Habari za Punde

UVCCM YAPIGA MSASA VIJANA WAKE, YAHOJI UTEKELEZAJI WA ILANI.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mjini, Bi.Hudhaima Mbarouk Tahiri akizungumza katika ziara ya Wilaya hiyo iliyofanyika katika Ofisi ya Jimbo la Kikwajuni Zanzibar (Picha na Afisi Kuu 

Na Is-haka Omar, Zanzibar.
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) Wilaya ya Mjini, Hudhaima Mbarouk Tahiri amewasihi vijana walioshindwa kuendelea na elimu ya juu kutokata tamaa badala yake watumie fursa ya sekta ya ujasiriamali kujiajiri wenyewe.

Wito huo ameutoa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka miwili ndani ya Jimbo la Kikwajuni Unguja.

 Amesema vijana wanatakiwa kuwa wabunifu katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa kujiunga na vikundi mbali mbali vinavyoanzishwa katika jimbo hilo ili kujikwamua kimaisha.

Amesisitiza umuhimu wa vijana wa UVCCM kujiendeleza kielimu katika fani mbali mbali kwani kufanya hivyo kutasaidia jumuiya kuwa na vijana imara wenye ujuzi utakaosaidia kuharakisha maendeleo ya umoja huo kwa haraka.

Pia amewashauri vijana hao kuwa kuwa wamoja na wenye msimamo usioyumba katika kupigania maslahi ya CCM ili iweze kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao.

“CCM ndio chama pekee kinachojali na kuwalea vijana katika misingi imara ya kuwajenga kifikra, kiitikadi na kimaadili  ili waweze kuwa viongozi bora wa baadae watakaoendeleza urithi wa Wanamapinduzi ya Mwaka 1964 kwa vitendo.”, alisema Mwenyekiti huo.

Akizungumzia tatizo la matumizi ya Dawa za kulevya, Mwenyekiti huyo wa UVCCM  alisema Wilaya ya Mjini imekuwa ni miongoni mwa sehemu zilizoathirika na janga hilo hivyo vijana wanatakiwa kujiepusha na matumizi ya dawa hizo kwani zinaangamiza nguvu kazi ya taifa.

Naye Katibu wa Wilaya hiyo Aboud Said Mpate , alisema lengo la ziara hiyo ni uongozi huo kutoa shukrani kwa wanachama waliowachagua viongozi hao pamoja na kupokea taarifa za utekelezaji wa Ilani kutoka kwa Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa Wilaya ya mjini ili wananchi waliowachagua waweze kujua mambo yaliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili.

Aboud amewataka vijana hao kuwa makini kwa kuepuka kutumiwa katika kutengeneza makundi ya kulinda maslahi ya baadhi ya viongozi hasa wakati huu wa uchaguzi unaoendelea ndani ya Chama na Jumuiya zake.

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani, Mwakilishi wa Jimbo hilo, Nassor Salim Jazeera amesema viongozi wa jimbo hilo kwa kushirikiana wameanzisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo kuendeleza mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya milioni 300, kuanzisha vikundi vya usafi ili vijana wasiokuwa na ajira wajiajiri wenyewe.

Mh. Jazeera alisema miradi mingine wameshauri na kushirikiana na   serikali kujenga barabara za lami mbili, ujenzi wa uwanja wa michezo wa Mao Tse Tung, Ujenzi wa Shule ya kisasa ya Ghorofa katika Mtaa wa Mwembe shauri pamoja na kuwasaidia akina Mama mitaji ya kuanzisha vikundi vya ujasiriamali.
Alifafanua kuwa lengo la viongozi hao ni kuhakikisha wanamaliza kero na changamoto zote zinazowakabili wananchi katika jimbo hilo kabla ya mwaka 2020.

Sambamba na hayo alisifu kasi ya kiutendaji ya UVCCM katika Wilaya hiyo na kuwasihi waendelee kushirikiana na viongozi hao bega kwa bega ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Ziara hiyo ya siku nne  itaendelea kufanyika katika Majimbo yote ya UVCCM Wilaya ya Mjini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.