya chekechea na kuuagiza uongozi wa Mkoa wa Kusini
Pemba kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali ili kwenda kuliona
eneo walilolitayarisha wananchi hao kwa ajili ya ujenzi huo na kama litaruhusu
basi Serikali itajenga hadi skuli ya msingi.
“Hakuna dhiki wa dhiki
bali baada ya dhiki ni faraja…basi wananchi endeleeni na subira”,alisema Dk.
Shein.
Akiwa katika ghala la
karafuu la ZSTC Mkoani, Dk. Shein alipata maelezo ya athari zilizotokea kutoka
kwa Afisa Mdhamini wa Shirika hilo Abdalla Ali Ussi ambaye alisema kuwa kabla
ya athari hizo ghala hilo lilikwua na karafuu kavu gunia 527 sawa na tani 23.7
kwa thamani ya TZS milioni 332.0 ambapo kwa bahati nzuri karafuu kavu gunia 518
sawa na tani 23.3 kwa TZS milioni 326.4 zilipatikana bila ya athari yoyote.
Afisa Mdhamini huyo
aliongeza kuwa magunia 9 ya karafuu kavu yenye uzito wa kilo 405 sawa na TZS
milioni 5.6 zimeathirika na kueleza kuwa
ujenzi waa eneo hilo liloloharibika kutokana na maji mengi yaliotokea
barabarani na kusababisha maporomoko na dongo na kusabiisha kugoka kwa mti
mkubwa ulioelemea ukuta wa ghala na kuuangusha na maji na matope pamoja na kti
kuingia ghalani humo.
Dk. Shein alipongeza
juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kurejesha hali yake ghala hilo pamoja
na juhudi za ziada zilizofanywa katika kuziokoa karafuu zilizokuwemo ghalani
humo.
Katika maelezo yake, Dk.
Shein huko Makombeni, aliwapa pole wananchi wa eneo hilo kutokana na athari za
nyumba zao zilizoathirika katika Wilaya hiyo zipatazo 540, ambapo Shehia 30
kati ya 34 zimeathirika na mvua hizo na kuwaeleza kuwa Serikali iko pamoja na
wao katika tukio hilo na kuwapongeza kwa uvumilivu na umoja wao waliouonesha
wakati wa maafa hayo.
Nao uongozi wa Wizara ya
Ujenzi pamoja na wataalamu wake walimueleza Dk. Shein hatua zilizochukuliwa
katika kuhakikisha barabara zote kisiwani Pemba zinapitika kama ilivyo hivi
sasa kwa hatua za awali huku juhudi zaidi zikiendelea kuchukuliwa.
Nao wananchi wa maeneo
mbali mbali ambayo Dk. Shein alipita kwa kuwapa pole na kuwafariji sambamba na
kuwapongeza kwa umoja na mshikamano wao waliouonesha wakati wa maafa hayo,
walimpongeza kwa kwenda kuwaona.
Wananchi hao
walimpongeza Dk. Shein kwa kufanya ziara yake hiyo kwa makusudi kwenda kuwaona
na kueleza jinsi walivyofurahi na kufarajika kwa kuona kumbe Rais wao yupo
pamoja na wananchi wake kwa wakati wote.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment