Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Mcha Hassan Mcha amesema Mpango Mkakati wa Saba (CP 7) wa mamlaka hiyo ambao unaendelea kuandaliwa na Menejimenti unarandana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na unalenga kuongeza wigo wa kodi.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao cha siku mbili cha Menejimenti kushiriki uandaaji wa Mpango Mkakati wa Saba wa TRA mkoani Morogoro Februari 02.2026 Naibu Kamishna Mkuu amesema Mpango Mkakati huo wa miaka mitano unakwenda kuchochea ukuaji wa mapato na kurahisisha ulipaji kodi kwa hiari.
Amesema Mpango Mkakati unaoandawa unaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa kutengeneza mkakati unaoiweka TRA mstari wa mbele katika usimamizi wa kodi nchini kwa kutumia ubunifu wa kidijitali, ushirikishwaji wa wadau, na ushirikiano wa kimkakati unaokwenda kuongeza wigo wa kodi.
“Mpango wetu unalenga kuboresha uzoefu wa walipa kodi, kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali, na kujenga utamaduni endelevu wa ulipaji kodi kwa hiari, na kwa msaada wa GIZ, tuna imani kubwa kwamba tutaweza kufanikisha malengo haya na kutoa mchango wa kudumu katika juhudi za Taifa za ukusanyaji wa mapato” amesema Bw. Mcha.
Naibu Kamishna Mkuu amesema mpango huo pia umejikita katika kukuza viwanda, kuunda ajira, na kuongeza ulipaji kodi kwa hiari kupitia maboresho ya huduma za kidijitali na kuimarisha ushirikiano na wadau huku ukilenga zaidi kuleta mageuzi ya kidijitali na matumizi ya mifumo.


0 Comments