Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Akifungua Soko Jipya la Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja Ikiwa Katika Shamrashamra za Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akikata utepe kuashiria kulifungua Soko jipya la Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja, kulia Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar. Mhe. Hamad Rashid Mohammed na kushoto Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu Bunge Kazi Ajira Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama, wakishuhudia hafla hiyo ya Uzinduzi wa Soko hilo kuadhimisha Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Mapinduzi matukufu ya Januari 12,1964 ndiyo yaliyoleta ukombozi hapa Zanzibar na yeyote aliyekuwa hayataki na anayabeza ni vyema akatafuta mahali akaenda.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa soko la Kinyasini, lililopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 yameongeza fursa kwa wananchi ambao wote wamefaidika nayo na hakuna hata mwananchi mmoja wa Zanzibar aliyekwua hakufaidika na Mapinduzi.

Mapinduzi yamefanyika kwa lengo la kuwapa hadhi Wazanzibari wote sambamba na kuwa huru kwani yameweza kuwakomboa watu wote wa Unguja na Pemba, shama na mjini.

Dk. Shein alieleza kuwa tangu Awamu ya Kwanza hadi leo hii, Awamu zote zinaendelea kuyaenzi, kuyatunza na kuyalinda Mapinduzi kwa nguvu zote sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza maendeleo yaliopatikana hivi sasa na yale yaliokuwepo kabla ya Mapinduzi na kuyafananisha hasa katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu jinsi ilivyoimarika hivi sasa na ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 katika maeneo yote ukiwemo Mkoa wa Kaskazini.

Alisisitiza kuwa soko hilo ni la wananchi wote wa Kaskazini A, B kwa maisha yao pamoja na wananchi wengine wa mikoa mengine ambao watakwenda kufuata mahitaji sokoni hapo.

Dk. Shein aliongeza kuwa si vyema soko hilo likageuzwa sehemu ya kupiga siasa na kuwataka wananchi kulitumia vyema soko hilo ili waweze kupata tija.

Alisema kuwa sehemu hiyo ni ya kihistoria na ni sehemu ya biashara, hivyo alisisitiza soko litumiwe vizuri na wanaouza wauze vizuri kwa kutambua kuwa wanaowauzia ni ndugu zao na wasiuze bidhaa zao kwa bei ambayo haishikiki.

Katika kuhakikisha kuwa haiba nzuri ya soko na mazingira yanayoonekana hivi leo yanakuwa endelevu lazima uwepo utaratibu mzuri wa kufanya usafi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa si muda mrefu Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kisasa kutoka Bububu hadi Mkokotoni huku akisisitiza kuwa hilo litafanyika kwani hajawahi kutoa ahadi asiitekeleza na cha kuomba ni uhai na uzima tu ili kila mmoja aweze kushuhudia ahadi hiyo.

Alisema kuwa barabara hiyo itakuwa ya kisasa na itakuwa na hadi ya soko hilo pamoja na hadhi ya watu wa Kaskazini huku akiahidi kwua barabara zote zilizojengwa katika mradi wa MIVARF kwa njia ya kifusi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itazitia lami kuanzia hapo mwakani katika bajeti yake ili kuwasaidia zaidi wananchi.

Pamoja na hayo, alisisitiza kuwa Muungano hauna mbadala kwani Muunganon ni uhai wa Watanzania wote ambao asili yake unatokana na Mmapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 pamoja na uhuru wa Tanganyika.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu Jenista Muhagama alieleza kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi muhimu ya Muungano ambayo ina malengo ya kuwasaidia wananchi katika kupambana na umasiki.

Alisema kuwa hatua hiyo ni kuhakikisha kuwa Serikali zote mbili zinaimarisha uchumi huku akitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa Mungano uliopo utaendelea kudumishwa kwa nguvu zote sambamba na kuendeleza mashirikiano yaliopo kati ya Serikali zote mbili.

Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi alieleza kuwa Wazanzibari ni vyema wakaheshimu tunu hiyo ya Mapinduzi iliyowatoa kwenye ujinga na iwapo kuna mtu anayakejeli Mapinduzi hayo basi hafai kuishi katika nchi hii.

Hakuna hata mmoja atakaebaguliwa katika kupata huduma katika soko hilo na watu wote watapata huduma bila ya ubaguzi kama ilivyo kwa huduma nyengine zote za maji, barabara na nyenginezo.

Alisisitiza kuwa ujenzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na kwa upande wake anaamini kuwa ni vyema wananchi wote wakamuunga mkono Dk. Shein pamoja na Serikali yake.

Alisema kuwa katika Muungano uliopo kuna mambo mengi yanafanywa na hakuna nchi zilizoungana ambazo zinapata mafanikio kama Tanzania kwani wapo watu ambao wanakuja kujifunza hapa Tanzania.

Alishangazwa na wale wote wanaosema wanataka kuleta ukombozi na kueleza kuwa hakuna ukombozi kwani tayari Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ndio yaliowakomboa wananchi wote wa Zanzibar.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Joseph Abdalla Meza alisema kuwa soko hilo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. Shein ambayo baada ya kuanza kuiongoza Awamu ya Saba ya uongozi wa nchi aliagiza wananchi wajenge maeneo bora na ya kisasa ya kuuzia bidhaa za kilimo na vitoweo na wanunuzi wapate bidhaa karibu na maeneo yao zikiwa katika hali ya ubora.

Alieleza kuwa soko hilo ni moja kati ya masoko yaliyojengwa katika Mikoa mbali mbali ya Jamhuri ya Muunagno wa Tanzania kupitia programu ya Miundombinu ya Masoko,Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).

Alisema kuwa soko la Kinyasini ambalo liko Wilaya ya Kaskazini A Unguja ndio soko kubwa kati ya masoko yote yaliojengwa kupitia Programu ya MIVARF Tanzania ambapo Kampuni ya ZECCON ndio iliyojenga soko hilo kwa gharama za TZS Bilioni 2.5.

Sambamba na hayo alisema kuwa kama masoko mengine soko hilo lina huduma ya vyumba viwili vya baridi kwa ajili ya kuhifadhia na kuongeza thamani ya mazao ya mboga, matunda, nyama, samaki na mengineyo na lina vibaraza 82 vitakavyotumiwa na wafanyabiashara ambavyo kati ya hivyo 18 vitatumika kwa nyama na samaki.

Alieleza kuwa ni tofauti ya soko la Kinyasini na mengine ni kuwepo kwa jengo la Utawala ambalo sehemu ya chini ndio vilipo vyumba vya baridi na huduma nyengine za msingi na sehemu ya juu ni ofisi 13 za utawala na uendeshaji wa huduma zitakazoonekana kufaa kuwepo sokoni kama vile za kifedha na takwimu.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.