Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Shein, Amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Uongozi wa Ofisi Yake Kwa Ushirikiano Wao.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amempongeza Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd kwa kumsaidia kazi na kuendelea kuisimamia vyema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.  

Dk. Shein  aliyasema hayo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wakati ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2017/2018, na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2018/2019.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongezi kwa Makamo wa Pili wa Rais  Balozi Seif Ali Idd kwa  kumsaidia kazi pamoja na kuupongeza uongozi wa Ofisi hiyo na watendaji wake kwa kufanya kazi zinazoonekana na zisizoonekana zikiwemo Mazingira na UKIMWI.

Pia, alimpongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wengine wote wa Ofisi hiyo kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya ndani ya Ofisi hiyo pamoja na nje ya Ofisi hiyo ikiwemo katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Pamoja  na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya usimamizi katika utekelezaji wa majukumu  ya kazi hatua ambayo huleta ufanisi mkubwa pamoja na uwajibikaji kazini.

Alieleza kuwa kuanzishwa kwa taasisi za utafiti ambazo zimeundwa kwa mujibu wa Sheria kuna umuhimu mkubwa katika kufikia malengo yaliokwekwa juu ya suala zima la tafiti hapa Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa upimaji wa UKIMWI ni jambo la hiyari hivyo alitoa  wito kwa uongozi huo kuendelea kutumia utamaduni wa kuwashajiisha wananchi kwenda kupima badala ya kuwalazimisha.

Hivyo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kutoa elimu kwa jamii juu ya suala zima la kupima UKIMWI hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliokusudiwa.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliendelea kusisitiza haja na wajibu kwa kiongozi katika kusimamia na kuwajibika katika utendaji wa kazi.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uwasilishaji Mpango Kazi na utekelezaji wake uliofanywa na Wizara hiyo na kusisitiza haja ya kwa uongozi wa Ofisi hiyo kuendelea kujenga taswira nzuri na kuwa mfano kwa wengine.

Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa  alieleza kuwepo kwa Kitengo cha kufuatilia maagizo na maelekezo ya Serikali ambacho tayari kimeshaanza  kazi hivyo mashirikiano yanahitajika kwa uongozi wa Wizara zote za Serikali na taasisi zake ili kufanikisha majukumu hayo.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais  Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed  alitoa pongezi na kumshukuru Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuiongoza vyema Zanzibar na kusimamia ipasavyo utendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwaletea maendeleo.

Uongozi huo ulitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa maelekezo na miongozo anayowapa ambayo imesaidia sana katika kutekeleza majukumu yao kwa wananchi.
“Tunamuomba Mola akuzidishie hekima, busara na afya  njema ili uzidi kutuongoza”, alisema Waziri Aboud.

Aidha, uongozi wa Ofisi hiyo  juhudi zake katika kupambana na dawa za kulevya ambapo Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar imeendesha mafunzo kwa Wahusika wa Madiko katika Shehia zenye bandari zisizo rasmi, kuteketeza dawa kutoka katika sehemu zilizo hifadhiwa pamoja na kufanya shughuli nyenginezo.

Pia, Uongozi huo  ulieleza mikakati iliyoiwekwa katika kupiga vita dawa za kulevya hapa Zanzibar pamoja na mashirikiano yaliopo kati yake na taasisi ziliopo nje ya Zanzibar katika kupambana na kadhia hiyo.

Katika maelezo pia, Waziri Aboud alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi zitaendea kuchukuliwa katika kuhakikisha elimu inatolewa juu ya suala zima la UKIMWI na maambukizi yake.

Pia, uongozi huo hatua zinazoendelewa kuchukuliwa katika kuhakikisha Miongozo ya miundombinu rafiki ambayo iko katika hatua ya mwisho kutekelezwa na huku ikiwekwa mikakati katika kuhakikisha jamiii inahamasika juu ya suala hilo kwa lamkuhakikisha mioundombinu ina kuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu.
  
 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.