Habari za Punde

SMZ imetekeleza vyema mipango yake ya maendeleo 2015 - 2017

 Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wakiomba kura kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM unaoendelea katika Ukumbi wa Kimataifa wa Jakaya Mrisho Kikwete Mjini Dodoma wachaguliwe kuwa wajumbe wa NEC.
 Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Tisa wa kawaida wa Chama cha Mapinduzi wakipiga kura kuwachagua Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM anayemaliza muda wake Nd. Ussi Yahya Haji akitafakari kumchagua Mjumbe anayestahiki kushika nyadhifa za Ujumbe wa Halamashauri Kuu ya CCM kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Mjini Dodoma.

Picha na – OMPR – ZNZ.


NA Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetekeleza vyema na kwa mafanikio makubwa mipango yake ya Maendeleo katika kipindi cha Miaka Miwili ya 2015 hadi 2017 iliyopelekea kuimarika kwa Uchumi wake.


Alisema pato la Taifa kwa mwaka 2016 limeongezeka na kufikia thamani ya shilingi Bilioni 2,628.4 ikilinganishwa na thamani ya shilingi Bilioni 2,309.5  kwa Mwaka 2015  hali iliyosababisha pato la Mtu binafsi kupanda na kufikia shilingi Milioni 1,806,000/- kutoka shilingi Milioni 1,633,000/-.Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiwasilisha Taariya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 -2020 kwa kipindi cha miaka miwili iliyoanzia Oktoba 2015-Septemba 2027 kwenye Mkutano Maalum wa kawaida wa CCM unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Jakaya Mrisho Kikwete uliopo Mjini Dodoma.Alisema kasi ya mfumko wa bei imefikia wastani wa asilimia 6.7%  kwa mwaka 2016 kutoka asilimia 5.7%  ya mwaka 2015 hali inayoonekana kudhibitiwa katika kiwango cha tarakimu Moja kutokana na mwenendo wa
bei wa bidhaa za vyakula Nchini.Balozi Seif  alieleza kwamba mkazo zaidi utawekwa na Serikali katika kugharamia uendeshaji wake na kutoa huduma bora kwa Wananchi kwa kutumia Rasilmali zilizopo Nchini na kuhakikisha matumizi yote yanayofanywa yanaleta tija kwa Umma.Alisema katika kufikia azma hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaongeza jitihada kubwa katika ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya ndani yaliyochangia uchumi na kufikia makusanyo ya shilingi Bilioni 50 kwa Mwezi kutoka shilingi Bilioni 30 kwa Mwezi katika kipindi cha Mwaka Mmoja  uliopita.Balozi Seif alieleza wazi kwamba mkazo zaidi utawekwa na Serikali Kuu katika kuimarisha wigo wa Mapato ili kuongeza makusanyo sambamba na kudhibiti matumizi kwa ajili ya maendeleo ya Wananchi.Akizungumzia Sekta ya Uvuvi na Ufugaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema jitihada za kuliimarisha eneo hilo zimechukuliwa na Serikali Kuu katika azma ya kunyanyua kipato cha wafugaji na Wavuvi hasa katika utoaji wa ajira endelevu.Alisema Serikali kupitia Taasisi zinazosimamia sekta hizo zimelazimika kuhamasisha Wafanyabiashara  na Taasisi za kiraia kusaidia upatikanaji wa zana za Kisasa zinazotumika katika kuziendeleza Sekta hizo muhimu
Nchini.Balozi Seif     alifahamisha kwamba hivi sasa yapo mazingira mazuri yaliyowekwa ya Uwekezaji katika Sekta za Uvuvi, Kilimo na Ufugaji hali iliyowavutia Wawekezaji wengi wanaojishughulisha na Sekta hizo kujitokeza kwa wingi kutumia fursa zilizopo kwenye eneo hilo na kuamua kuwekeza miradi yao.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa katika kipindi kifupi kijacho yapo matarajio makubwa yatakayojitokeza  katika Sekta hizo jambo ambalo ni chachu katika kuimarisha uchumi kwa jumla.Balozi Seif  ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alifahamisha kwamba kuimarika kwa Demokrasia katika hali ya Amani na Utulivu Nchini ambayo ni Haki ya kila Mwananchi kujivunia
