Habari za Punde

Wafanyakazi wa Idara ya Habari Maelezo wafanya Usafi

 Wafanyakazi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar wafanya Usafi ndani ya Ofisi yao iliopo Raha leo Mjini Unguja, wakitekeleza agizo lililotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kufanya usafi katika kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 Wafanyakazi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar wakiendelea kufanya usafi wa Mazingira katika maeneo ya Ofisi yao Raha leo Mjini Unguja katika kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mfanyakazi kutoka Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Dude David John akizowa taka baada ya kufanya Usafi katika eneo la Ofisi ya Idara ya Habari Maelezo Zanzibar .
Picha na Maryam Kidiko - Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.

Na Maryam Kidiko / Kijakazi Abdala- Maelezo .     

MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Hassan Vuai Mbarouk amewapongeza Wafanyakazi wa Idara hiyo kwa kujitokeza kwa wingi katika wito wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya kazi zao ili kwenda sambamba na shamra shamra za sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza baada ya kufanya usafi huo Ofisini kwake Raha leo Mjini Unguja alisema katika kuazimisha miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar Serikali imetowa agizo kwa Taasisi zote za Zanzibar kufanya usafi wa mazingira kwa maeneo yote yaliyowazunguuka hivyo hatua iliyooneshwa na wafanyakazi hao inahitaji kupongezwa kwa hali ya juu.

Hata hivyo alisema kuwa pamoja na agizo hilo la Serikali lakini vyema jamii inapaswa kutambua kuwa suala la usafi ni jambo la kawaida kufanya katika mazingira yaliyotuzunguuka  wala halihitaji kusubiri siku za sherehe ndiyo tufanye usafi huo jambo hilo si zuri kwani husababisha maradhi mbali mbali ya miripuko.

“Usafi wa Mazingira ni muhimu katika maisha yetu kwani huepukana na maradhi mbali mbali katika jamii hivyo tuendeleze usafi ili muonekano wa mazingira yetu uwe mzuri.”Alisema Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo alisema kuwa agizo jengine lilotolewa ni pamoja na kupamba mapambo mbali mbali yenye muonekano wa Bendera ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuweza kuleta muonekano mzuri.

Nae Muangalizi wa Ofisi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Arafa Othman Hamad alisema suala la usafi ni suala la watu wote hivyo ni wajibu wa wafanyakazi ngazi mbali mbali kushirikiana kwa pamoja katika kufanikisha shughuli au kazi hiyo.

“Wafanyakazi sote pamoja na Wananchi kwa umoja wetu tushirikiane na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuweza kutimiza lengo lilokusudiwa”aliongeza  Muangalizi wa Ofisi Arafa.

Nao Wafanyakazi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar walisema kuwa wameitikia wito huo kwa kutekeleza agizo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanya usafi wa mazingira sambamba na kupamba mapambo katika Ofisi.

Sambamba na hayo walisema wameitikia wito huo kwa kuanza kukarabati Jengo la idara yao kwa kupaka rangi, kupamba ndani ya ofisi ili kuleta muonekano mpya wa mazingira ya ofisi na kumalizia kwa kufanya usafi pamoja na kuweka mapambo yaliyotakiwa.

Hatua hiyo ya ufanyaji wa usafi katika eneo la Idara ya Habari ni miongoni mwa agizo la Serikali kuu kwa Idara na taasisi mbali mbali za Serikali na binafsi kufanya usafi katika kipindi hiki cha kuelekea siku ya sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo kilele chake kitafanyika January 12 visiwani humu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.