Habari za Punde

Kituo cha Mkono kwa Mkono Kivunge Chapokea Kesi 23 za Udhalilishaji Kwa Mwezi wa Agusti hadi Oktoba 2017.

Na Maryam Kidiko - Maelezo Zanzibar.                   03/12/2017.
JUMLA ya Vijana 23 wameripotiwa kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika kituo cha mkono kwa mkono cha Kivunge, Mkoa Kaskazini Unguja wakiwemo watoto wa kiume kwa mwezi Ogasti, Septemba na Oktoba Mwaka huu.
Takwimu hiyo  ilitolewa na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa Kaskazini Unguja Nd. Mussa Haji Kessi katika Skuli ya Elimu Mbadala Rahaleo wakati wa kongamano lililozungumzia vitendo vya udhalilishaji lililoandaliwa na Jumuiya ya wanafunzi waliosoma Marekani kupitia mradi wa YESS (Zanzibar Yess Allumni Association).

Alisema takwimu hiyo inawahusu vijana aliofanyiwa vitendo hiv yon a kutoa taarifa lakini wapo wengine wengi wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya udhalilishaji bila ya kutoa taarifa katika kituo hicho.

Aidha alisema tatizo la udhalilishaji hivi sasa limekuwa kubwa na jamii  inapaswa kushirikiana katika kulipiga vita kwani itapelekea Vijana kuathirika kiakili na kuharibu muelekeo mzima wa maisha yao ya baadae.

Hata hivyo alisema Wizara Kazi, Uwezeshaji, Wazee Vijana, Wanawake na Watoto  kwa kushirikiana na taasisi nyengine  zinaendelea na juhudi za kupunguza vitendo hivyo, na kuviomba vyombo vya sheria kuwa tayari kutoa ushirikiano.

“Kwa upande wetu sisi tunafanya kazi kama inavotakiwa na kupeleka ushahidi sehemu husika ili kuendelea na uchunguzi lakini hatma ya kesi hizo inakuwa mtihani, ”alisema Afisa huyo.

Ndugu Mussa alisema Wizara inakerwa sana na vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa watoto wa kike na kiume ambavyo ni kinyume na maadili na mafundisho ya dini zote vinahatarisha ustawi wa vijana hao.

Raisi wa Jumuiya ya wanafunzi hao Nd. Saidi Ali alieleza kuwa lengo la kuanzishwa Jumuiya hiyo ni kuihamasisha Jamii kuwa na moyo wa kujitolea na kuelewa umuhimu wake katika maendeleo ya nchi.

Alisema tokea kuanzishwa Jumuiya hiyo wamekuwa wakijitolea katika kutoa elimu sehemu mbali mbali na kusaidia katika shughuli  za kutunza mazingira.

Pea alisema wameweza kupata nafasi kwa Wanafunzi kwenda Marekani kwa mwaka mmoja  na  kuweza kusaminiwa vipaji walivyokuwa navyo kitu kinachofanya wawe na hamu ya kutimiza walichoendea.

Katibu Mkuu wa Mradi wa YESS Nd. Msimu Ali aliwashukuru wenyeji wao wanapokuwa Marekani kwa mashirikiano mazuri wanayoyapata jambo ambalo linawapa wepesi wa kutekeleza majukumu yao ya kusoma.

Aliwaomba Wazazi kuondowa wasi wasi kwa Watoto wao wanaopata nafasi ya kwenda Marekani kusoma na kuwaomba kuwapa mashirikiano ili kutimiza malengo yao.

Jumuiya ya Zanzibar Yess Allumni imeanzishwa mwaka 2007 na vijana wa Skuli za Sekondari Zanzibar waliopata nafasi ya kusoma nchini Marekani kwa kipindi cha mwaka mmoja na malengo yake ni kusaidia jamii ya Zanzibar.
                                                         MWISHO.
           IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.