Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akiwasha mshumaa kama ishara ya kumbukumbu
ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya Rwanda. Kulia ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa
Mataifa Alvaro Rodriguez na kushoto ni balozi wa Rwanda nchini Eugene Kayihura.
Na: Mwandishi wetu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt
Harrison Mwakyembe, amewaasa Watanzania kuhakikisha wanapambana na viashiria vyote
vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na mauaji ya kimbari. Kauli hiyo Dkt. Mwakyembe ameitoa wakati wa maadhimisho ya
kumbukumbu za mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda miaka 24 iliyopita.
Kwenye hotuba yake Dkt. Mwakyembe amesema mauaji
ya kimbari hayatokei ghafla bali huanza kwa chokochoko na kauli za kichochezi
ambazo zina lengo la kuigawa jamii vipande vipande. “Kilichotokea Rwanda ni
fundisho kwetu, mauaji ya kimbari hayatakiwi kutokea tena. Kuhakikisha
hayatokei lazima tuyadhibiti mambo yote yanayoweza kuligawa taifa kwa faida ya
kizazi cha leo, kesho na keshokutwa” Dkt. Mwakyembe alisisitiza.
Kuendelea kutia mkazo wa ujumbe wake Dkt.
Mwakyembe aliinukuu kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli, aliyoitoa wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Rwanda ambapo alisema “haya hayatatokea tena, hatuwezi kubadili kilichotokea awali, lakini
tunaweza kubadilisha hali ya leo na hata ya baadae”.
Balozi wa Rwanda nchini mheshimiwa
Eugine Kayihura ameishukuru Serikali na wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kuwa
pamoja na Wanyarwanda. Pia ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kindugu kati ya
Tanzania na Rwanda kwa maendeleo ya watu wake.
Kwa upande wake Mratibu Mkazi wa Umoja
wa Mataifa, Alvaro Rodriguez amesema nchi zote zina wajibu wa kuwalinda
wananchi wake dhidi ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya
binadamu. Pia zinatakiwa kuhakikisha zinaungana kupambana na mtu au kikundi
chochote chenye nia ya kutekeleza uhalifu kama huo.
Kumbukumbu za mauaji ya kimbari ya
Rwanda huadhimishwa kila mwaka na mwaka huu maadhimisho hayo kwa Tanzania
yamefanyika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City ambapo Dkt. Mwakyembe alikuwa
mgeni rasmi. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali
wakiwemo mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, watu mashuhuri, viongozi
wa serikali na mashirika ya kimataifa na wanafunzi wa shule za sekondari za
jijini Dar-es-salaam.
No comments:
Post a Comment