Habari za Punde

Balozi Seif awaasa watendaji kufanya kazi kwa bidiii ili kuongeza ufanisi

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kutoka Kulia akizungumza na Watendaji Wakuu wa Ofisi yake kufuatia mabadiliko ya hivi karibu yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar ya Viongozi na Taasisi za Serikali.
 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Nd. Abdulla Hassan Mitawi, Mkurugenzi Utumishi Bi Halima Ramadhan Toufiq wakifuatilia hotuba ya Balozi Seif wakati akizungumza na Watendaji hao.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa Balozi Seif na Watendaji Wakuu wa Ofisi hiyo.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif  Mohamed akitoa muhtasari wa Kikao cha Watendaji wakuu wa Ofisi hiyo waliokutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
 Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ameir Makame Ussi akitoa Muhtasari wa Matayarisho ya Bajeti ya Ofisi hiyo mbele ya Kikao cha Watendaji Wakuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ofisini Vuga.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema jambo pekee litakalosaidia ufanisi wa kazi ni kwa Viongozi pamoja na Watumishi wa Taasisi za Serikali  kufanyakazi kwa bidii ili ile kiu ya Umma ya matarajio ya kupata huduma kutoka  Serikalni ifikiwe vyema.
Alisema bidii hiyo ni vyema ikaenda sambamba na Watumishi na viongozi hao kuwa na upeo wa ubunifu kwa lengo la kupata ufanisi wa Wizara ya Taifa kwa jumla wakiweka mbele ushirikiano wa karibu baina yao utakaofanikisha majukumu yao ya kila siku.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watendaji Wakuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kufuatia mabadiliko makubwa ya Viongozi na Taasisi za Serikali yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hivi karibuni.
Alisema haipendezi kumuona Katibu Mkuu wa Wizara anaonekana kuzunguuka na kirungu mkononi kuwaamuru Watendaji kutekeleza majukumu yao kitendo ambacho kila mtumishi anapaswa kuheshimu Kanuni na taratibu zote zilizowekwa za Utumishi Serikalini.
Balozi Seif alitahadharisha  Watumishi wa Umma kuepuka vitendo vya kupikiana majungu hasa katika maeneo ya Kazi wakizingatia mgawanyo wa majukumu yao ya uwajibikaji kitu ambacho kuendelezwa kwake kunaweza kusababisha hatari.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alihimiza uingiaji kazinini kwa wakati uliowekwa na kuhakikisha jukumu lao la kazi lilioko mkononi linamalizika na ndipo wafikie uamuzi wa kurejea Nyumbani.
Akizungumzia matayarisho ya Bajeti ya Mwaka 2018/2019 Balozi Seif Ali Iddi aliwakumbusha Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo kuangalia mambo ya kwanza muhimu na ya msingi ili kurahisisha utendaji wa kazi wao.
Balozi Seif alisema si vyema Kiongozi wa Idara au Taasisi ya Umma kudai au kulalamikia kitu ambacho hajakiweka katika Bajeti yake aliyoiandaa ndani ya Taasisi yake kwa Mwaka husika.
Akiwasilisha muhtasari wa matayarisho ya Bateti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ya Mwaka 2018/2019,  Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti Nd. Ameir Makame Ussi alisema Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo tayari wameshawasilisha mpango wa Bajeti kwa Taasisi hizo.
Nd. Ameir  alisema Bajeti hizo zimezingatia mfumo Mpya ujuilikanao MTF uliotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar ambao tayari umeanza kuchukuliwa hatua zinazostahiki.
Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed  Aboud  Mohamed alisema utendaji wa muda mfupi unaoendelea kuchukuliwa na Viongozi Wapya  kwa kushirikiana na waliopo umeonyesha mwanzo  mzuri wa matumaini.
Waziri Aboud alisema hatua hiyo itaongeza chachu ya uwajibikaji ndani ya Ofisi hiyo iliyokuwa tegemeo kubwa kwa Jamii hapa Nchini kwa kuzingatia kwamba  ndio inayosimamia utendaji mzima wa shughuli za Serikali Kuu.
Akigusia nidhamu kazini Mh. Mohamed Aboud alisema Uongozi wa Wizara chini ya Usimamizi wa Idara inayosimamia Utumishi imeanza kusimamia vyema nidhamu kazini kupitia mfumo maalum wa Teknolojia ya kisasa.
Alisema mfumo wa mashine Maalum iliyoweka kwa lengo la kukusanya kumbukumbu za Wafanyakazi wote itawezesha kudumisha nidhamu kazini kwa kutoa taarifa ya miendendo ya Watendaji wote bila ya kuonewa Mtu.
Naye  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdulla Hassan Mitawi alisema Ofisi hiyo inatarajia kuwa na Ukumbi wa Mikutano utakaokuwa na hadhi ya Mawasiliano ya Kisasa utakaowezesha kupatikana kwa mazungumzo ya moja kwa moja baina ya Zanzibar  na Tanzania Bara na hata kwa zile Taasisi za Kimataifa za nje ya Nchi.
Nd. Abdulla alisema uwekaji wa miundombinu hiyo inayotekelezwa na Kampuni ya Kizalendo ya Simu Tanzania {TTCL} unatarajiwa kukamilika hivi karibuni ili kurahisisha huduma za kiutendaji kwa kutumia mfumo huo wa mawasiliano ya Kisasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.