Habari za Punde

PACSO wapata viongozi wapya


HABIBA ZARALI, PEMBA

Umoja wa Jumuiya zisizo za kiserikali Pemba (PACSO), umepata viongozi wapya, kufuatia Mkutano mkuu wa Jumuiya hiyo, uliofanyika katika skuli ya Maandalizi Madungu mjini Chakechake kwa kuwachagua viongozi wapata watakaoiongoza Jumuia hiyo kwa miaka mitano.

Waliochaguliwa ni pamoja na Omar Ali Omar kuwa Mwenyekiti, Mohamed Ali Khamis kuwa Makamo Mwenyekiti, Sifuni Ali Haji amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu huku Mshika Fedha akichaguliwa Is-haka Asaa Hamad.

Kwa upande wa wajumbe wa kamati tendaji, waliochaguliwa ni Juma Ali Mati Mkoani, Ali Shomari Chake Chake, Ali Kombo Mali, Asha Pandu, Othman Hamad  na Fadhila Khamis wa Micheweni.

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kuchaguliwa Katibu mkuu mpya Sifuni Ali Haji, alisema ushirikiano mazuri kati ya taasisi nyengine na PACSO, ndio njia ya msingi ya kiziwezesha asasi za kiraia, kuwapeleka mbele na kuwaletea maendeleo.

Alisema wakati umefika kwa asasi za kiraia kuwa bega kwa bega na jumuiya ya ‘PACSO’ ili kuweza kufanya mambo yanayoweza kuwasogeza mbele katika harakati za kazi zao.

Aliitaja mikakati aliyonayo wakati wa uongozi wake, alisema ni kuzishirikisha asasi za kiraia kwa kudumisha umoja na kuleta maslahi katika asasi hizo na kuandaa kamati za taaluma  na ufuatiliaji kama ulivyopangwa.

“Ntahakikisha natatekeleza mazuri na kudumisha umoja na mshikamano katika taasisi zote, ili umoja huu uzidi kusonga mbele na kuweza kuleta faida kwa yale yaliokusudiwa”,alisema.

Katibu Mkuu huyo aliziomba taasisi mbalimbali kuachana na dhana potofu ya kuwa ‘PACSO’ haina faida na kuwataka kujiunga na uwanachama, ili kuweza kuzidisha nguvu na kujiletea maendeleo katika taasisi zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Omar Ali Omar, alisema  ni vyema kwa asasi hizo zikawa na upendo utakaowaonesha njia sahihi katika kujitafutia fursa mbalimbali za kimaendeleo.

Alisema wakati umefika wa kuondowa tabia ya kulaumiana na kulalamikia jambo lisilo na msingi ndani ya asassi zao badala yake wachukuwe juhudi  binafsi za kurekebisha panapohitajika.

“Pale ambapo asasi moja itaona kwamba kuna fursa  mahali fulani basi iweze kuitaarifu  na asasi nyengine ili kwa umoja huu uweze kutekeleza majukumu na malengo yaliowekwa”,alisema.

Mapema akielezea miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika jumuiya hiyo, Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake Mohamed Najim Omar, alisema ni pamoja na jumuiya kuongeza idadi ya wanachama kutoka 77 hadi kufikia 84, kupata bodi ya wadhamini.

Alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo ni pamoja na ulipaji mdogo wa ada kwa wanachama kwenye mtandao, ukosefu wa mfanyakazi wa kudumu  anaeweza kushughulikia harakati za kila siku  za ofisi, ili aweze kuwapatia taarifa wanaohusika na kutokuwa na ofisi ya kudumu.


Mtandao wa asasi za kiraia kisiwani Pemba una mashirikiano na wadau mbalimbali, ikiwemo watu binafsi ,sekta za umma na asasi mbalimbali katika wilaya zote za Pemba, kwa lengo la kuleta umoja na maendeleo ya wananchi kwa kuzididisha nguvu za pamoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.