MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kinachotakiwa siku ya Oktoba 27,
2018 katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe ni kuhakikisha heshima ya CCM
inaendelea kuwepo katika Jimbo hilo kwani lina historia kubwa.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika uwanja wa Muembe Matarumbeta, Jimbo la Jang’ombe, Wilaya
ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja katika mkutano wa kufunga Kampeni
za Jimbo hilo ambazo zilianza Oktoba 14, 2018 na uchaguzi wake unatarajiwa
kufanyika Jumaamosi Oktoba 27 mwaka huu.
Alisema kuwa ushindi
wa CCM itaendeleza heshima na historia ya Jimbo hilo kwani Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alisisimama
kuwa mgombea wa wa Chama cha ASP mnamo mwaka Januari 1961 ambapo alipata kura 3028
na kuwashinda viongozi wawili walioungana kwa pamoja kutoka kambi ya upinzani
wapinzani waliopata kura 216 TU.
Akitoa historia hiyo
Rais Dk. Shein alisema kuwa katika uchaguzi uliofuata Mzee Karume pia,
aliendelea kushinda na kupata kura zipatazo 5701 katika uchaguzi wa mwezi Juni na kuwataka wananchi kuyafanyia
kazi maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi wao katika mikutano ya kampeni za
Jimbo hilo.
Katika maelezo yake
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, alieleza kuwa Jimbo la Jang’ombe ni
lazima lirudi mikononi mwa CCM kwani lina historia kubwa ndani ya chama
hicho.
Alisema kuwa Ramadhani
Hamza Chande hakupendelewa na ameteuliwa kwa sifa, uwezo na heshima pamoja na uwanachama
wake wa CCM na uzalendo wake mkubwa alionao pamoja na imani ya nchi yake na
Jimbo lake.
Dk. Shein alisema kuwa
huo ni uchaguzi mdogo, lakini hakuna
uchaguzi mdogo uliokuwa haufanyiwi kampeni wala wanachama wake hawahangaiki
hivyo, ni lazima wanaCCM wa Jimbo hilo wahakikishe wanakipigania chama chao na
wanakipa ushindi.
Makamo Mwenyekiti huyo
wa CCM Zanzibar alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. John Pombe Magufuli
kwa kuendesha kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanya uwamuzi wa
kumteua Ramadhan Chande kwani ni uwamuzi sahihi wa kuwaletea ushindi wanaCCM wa
Jimbo la Jang’ombe.
Dk. Shein alimpongeza Makamu
Mwenyekiti wa CCM Bara Philip Mangula kwa kuja kuzindua Kampeni hizo hapa
Zanzibar mnamo tarehe 14 mwezi huu ambapo leo zimefungwa rasmi na kuwataka
wananchi na wanaCCM kumchangua mgombea huyo na kuwapongeza viongozi wote
waliokuwa wageni rasmi katika mikutano kadhaa iliyopangwa.
Licha ya mvua zilizokuwa
zikinyesha katika eneo la mkutano huo, wanaCCM na wananchi walijitokeza kwa
wingi na kumsikiliza Rais Dk. Shein ambaye na yeye kwa upande wake aliwapongeza
wanaCCM wa Jimbo la Jang’ombe kwa kuhudhuria kwa wingi katika mikutano yote ya
chama hicho tokea kuanza mikutani ya Kampeni na kuwataka kutofanya kosa na
badala yake wamchangue Ramadhan Hamza Chande .
Rais Dk. Shein alisema
kuwa katika uchaguzi huo mdogo hakuna Ilani mpya ya CCM ila kuna mgombea mpya
wa Jimbo la Jang’ombe ambaye atatekeleza Ilani hiyo na kusisitiza kuwa Serikali
imetekeleza Ilani hiyo ndani ya miaka mitatu kwa mafanikio makubwa sana ikiwa
ni pamoja na kuimarisha sekta za jamii,kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuimarisha
sekta ya afya, maji, elimu, uzalishaji na nyenginezo.
“Na wapo wanaosema
hatujafanya kitu, nawambia yaguju” Dk. Shein alisema kuwa mafanikio makubwa
yamepatikana katika kuipatia Zanzibar maendeleo ikiwa ni pamoja na Utiaji
Saini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia, hafla
iliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar.
Kutokana na hatua hiyo
iliyofikiwa na Zanzibar, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wote wa Zanzibar
kutulia kwani mambo mazuri zaidi yanakuja na wale wote waliosema hayawi wasiwajibu
wawatazame watayaona na watayaacha wenyewe.
Alisema kuwa pamoja na
mafaikio yaliopatikana katika Majimbo ya Unguja na Pemba ndani ya Majimbo yote hayo
54 pamoja na Jimbo la Jang’ombe bado zipo changamoto ambazo Serikali inaendelea
kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Alisema kuwa wapo watu
wanaoshutumu kuwa skuli ya Kidongochekundu ambayo imejengwa mwaka 1956 imetupwa
jambo ambalo sio la kweli na kueleza kuwa skuli hiyo kamwe haiwezi kutupwa na badala
yake itatengenezwa na kuwa ya kisasa kwani fedha zipo.
Alisema kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inayafanya juhudi katika kuhakikisha inawafikisha
huduma za maji katika Majimbo ya mji wa Zanzibar likiwemo Jimbo la Jang’ombe
kwa gharama ya Dola milioni 21 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ili kuhakikisha
tatizo la maji linaondoka kabisa.
Alieleza kuwa tayari
mchakato wa kusambaza mabomba kutoka visima vikubwa 9 vilivyopo Bumbwisudi
unaendelea ambapo tayari mabomba yameashaanza kuwekwa na Kampuni kutoka China
na si muda mrefu mradi huo utakamilika.
