Habari za Punde

Wizara ya Habari yatekeleza ahadi kwa wanamichezo 43 Kisiwani Pemba



Afisa Mdhamini Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo Mh. Khatibu Juma Mjaja  akimkabidhi zawadi Abdalla Kombo Hamad ambae alishiriki mashindano ya baiskeli hatua ya fainali katika tamasha la Pemba Weekend Bonanza lililofanyika tarehe 28-30 Julai 2017

Baadhi ya washiriki wa mashindano ya ngalawa na resi za baiskeli ambao walihudhuria katika ukumbi wa uwanja wa michezo wa Gombani chake chake Pemba kupokea zawadi zao kama walivyoahidiwa na Waziri wa Habari Utalii Utamaduni na Michezo Mh. Rashid Ali Juma katika kilele cha Tamasha la Pemba Weekend Bonanza Vumawimbi 


Na Ali Othman Ali, Pemba

Afisa Mdhamini Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo Mh. Khatibu Juma Mjaja  amekabidhi zawadi kwa wanamichezo mbalimbali walioshiriki tamasha la kimichezo la Pemba Weekend Bonanza lililoandaliwa na taasisi ya Rafiki Nework Kisiwani Pemba mnamo tarehe 28-30 Julai mwaka huu.

Makabidhiano hayo ambayo yamefanyika katika ukumbi wa Uwanja wa michezo wa Gombani Chake Chake Pemba yalijumuisha wanamichezo 43 ambapo 27 kati yao ni washiriki wa mchezo resi za za baiskeli na 16 ni manahodha wa ngalawa walioshiriki katika pambano la resi za ngalawa.

Akizungumza na wanamichezo hao kabla ya kuwakabidhi zawadi ikiwa ambazo zilitokana na utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Mh. Waziri wa Habari Utalii Utamaduni na Michezo Mh. Rashid Ali Juma, Mh. Mjaja amewataka vijana kuthamini vipaji vyao kwa kufanya bidii katika mazoezi ili kujiweka sawa kwa mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Aidha Mh. Mjaja amepongeza juhudi za Taasisi ya Rafiki Network kwa kuandaa na kusimamia kwa umahiri Tamasha kubwa lakimichezo ambalo lilijumuisha michezo mbali mbali kama vile Mchezo wa Ng’ombe, resi za baiskeli, mashindano ya kuogelea na resi za ngalawa.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Rafiki Network kwa kuandaa tamasha ambalo lilifungua milango na hisia za kutaka kuanzishwa matamasha zaidi kwa nia ya kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi yetu”

“Katika maisha yangu sijawahi kushuhudia tamasha kubwa  kusimamiwa na taasisi binafsi kufanyika kisiwani Pemba, Tamasha la Pemba weekend Bonanza lililoandaliwa na Taasisi ya Rafiki Network ni la kwanza na la aina yake”

Awali Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa Taasisi ya Rafiki Network Ndugu Ali Othman Ali ameipongeza Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo kwa kuthamini juhudi za Taasisi ya Rafiki Network za Kuhakikisha kwamba hali za watu zinaboreka katika Nyanja mbali mbali kama vile kiuchumi na kijamii.


Aidha Mkurugenzi huyo wa Habari na Mahusiano wa Taasisi hiyo, amewahakikishia wanamichezo hao kwamba wataendelea kufaidi matunda ya vipaji vyao baada ya kumalizika kwa tamasha la Pemba weekend bonanza kwa kupatiwa fursa mbali mbali kila zinapotokea. 

Akitoa mfano wa fursa hizo Nd. Ali amesema Taasisi ya Rafiki Network imetoa fursa kwa washindi watatu kuhudhuria na kushiriki katika pambano la resi za baiskeli kisiwani Unguja ambapo mchezo huo nimiongoni mwa michezo itakayofanyika katika tamasha la Zanzibar New Year Bonanza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.