imesaidia kuharakisha maendeleo ya Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa.Akigusia suala la Makaazi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchimi Zanzibar {ZIPA} inaendelea kusimamia Uwekezaji katika Mji Mpya  na wa Kisasa unaojengwa katika Kijiji cha Fumba baada ya kukamilika kwa Mpango Mkuu wa matumizi ya Ardhi.Alisema Miji Mipya ya Makaazi na Kibiashara inaimarishwa  ili kuwa na Makaazi bora pamoja na kupanua wigo wa Biashara katika dhana nzima ya kuitangaza Zanzibar kurejea katika hadhi yake ya kuwa kituo cha Kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.Balozi Seif alieleza hadi kufikia Septemba 2017 ujenzi wa Nyumba za Makaazi 170 zinaendelea kujengwa ambapo nyengine tayari zimeshakuwa katika hatua mbali mbali na nyumba Tano za mfano zimeshakamilika.Alifahamisha kwamba ili kutimiza malengo ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 Serikali imeendeleza Mji Mdogo wa Fumba { Fumba Town Development } mradi unaotekelezwa katika Kijiji cha Nyamazi na Serikali tayari imeshatenga eneo ukubwa la Hekta 63 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.Balozi Seif alisema kwamba dhana ya mradi huo ni kuanzisha Mji Mdogo wa Kisasa wa Nyumba  za gharama nafuu ambapo jumla ya nyumba 1,400 zinatarajiwa kujengwa.Alieleza hadi kufikia Septemba 2017  kwa awamu ya kwanza Nyumba zipatazo 20 zimejengwa na tayari ziko katika hatua ya kukamilika na maandalizi ya ujenzi wa nyumba nyengine 100 zinaendelea.Balozi Seif aliwahakikishia Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwamba katika kupiga hatua kubwa za Maendeleo ya Wananchi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutekeleza maelekezo yaliyomo ndani
ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM hatua kwa hatua.Alisema uandaaji wa Taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi hupitia Wizara, Idara na Taasisi zake kwa mujibu wa Mpango Kazi wa Taasisi hizo unazingatia  maelekezo yaliyomo ndani na Ilani hiyo.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru Wananchi wote Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa ustahamilivu wao na imani yao kubwa  kwa Serikali kwa muda wote wakati Serikali ikiendelea kuyatafutia ufumbuzi
masuala tofauti Nchini. Aliwapongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John  Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kwa juhudi wanazochukuwa za kuliongoza Taifa la
Tanzania katika pande zote mbili za Muungano.Alisema kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Viongozi hao imeanza kuleta matumaini hasa katika kumfanya Kila Mtanzania afaidi matunda ya Taifa lake pamoja na kujenga Nidhamu Serikalini.“ Nafarajika sana kuona Serikali zetu mbili zinazoongozwa na Chama cha Mapinduzi zinaendelea kuyatekeleza malengo  yaliyojipangia na kupata mafanikio makubwa ya Maendeleo ya Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa ”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.Alieleza Viongozi hao Wakuu wamekuwa mstari wa mbele katika kusimamia kupambana dhidi ya adui Rushwa, Ufisadi na wizi wa Rasilmali za Taifa mbapo juhudi hizo zinaonekana  zikichanja mbuga kwa kasi kubwa ya
ajabu inayoishangaza Dunia wakati huu.Akielezea furaha yake isiyo na kifani kutokana na hatua kubwa iliyofikia Timu ya Taifa ya Zanzibar { Zanzibar Heroes } kufikia Fainali ya mashindano ya Kombe la CECAFA Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar pamoja na Wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla  aliwashukuru mashujaa hao.Balozi Seif alisema kitendo cha mashujaa hao cha kupeperusha vyema Bendera ya Zanzibar na Tanzania kimeleta heshima kubwa ndani ya ardhi ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.Alisema Wazanzibari na Watanzania hawana budi kuonyesha furaha, kuwaunga mkono na kuwapongeza Zanzibar Heroes waliopigana kishujaa kama jina lao linavyofahamika na hatimae kuibika na ushindi wa Pili katika mashindano hayo ya Cecafa Challenge Cup.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.