Habari za Punde

Rais Magufuli azindua kituo kikuu cha Taifa cha kuhifadhi Mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia ya elektronik

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Dar-es-Salaam                                                       1.06.2017
---
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amekizindua kituo kikuu cha Taifa cha kuhifadhi Mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia ya elektroniki na kuzitaka taasisi mbali mbali zikiwemo za Serikali, Kampuni na Benki kujisajili katika kituo hicho ili kuweza kukusanya kodi kwa ufanisi zaidi.

Hayo aliyasema hay oleo huko Kijitonyama jijini Dar es Salaam, wakati akizindua  Kituo hicho, kilichoandaliwa kwa mashirikiano ya pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), ili kusaidia kuondosha miaya ya uvujaji wa mapato ya serikali zote mbili.
Sherehe za Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, Mawaziri wa Fedha wa Serikali zote mbili na viongozi mbali mbali wa serikali,dini na  watendaji, wakuu wa Makampuni.

Aliyaomba makampuni ya simu na makampuni mbali mbali wajisajili katika kituo hicho ikiwemo Vodacom, Airtel, Tigo, Zanteli na zote zilizokuwa bado wafanye hivyo kwa hiari, ili kusudi wasiwaone na wao wasionewe katika kuweka usawa pande zote hizo na kuwasisitiza wanaogopa kitu gani kama wanalipa kodi kupelekwa katika hiyo mashine hizo.

Alisema kituo chicho kilianza kazi tokea mwezi Oktoba mwaka jana, lakini hadi sasa muitikio wa taasisi za Serikali na makampuni binafsi kujiunga sio mkubwa na  mpaka sasa ni makampuni matatu ndio yaliyojiunga, ikiwemo TTCL,  Halotel na Smart,  hivyo ametoa wito kwa taasisi zote kujiunga.

Rais Magufuli alisema kuwa kwa kutumia kituo hicho makusanyo ya kodi yatayotolewa hayatokuwa na ulalamishi, kwa sababu hapo awali walikuwa wakikusanya mapato kwa kutumia njia ya mtu na mtu, kulipa kodi, ambapo yule mtu anategemea na uaminifu wake, kwa vile wapo wengine wamekuwa sio waaminifu.

Alifafanua kuwa fedha za Serikali zinatakiwa zikusanywe na sio kubaki katika mikononi kwani wenye utendaji mzuri katika masuala ya ukusanyaji wa mapato sio wote, jambo ambalo husababisha malalamiko katika pande zote mbili, hivyo ili kuondoa kasoro hizo za wale wanabambikiziwa kodi na wale waliokuwa hawataki kulipa kodi, muarubaini ni kituo hicho.

Aliongeza kuwa kituo hicho ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya nchi, kama inavyofahamika Serikali iliamua kujenga kituo kwa makusudi makubwa mawili ikiwemo kuhakikisha kunalindwa usalama wa taifa na taasisi za serikali na makampuni binafsi yanayoendesha shughuli zake nchini.

Alisema kuwa, Taasisi za Serikali na Makampuni binafsi yatakayotunza taarifa zao katika kituo hicho yatakuwa na uhakika wa usalama wa taarifa zao.

Alieleza sababu ya pili kujengwa kituo hicho ni  dhamira ya serikali ya kuimarisha na kukuza sekta ya teknolojia ya habari na Mawasiliano, ambayo inakuwa kwa kasi na ndio kichocheo kikubwa katika maendeleo ya kiuchumi duniani kote, ambapo nchi zote zilizopiga hatua katika sekta hiyo zilijenga vituo vya kutunza taarifa (data centre).

Katika hotuba yake, Rais Magufuli ameiangiza Mamlaka ya Mawasilino Tanzania (TCRA) kuchukua hatua zaidi kwa makampuni ya simu badala ya kuzitoza faini.

Alisema hakuna mtu duniani anayependa kulipa kodi hivyo, wakusanyaji kodi wa TRA na ZRB wasitegemee kama watakuwa na mapenzi makubwa katika jamii hata siku moja ila kinachohitajika  kwa upande wao ni kukusanya mapato ya serikali tu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein nae kwa upande wake alieleza kuwa historia inaeleza kuwa hata zile dola zilizovuma na kutawala katika enzi za zamani ni zile zilizokuwa na mifumo imara na yenye nguvu katika ukusanyaji wa mapato.

Dk. Shein alieleza kuwa kuzinduliwa kwa Mfumo huo kumeonesha wazi kuwa Serikali itaondokana na Mfumo wa kukusanya mapato bila ya kufuata utaratibu na badala yake alitumia msemo wa wahenga kuwa ‘Mali bila ya daftari hupotea bila ya habari”,hivyo kwa maelezo yake hayo leo daftari jipya limezinduliwa ambalo hapo nyuma halikuwepo nalo ni kituo hicho cha Taifa cha kuhifadhi Mifumo ya ukusanyaji kodi kwa njia ya kielektroniki.

Katika maelezo yake Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kuwa tokea alipoingia madarakani Novemba 3 mwaka 2015 amekuwa akisimamia vyema ukusanyaji wa mapato hatua ambayo imepelekea kuimarika kwa uchumi ili kusaidia maendeleo ya wananchi

Alitoa pongezi kwa Wizara zote za Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapidunzi ya Zanzibar pamoja na Mawaziri wake kwa hatua hiyo ya kuanzisha kwa Mfumo wa Serikali wa ukusanyaji Kodi kwa njia ya kielektroniki.

Aidha, alizipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) huku akisisitiza kuwa katika ulipaji wa kodi suala la umakini lina umuhimu mkubwa na ndio maana tokea kuingia madarani katika uongozi wake mapato ya Zanzibar yameongezeka mara nne na kueleza kuwa taasisi hizo zimeweza kushirikiana kwa mambo ya Muungano na yasio ya Muungano.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango alisema kuzinduliwa kwa mfumo huo utasaidia kupunguza upotevu wa mapato ya serikali na kuondosha usumbufu kwa wadau mbali mbali.

Alieleza nchi imeweka kipaumbele katika kuhakikisha inakusanya mapato kwa usahihi ili iweze kujenga uchumi wake na kuondokana na kuomba omba, na kueleza imani yake kwa Taasisi za TRA na ZRB baada ya kuanza kwa Mfumo huo.

Mapema Rais Magufuli na viongozi wengine walitembelea katika kituo hicho cha Taifa cha Ukusanyaji wa Mapato kwa njia ya kielektroniki.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar


Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.