Habari za Punde

Jumuiya ya Istikama Zanzibar Yakabidhi Msaada wa Fedha Kwa Wananchi wa Kisiwa Tumbatu Waliopata Maafa ya Upepo Wiki Iliopita.

WAFANYAKAZI wa Jumuiya ya Istikama Zanzibar wakiwa kwenye Boti wakielekea katika Kisiwa cha Tumbatu kwaajili ya kukabidhi  Msaada wa fedha kwa Wananchi waliopatwa na Maafa ya Upepo hivi karibuni.
MWENYEKITI wa kitengo cha Maafa  Jumuiya ya Istikama Zanzibar Said Hemed Alshaybar  akimkabidhi Msaada wa Fedha Bi. Dawa Jabiri Haji mkaazi wa Tumbatu Uvivini ambae Nyumba yake iliharibiwa na upepo.
MKURUGENZI Mtendaji Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Makame Khatibu Makame akimkabidhi Msaada wa fedha Makame Mdungi Makame mkaazi wa Shehiya ya Bomani.
MWENYEKITI wa Kitengo cha Maafa katika Jumuiya ya Istikama Zanzibar Said Hemed Alshaybar  akizungumza na Wananchi wa Tumbatu baada ya kukabidhi Msaada wa fedha kwa  waliopatwa na Maafa ya upepo.
SHEHA wa Shehiya ya Uvivini Hassan Muhidini akitoa shukurani kwa niaba ya Masheha wa Shehiya wenzake wa shehia tatu za Tumbatu, kwa Jumuiya ya Istikama, baada ya kukabidhiwa msaada wa fedha kwaajili ya kununulia vifaa vya ujenzi.(Picha na Abdalla Omar  Maelezo - Zanzibar.)

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar. 8.7.2018
Jumuiya ya Istiqama Zanzibar kwa kushirikiana na Radio Adhana imekabidhi msaada wa shilingi 13,600,000/  kwa wananchi wa Shehia tatu za Tumbatu waliopata maafa  ya upepo uliotokea tarehe 30 mwezi uliopita.
Mwenyekiti wa Kitengo cha Maafa Jumuiya ya Istika Zanzibar Said Hemed Al shaybar alikabidhi msaada huo katika hafla iliyofanyika Shehia yaTumbatu Uvivini na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Makame Khatib Makame.A
Al shaybar alisema Jumuiya ya Istiqama imepokea kwa masikitiko makubwa athari zilizosababishwa na upepo huo ambapo watu sita walijeruhiwa kwa kuangukiwa na bati na matufali na kuharibu nyumba 136 za wananchi na nyumba za Ibada na vyuo vya Qur ani.
Mwenyekiti huyo alitoa mkono wa pole kwa wananchi wote wa Tumbatu Maafa ya upepo huo na kuwaomba wawe wastahamilivu katika kipindi hiki kigumu  kwani hiyo ni Rehma za Mwenye-ez-Mungu.
Aliahidi kuwa Jumuiya ya Istiqama itaendelea kushirikiana na wananchi wote wa Zanzibar watakaofikwa na Maafa ya aina hiyo kwa kuwapatia msaada wa hali na mali utakaoweza kuwasaidia kuwapunguzia  matatizo.
Hata hivyo aliwataka wananchi waliopata msaada huo kuutumia katika malengo yaliyokusudiwa ya kununua vifaa vya ujenzi ili waweze kurejea katika hali ya maisha ya kawaida.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Kukabaliana na Maafa Zanzibar Makame Khatibu Makame alisema uwamuzi wa Jumuiya ya Istikama ya kutoa msaada huo ni kusaidia juhudi za Serikali za kuwafariji wananchi wanaopatwa na maafa ya aina hiyo.
Alisema Serikali kwa upande wake ilianza kutoa msaada kwa wananchi waliopata maafa hayo katika shehia tatu za uvivini, Bomani na Mtakuja mara tu baada ya kutokea na hatua ya Jumuiya Istikama ni muendelezo wa kuwasaidia wananchi hao.
Aliwashauri wananchi wa Zanzibar kuendelea kuungana na kushirikiana hasa panapotokezea matatizo ya kiminaadamu bila kujali tofauti zao kwani kufanya hivyo ni kuendeleza umoja na udugu uliopo.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.