Alisema kuwa hakuna
mda mrefu mambo hayo yatakamilika na kueeleza kuwa katika suala zima la ujenzi
wa barabara za ndani zikiwemo za Jimbo la Jang’ombe zitajengwa kwani kutojengwa
kwake kumetokana na uhaba wa vifaa vya kutengenezea barabara ambavyo hivi
karibuni vitawasili.
Dk. Shein aliwaahidi
wananchi wa Jangombe kuwa barabara zao za ndani zitajengwa na kwa kiwango cha
lami na kueleza kuwa kama ahadi aliyoiahidi ya ujenzi wa mtaro mkubwa kwa ajili
ya kutoa maji machafu aliyoiahidi wakati
akigombea urais alivyoitekeleza na hilo halina mjadala.
Akieleza hatua
zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha
inanunua vikalio, tayari vikalio vipatavyo 44,000 vishanunuliwa kutoka China ambavyo
vitawasili hivi karibuni na vitasambazwa katika skuli zote za Unguja na Pemba
ikiwemo skuli ya Kidongochekundu na Jangombe.
Makamo huyo wa
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alisema kuwa Hospitali ya jumba la vigae
imeshakarabatiwa na wagonjwa wa akili ya Kidongochekundu inafanyiwa matengenezo
makubwa huku hatua za Serikali za
kujenga hospitali mpya ya kisasa huko Binguni zikiendelea ambayo itasaidia
katika kutoa huduma mbalimbali.
Alisema kuwa CCM haina
papara wala pupa kwani siasa inaijua na chama hicho kimekuwa kikiimarika kila
siku na kusema kuwa hakuna jambo ambalo limeahidiwa na hivi sasa haitekelezwi.
Alisema kuwa Jang’ombe
ina heshima kubwa sana ni Jimbo la historia na viongozi wengiwa Zanzibar wametoka
katika Jimbo la Jangombe “Jangombe ina wenyewe na wenyewe ni CCM, na tarehe 27
ni lazima mkaiendeleze historia hiyo”,alisisitiza Dk. Shein.
Akimuelezea mgombea
huyo, Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema kuwa Ramadhan Hamza Chande
anapenda watu wake na ana heshima kwa watu wake na wazee wake na wa wenzake na
majirani zake ambaye pia, ana sifa zinazofaa za kuwa Mjumbe wa Jimbo la
Jangombe “Hakuna aliyekuwa hana udhaifu kwani hakuna aliyekamilika hata mmoja”alisisitiza
Dk. Shein.
Dk. Shein aliwahimiza
wanaCCM wa Jimbo hilo kutofanya dharau kwani hakuna dharau katika kuongoza dola
hivyo, kuna kila sababu ya kuipa ushindi CCM kwani chama hicho kinataka watu wenye
uwezo na kutokana na uwezo alionao Ramadhan Hamza Chande anaweza kuwa
Mwakilishi mzuri wa Jimbo hilo.
Dk. Shein
alimtambulisha Ramadhan Hamza Chande kwa wanaCCM na wananchi wa Jimbo la Jang’ombe
na kuwataka kumchagua mgombea huyo kwani anaijua Ilani ya CCM na ataitekeleza
kwa mashirikiano ya viongozi wengine wa chama hicho na mashirikiano ya Serikali
kwa jumla.
Nae Ramadhan Hamza
Chande alitoa shukurani kwa wanaCCM wote pamoja na wananchi walioshiriki katika
Kampeni hizo pamoja na kuwapongeza viongozi wote waliomchagua kuanzia ngazi za
chini hadi juu.
Mgombea huyo alimuahidi
Rais Magufuli kuwa amekubali kutekeleza Ilani ya Chama hicho na kuahidi
kuitekeeleza kwa vitendo na kushirikiana na viongozi wote waliomtangulia.
Aliwataka wanaCCM na
wananchi wa Jimbo la Jangombe kumpa mashirikiano ili kuweza kushinda uchaguzi
huo huku akiwataka wananchi na wanaCCM wa Jimbo hilo kushirikiana katika
kulijenga Jimbo lao hilo la Jang’ombe.
Nae Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alieleza mafanikio ya CCM na kusema kuwa
mgombea wa CCM nafasi ya Uwakilishi katika jimbo hilo ana sifa zote
zinazohitajika hivyo wananchi wanapaswa kumchagua.
Alisema kuwa Kampeni
za CCM zimeenda vizuri sana kutokana na viongozi wa Jimbo hilo pamoja na
Serikali kutekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM kwa vitendo.
Alisema kuwa CCM ni
chama cheye uwezo, upeo pamoja na kuweza kuwaunganisha watu ili waishi kwa pamoja
na ndicho chama pekee kilicholeta maendeleo.
Mamia ya wananchi na
wanaCCM walihudhuria katika mkutano huo wa kufunga Kampeni za Uchaguzi wa Jimbo
la Jang’ombe ambapo uchaguzi wa Jimbo
hilo unafanyika baada ya aliyekuwa Mwakilishi
wake Abdalla Maulid Diwani kufukuzwa uanachama katika chama hicho.
Viongozi mbali mbali
wakiwemo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein
kwa kutekeleza vyema Ilani ya Uhaguzi ya CCM ikiwa ni pamoja na kuulinda na
kuuendeleza Muungano.
Walieleza kuwa kuna sababu
nyingi za Kumchagua Ramadhani Hamza Chande na kuichagua CCM kwani mgombea huyo
ana uwezo huku wakisisitiza kuimarisha amani na utulivu.
Viongozi kadhaa
walihudhuria katika mkutano huo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Idd, ambapo mkutano huo ulienda sambamba na burudani kutoka vikundi mbali mbali vikiwemo vya muziki pamoja
utenzi Maalum.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment