Habari za Punde

ZANCHIK yanunua tani nne za samaki kutoka wavuvi wa Kichina

NA ABDI SHAMNAH

JUMLA ya tani nane za samaki wa aina mbali mbali zimeshushwa kutoka katika meli za Uvuvi za kampuni ya Yu Shian Shandoay kutoka China, na kuuzwa kwa kampuni ya ZANCHIK, kwa lengo la kuwafikia walaji wa kawaida waliopo katika maeneo mali mbali ya Zanzibar.
Mwishoni mwa wiki iliopita meli tatu za kampuni ya Yu Shian Shandoay, zikiwa na kiwango kikubwa cha samaki ziliwasili Zanzibar kwa lengo la kufanyiwa ukaguzi, ikiwa ni taratibu katika upatikanaji wa leseni ya uvuvi wa bahari kuu.
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti katika Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, Christian Alphonce Zowa, alisema kuwa samaki hao ni miongoni mwa kiwango kikubwa cha samaki wanaolengwa kushushwa na kuuzwa kwa wananchi wa Zanzibar, kupitia kampuni mbali mbali zilizotuma maombi.
Alisema kuuzwa kwa samaki hao, kunalenga kukabiliana na mahitaji makubwa ya kitoweo yanaoyawakabili wananchi wa Zanzibar.
“Kuanza kuuzwa kwa samaki hawa, na wengine watakaouzwa hapo baadae kutasaidia sana kupunguza kasi ya mahitaji ya kitoweo kwa wananchi”, alisema.
Nae, Ofisa leseni wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Daniel Pius Kawiche, alisema katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo wimbi la maombi ya kampuni za meli zinazohitaji kupatiwa leseni ya uvuvi katika eneo la Bahari Kuu ya Tanzania.
Alisema katika kipindi cha wiki moja iliyopita,  jumla ya maombi 24 yalipokelewa kwa mahitaji hayo, na kubainisha kuwa katika meli 13 zilizowasili, tayari meli nane zimeshakaguliwa, zikiwemo tatu kutoka Kampuni ya Yu Shian Shandoay ya nchini China.

Alisema ukaguzi wa meli hizo umefanyika kwa weledi na umakini na mkubwa, na kubainisha kuwa zote zimekidhi viwango vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria na kanuni za mwaka 2009, ambayo  ilifanyiwa marekebisho 2016.
“Meli hizo zimekaguliwa na kuthibitika zinakidhi viwango kwa mujibu wa sheria zetu, hivi sasa zinaendelea na taratibu zilizobaki, ikiwemo kulipia ada kwa ajili ya kupatiwa leseni”, alisema.
Katika hatua nyengine, Mkurugenzi wa  Kampuni ya ZANCHIK, ambayo ni maarufu kwa uingizaji wa kuku ‘Perdue’, Issa Kassim Issa, alisema kwa kuanzia Kampuni hiyo imenunua samaki tani sita, ambao wataingizwa katika kiwanda cha Kampuni hiyo kiliopo Maruhubi na kusarifiwa vizuri na hatimae kuweka (packing) katika vifaa maalum, kabla ya kufikishwa katika masoko mbali mbali na kuwafikia walaji.
Alisema kampuni hiyo baada ya kujikita katika uingizaji  wa kuku aina ya Perdue, hivi sasa inalenga kununua samaki kutoka katika Meli mbali mbali zitakazoendesha uvuvi katika Bahari Kuu ya Tanzania.
Alisema hatua ya Serikali kufungua milango ya uwekezaji katika sekta ya Uvuvi, italeta faraja kubwa kwa wananchi wa Zanzibar, kuimarisha uchumi pamoja na kupanua soko la ajira, hususan kwa vijana.
Aidha alisema samaki wote watakaonunuliwa na Kampuni hiyi kutok meli za Uvuvi, watauzwa katika soko la ndani, na kubainisha kuwa Kampuni hiyo haina mpango wa kusafirisha samaki hao nje ya nchi.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo hakuwa tayari kueleza bei halisi ya ununuzi wa samaki hao, sambamba na bei itakayotumika kuwauzia wananchi.
“Bei itakuwa nafuu  tu kwa wananchi, kaam ilivyo kwa perdue, si unaona, kila mtu anamudu kununua, basi na samaki nao watakuwa hivyo hivyo,” alisema.
Aidha juhudi za gazeti hili kumpata Mkurugenzi wa Kampuni inayomiliki meli hizo, Simon Chen, kuelezea kiwango cha bei ya samaki hao kwa kipimo cha tani,hazikuweza kuzaa matunda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.