Habari za Punde

UNFPA ITAENDELEA KUTOA MASHIRIKIANO KUENDELEZA UZAZI SALAMA ZANZIBAR

 MWAKILISHI wa UNFPA Tanzania Jacguline Mahon akizungumza na Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed kuhusu kuongeza ushirikiano juu ya uzazi salama na kuimarisha afya ya Mama na Mtoto, (kulia kwake)  ni Mwakilishi wa (UNICEF) Maniza Zaman 
WAZIRI wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizungumza na Wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
WAZIRI wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed katika akipiga picha ya pamoja na Wawakilisi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania, (kushoto) Mania Zaman wa UNICEF  na  Jacguline Mahon wa UNFPA (Picha na Abdalla Omar  Maelezo - Zanzibar).
Na Mwashungi  Tahir.  Maelezo Zanzibar.
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa linaloshuhulikia Idadi ya watu Duniani UNFPA Jaqline Mohan amesema Shirika lake litaendelea kutoa mashirikiano katika sekta ya afya hasa katika uzazi salama ili kuweza kuyanusuru maisha ya mama na mtoto.
Hayo ameyasema huko katika ofisi ya Wizara ya Afya Mnazi Mmoja wakati alipokuwa akielezea lengo la matarajio yao katika kusaidia mpango wa uzazi salama wa mama na mtoto.
Alisema afya na mama na mtoto ni muhimu katika jamii hivyo wataendelea kusaidia sekta hiyo ya afya  ili kuhakikisha kuwa kinamama wanapata huduma bora wakati wa kujifungua  pamoja na watoto kupata makuzi yaliyo salama ili kupunguza vifo wakati wa uzazi.
Alisema vifo vingi vya akinamama na watoto  hutokea wakati wa kujifungua hivyo huduma hiyo  itaweza kupunguza vifo na kusaidia kuwapa uzazi salama kwa kujenga afya bora na makuzi mazuri wa watoto.
 “Tuna mpango  wa kusaidia Wizara ya Afya katika mambo ya kijamii , uzazi salama kwa mama na mtoto na kushuhulikia vijana katika kujua afya zao” alisema mwakilishi huyo.
 Alieleza kuwa Shirika lake pia lina  lengo la kuwasaidia  vijana kwa kuhakikisha kuwa wanaishi  na afya bora , kuwapa uhuru wa kujipanga katika kujiletea maendeleo yao pamoja na kuwasaidia kwenye mambo ya kiuchumi. kwani  ndio nguvu kazi ya Taifa
Nae Waziri wa Afya Hamadi Rashid Mohammed amelishukuru shirika hilo kwa kutoa mashirikiano katika kuboresha afya za mama na watoto katika uzazi ulio salama.
Alisema watazidi kushirikiana  kwenye kutoa elimu zaidi  ya uzazi wa mpango ulio salama ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, kwani elimu ya uzazi  bado uzazi  wa mpango iko chini na kuwataka  akinamama kuwa na muamko wa kupanga uzazi ilikunusuru maisha yao pamoja na  kuwa na afya bora
“Elimu inahitajika zaidi kwa jamii na    iendelee kutolewa katika suala zima la uzazi wa mpango salama kwa mama na mtoto  na pia kuwashauri akina baba kuwapa fursa akina mama kujiunga na uzazi salama”, alieleza Waziri Hamad .
Waziri Hamad  alisema shirika hilo limesaidia kutoa dawa kwa ajili ya jamii ikiwemo  vifaa vya uzazi kwenye wodi ya uzazi katika Hospitali ya Mnazo Mmoja na mwembeladu pamoja na kutoa mafunzo wafanyakazi ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
 “ Uzazi wa mpango ulio salama umo mpaka katika vitabu vya  dini yetu ya kiislamu hivyo tujitahidini ili kuweza kuleta afya iliyo bora kwa mama na mtoto na kupata nguvu ya kulea mtoto miaka miwili na kupumzika angalau  mwaka mmoja”, alisema Waziri huyo.
 Mkurugenzi  Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi Mmoja   Ali Salim alisifu  jitihada wanazozitoa shirika hilo katika kuboresha sekta ya afya ya mama na mtoto  jinsi wanavyoweza kutoa juhudi za Afya za mama na mtoto katika kuweka uzazi ulio salama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.