Habari za Punde

Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar Ravia Idarous Faina Ajiuzulu Nafasi Yake.

Na. Mwandishi Wetu.
RAIS wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ravia Idarous Faina,  ameandika barua rasmi ya kujiuzulu nafasi yake kukiongoza chombo hicho cha juu chenye kusimamia soka visiwani hapa.
Rais huyo sasa ataungana na Makamu wa Rais wa ZFA Unguja, Mzee Zam Ali na Mkurugenzi wa Ufundi, Abdulghan Msoma ambao walitangaza kujiuzulu mwishoni mwa mwezi Mei, 2018.
Katibu Mkuu wa ZFA, Mohammed Ali Hilali 'Tedy, amethibitisha kupokea barua hiyo ya Ravia ambayo hata hivyo,alisema, haikueleza sababu za kufikia uamuzi huo uliokuwa ukitarajiwa na wengi.
“Ni kweli ameandika barua ya kujiuzulu nafasi yake, barua ameileta leo Jumatano (jana) saa 9 za mchana”, alisema Tedy.
Ravia alipokea kijiti hicho cha Urais kutoka kwa Amani Makungu ambaye aliachaia madaraka muda mfupi baada ya kukaa madarakani.
Sakata la viongozi hao wa juu wa ZFA kutakiwa kuondoka madarakani lilikuja baada ya timu ya taifa ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 17 kuondolewa katika mashindano ya vijana yaliofanyika chini Burundi.
Zanzibar ilitimuliwa katika mashindano hayo kutokana na kukiuka kanuni za mashindano hayo,ikitajwa kupeleka vijeba.
Mbali ya kuondolewa kwenye michuano hiyo, pia Zanzibar ilipewa adhabu kulipa faini ya dola 15,000 ambapo fedha hizo zitafidia gharama za tiketi, malazi na chakula ya timu katika kipindi chote walichokaa Burundi.
Aidha, Zanzibar wamefungiwa kutoshiriki mashindano yanayoendeshwa na CECAFA hadi hapo watakapolipa faini hiyo ambayo inatakiwa kurudishwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.