Na.Mwashungu Tahir -Maelezo Zanzibar.
Tani 8,533.65 za karafuu zilinunuliwa na shirika la Biashara la taifa la Zanzibar (ZSTC) kutoka kwa wakulima Unguja na Pemba katika kipindi cha mwaka 2017 /2018.
Kati ya hizo, tani 290.88 zilinunuliwa Unguja na 8,242.76 kisiwani Pemba, zote zikiwa na thamani ya shilingi Bilioni 119.4.
Kiasi hicho kimevuka lengo, kwaini makadirio yalikuwa kununua jumla ya tani 6,770, amapo Pemba kulikisiwa kupatikana tani 6,500 na Unguja 270 kwa mwaka huo.
Akitoa mada kuhusu tathmini ya utekelezaji wa kazi za msimu wa mavuno ya karafuu kwa mwaka 2017/2018, Mkurugenzi Masoko wa ZSTC Salum Abdalla Kibe huko Mkokotoni Kaskazini Unguja katika mkutano na wakulima wa zao hilo, amesema manunuzi hayo ni sawa na asilimia 126 ya malengo yaliyowekwa.
Alisema kuwa, bei ya manunuzi kutoka kwa wakulima ilikuwa shilingi 14,000 kwa kilogramu moja ya karafuu za daraja la kwanza, shilingi 12,000 daraja la pili, na la tatu ni shilingi 10,000.
Aidha, alisema mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi chote hicho, yametokana na ushirikiano mzuri baina ya wakulima, masheha na wafanyakazi wa shirika hilo katika kusimamia vyema uendelezaji wa zao hilo ili kuhakikisha linaleta tija kwa wakulima na wananchi kwa jumla.
Mkurugenzi huyo pia, amesema, kwa mwaka huu, ZSTC imefanikiwa kuanzisha vituo 33 kisiwani Pemba vinavyoendelea kutoa huduma ya kununua karafuu kutoka kwa wakulima.
Hata hivyo, alisema kuwa, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa kwa wakulima kuchanganya karafuu zao na makonyo, matende na uchafu mwengine wanapopeleka vituoni kwa ajili ya kuziuza.
Aliitaja changamoto nyengine kuwa ni kuzianika bila kuzingatia maelekezo ya kuimarisha viwango vya ubora wanayopewa na wataalamu kwa kuacha kuzianika barabarani, sakafuni na kwenye mapaa ya nyumba.
Pamoja na hayo, pia alisema baadhi ya wakulima hawarejeshi kwa wakati fedha wanazokopeshwa na kulisababishia shirika gharama za ziada katika kufuatilia madeni.
Kwa upande wake, Ofisa Masoko kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Abdalla Jabir Abdalla, aliwasihi wakulima wa zao hilo na masheha kutumia huduma benki kwa njia ya simu za mikononi (Mobile Easy Pesa), kwa kuweka fedha zao.
Alisema kufanya hivyo, kutawaondoshea usumbufu wa foleni katika benki, pamoja na kujihakikishia usalama wa fedha zao.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi Mohammed, aliwashukuru wakulima wa zao hilo mkoani humo, pamoja na kuwazawadia wakulima bora wa kila wilaya mwaka huu.
Pamoja na zawadi za fedha, wakulima hao pia walitunukiwa vyeti pamoja na vitambulisho.
No comments:
Post a Comment