MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekitiwa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kwamba CCM ina
uzoefu mkubwa wa kufanya mageuzi ya kifikra, itikadi, Sera na mabadiliko
mengine ya kimaendeleo kwa kufuata matakwa ya wananchi bila ya kuathiri misingi
imara iliyowachwa na waasisi wa Taifa hili.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika Mkutano Mkuu wa CCM wa Mkoa wa Kusini Unguja ulioenda sambamba
na uchaguzi wa viongozi wa Mkoa huo Kichama, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa
Hoteli ya Coconut, Marumbi, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ambapo Makamo
wa Rais wa Jamhuri ya Muunago wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan alihudhuria.
Katika maelezo yake
Dk. Shein alisema kuwa CCM si chama cha mtu mmoja kama ilivyo vyama vyengine
vya siasa vinavyoendelea kupoteza muelekeo na kusambaratika hivi sasa kwa
kukosa uzoefu wa historia kama ilivyo kwa CCM.
Dk. Shein ambaye Mkoa
huo ndio Mkoa wake Kichama aliongeza kuwa ni vyema kwa wajumbe wa mkutano huo
wakatambua hivyo na wakahakikisha kwamba viongozi watakaowachagua wanaielewa
itikadi ya chama hicho na sera zake na wapo tayari kuzilinda, kuzisimamia na
kuzitekeleza kwa vitendo.
Alisisitiza kuwa
viongozi watakaochaguliwa katika mkutano huo ambao wamepelekwa na CCM
watalazimika kuwa tayari kuwakemea na kupambana na wazembe, wababaishaji,
wabinafsi na wale wote wenye tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
Makamo Mwenyekiti huyo
wa CCM Zanzibar aliwataka viongozi watakaochaguliwa hawanabudi wawe makini,
kama ilivyokawaidida kwa viongozi wa CCM ambapo umakini wao katika uchaguzi wa
viongozi pamoja na kukemea maovu ndio unaokipa chama hicho nguvu zaidi za
kukubalika, kuchaguka na kupendwa na wananchi wote wanaopenda amani na
maendeleo nchini.
“Chama chetu
kinapendwa kina wavutia wananchi na kina uwezo mkubwa na wa peke yake wa
kurejesha na kujenga matumaini mapya kwa wananchama wake na wananchi wete
hivyo, hapana shaka tuna nafasi nzuri ya kuendelea kushika dola kwa pande zote
mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dahari na zama nyingi zijazo”,alisisitiza
Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa ushindi wa kishindo ambao CCM umeipata katika uchaguzi Mdogo wa
Madiwani uliofanyika wiki iliyopita tarehe 26 Novemba, 2017 katika Kata 43
zilizoko katika Mikoa 19 ya Tanzania Bara ni ithibati ya kwamba CCM ilipitisha
viongozi wenye sifa, uwezo, nia njema na waliokubalika kwa wananchi katika
kugombea nafasi hizo.
Alisema kuwa ushindi
mkubwa uliopatikana hata katika maeneo ambayo wapinzani walidhani kwamba ni
ngome zao ni uthibitisho wa kuwa wananchi wanaendelea kukiamini na kukipenda
chama hicho na kwamba maendeleo ya dhati ya nchi yamo ndani ya CCM.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliupongeza Mkoa huo kwa kuendelea kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi
Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambapo tayari wameaza kutekeleza vyema kwa
kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari hadi Disemba 2016 kwa kushirkiana na
Serikali ambapo mafanikio yamepatikana katika sekta za kiuchumi na kijamii.
Aliwahakikishia
wananchi wa Mkoa huo kuwa Serikali anayoiongoza itafuata maelekezo ya Ilani
hiyo ya CCM katika kuwafikishia huduma bora za jamii huku akitumia fursa hiyo
kuipongeza Wizara ya Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira pamoja na taasisi zake za ZECO na ZAWA kwa kutekeleza
agizo lake alilolitoa katika ziara yake la kuhakikisha wananachi wa Makunduchi
na Kibuteni wanapata maji kutoka katika kisima cha Mwambiji.
Aliongeza kuwa hivi
leo tayari maeneo ya Kibuteni na Makunduchi yameshapata huduma za maji
zinazotokana na kisima cha Mwambiji ambapo tangi lenye uwezo wa lita laki tatu
limeleta ufanisi kwa wananchi kupata maji kwa kutwa nzima bila ya usumbufu
badala ya saa sita tu kama ilivyokuwa hapo mwanzo na kueleza kuwa mapema mwezi
ujao maji yatapatikana kwa uhakika zaidi katika maeneo hayo.
Pia, Dk. Shein
alieleza kuwa katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la upatikanaji wa maji
safi na salama kwa upande wa Michamvi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana
na Serikali ya Ras al Khaiman imechima kisima maalum katika eneo la Ghana,
Bwejuu kwa ajili ya kupeleka maji safi na salama katika kijiji hicho.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwasihi viongozi wote ambao kura zao hazitotosha, wasivinjike moyo na
watambue kuwa mwisho wa uchaguzi mshindi mkubwa ni CCM huku akiwanasihi
viongozi watakaochaguliwa kusimamia nyadhifa na majukumu watakayokabidhiwa
vizuri, ili Mkoa huo uendeleze historia yake ya kuwa ni tishio kwa wapinzani.
Nae Makamo wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ambaye pia, ni Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM, alitoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania
na Mwenyekiti wa Chama hicho Dk. Johm Pombe Magufuli na kusisitiza haja kwa wajumbe
wa Mkutano huo kuwachagua viongozi watakaokiimarisha zaidi chama hicho ili
kiendelee kupata ushindi katika chaguzi zake zote zijazo.
Mapema Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Juma Abdalla Mabodi alitoa salamu za chama na kueleza
mchakato wa uchaguzi ulivyooanza tokea Shina na kueleza kuwa chama kimekuwa
imara na viongozi waliochaguliwa na watakaochaguliwa katika Mkutano huo ni
weliedi na watakipeleka chama hicho katika ushindi mkubwa wa uchaguzi wa mwaka 2020 na kusisitiza kuwa
chama hicho hakitokuwa na chuwa huku
akiwapongeza viongozi wa CCM wa Mkoa huo waliopita kwa kukipa ushindi mkubwa
chama hicho katika chaguzi zote zilizopita.
Nao viongozi wa CCM
Mkoa huo wa Kusini walitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake
kuwa aanazozichukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar na kumpa
pongezi maalum kwa kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma sambamba na kuwapa wazee waliofikia umri wa
miaka 70 pencheni jamii ambayo imeipa
sifa kubwa Zanzibar.
Pia, viongozi hao
walimpongeza Dk. Shein kwa juhudi maalum alizozichukua kutokana na agizo lake
alilolitoa katika ziara yake aliyoifanya katika Mkoa wa Kusini mwezi Agosti
mwaka huu la kuitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha ndani ya mwezi
mmoja wananchi wa Mitakawani wanapata kaji safi na salama jambo ambalo
limefanikiwa na wananchi hao wanapata
huduma hiyo.
Wakati huo huo, Dk. Shein pamoja na
Mama Samia Suluhu Hassan ambao wote ni wajumbe wa Mkutano huo, uliosimamiwa na
Professa Makame Mbarawa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitumia
fursa hiyo kuwapigia kura viongozi wa Chama wa Mkoa huo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment