NA HAJI NASSOR, PEMBA
MASHEIKH, wanaharakati wa mambo ya kiislamu, waalimu wa
madrassa na waislamu wilaya ya Wete kisiwani Pemba, wamependekeza kuwe lazima sheria
mpya ijayo ya Mufti, impe hadhi ya kipekee, ili aweze kufanya shughuli zake kwa
ufanisi.
Walisema
kama zilivyo sheria nyengine zilivyowapa hadhi baadhi ya viongozi, hivyo ni
vyema ndani ya sheria hiyo, kiwemo kifungu kinachoonyesha Mufti wa Zanzibar
anakuwa na hadhi, kama wanavyoshuhudia wa nchi nyengine.
Wakitoa
maoni yao juu ya mswada wa sheria ya Mufti mjini Wete mbele ya wajumbe wa Tume
ya Kurekebisha waliofika wilayani humo, kukusanya maoni, walisema wakati
umefika kwa Mufti nae kuwa na hadhi ya kipekee.
Sheikh
Khamis Rashid Suwedi, Imamu wa msikiti wa Ijumaa wa Hanafi, alisema hadhi
ambayo wanaitaka kwa Mufti iwe zaidi ya waziri, katibu mkuu au wakurugenzi.
“Kuanzisha
sheria kwa ajili Mufti na ofisi yake, ni jambo jema, maana kwa sasa anaonekana
kama mtu wa kawaida anapokuwa kwenye misafara yake, jambo ambalo sio sahihi”,alisema.
Nae
mwalimu Abeid Seif, alisema baada ya kuwepo kwa kifungu hicho ndani ya sheria
hiyo ijayo, lazima kuwe na utekelezaji wake, maana zipo sheria kadhaa nzuri
lakini ubora wake hauonekani.
Nae
Naibu Katibu wa Jumuia ya Maimu wilaya ya Wete Rashid Khamis Hamad, alisema
wasimamizi wa sheria hiyo baada ya kupita, lazima waache ubabaishaji katika
kuitekeleza kwake, maana ni tafsiri ya Kur-an na hadithi.
“Kwa
Mufti ni kiongozi wa dini ya kiislamu hivyo, hata mambo atakayoyaongoza ni yale
ya kiislamu, na hata sheria yake inatokana na kitabu kitakatifu, hivyo lazima
kusiwe na ubabaishaji katika hili”,alieleza.
Wakichangia
mswada wa sheria ya ndoa na talaka, viongozi hao wa dini walisema, kama ikipita
inawez kuondoa mkanganyiko wa tafsiri wa mambo mbali mbali kama mfano wa talaka
zilizotokewa tatu kwa wakati mmoja.
Mjumbe
kutoka Jumuia ya Maendeleo ya Kiislamu, sheikh Haji Mkubwa Ahmed , alisema wapo
masheikh na makadhi wamekuwa na uamuzi unaotofautiana juu ya tamko la talaka
zilizotolewa zaidi ya tatu.
“Naamini
ujio wa sheria hii, sasa waislamu wanaolalamikiana juu ya matamko ya maandishi
ya talaka zilizotolewa 10, sita au tatu na hata mbili kwa wakati mmoja, sasa
sheria itaoongoza”,alisema.
Mapema
mwanasheria kutoka Tume hiyo Mohamed Ahmed, alisema sheria inayokuja ya ndoa na
talaka, itakuwa ya kipee kwa nchi za Afrika Mashariki.
Alisema
nchi zote hizo hadi sasa, hazina sheria ya aina hiyo, hivyo anaamini
itakapomalizika wanaweza kufika Zanzibar kuiga mfano kwa ajili ya nchi zao.
Tume
ya Kurekebisha Sheria Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mshibe Ali Bakari
na Katibu wake Asma Jidawi, imeshakamilisha ziara yake ya siku nne kisiwanin
Pemba, ambapo ilikusanya maoni, juu ya miswada mitatu ya sheria za Mufti, ndoa
na talaka na kuifanyia mapitio sheria ya asasi za kiraia no 6 mwkaa 1995.
No comments:
Post a Comment