Habari za Punde

UNICEF KUISAIDIA SERIKALI KUFANYA TAFITI ZA MAENDELEO YA MTOTO

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na  Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na  Ujumbe wa UNICEF  ukiongozwa  na Mkurugenzi wa Shirika hilo  Kanda ya 
Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika Bi. Leila Pakkala katika Mkutano Jijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akieleza kuhusu Serikali kuwa na Dawati linaloshughulikia bajeti ya maendeleo ya watoto wakati wa Mkutano na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika Bi. Leila Pakkala (hayupo pichani) uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika  ukiongozwa na  Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Leila Passala (katikati), wakifatilia kwa makini maelezo ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, (hayupo pichani) kuhusu elimu, lishe na sheria ya  mtoto, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma. 
 Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika Bi. Leila Pakkala akieleza nia ya Shirika hilo ya kusaidia kufanya tafiti za maendeleo ya mtoto nchini Tanzania, wakati wa Mkutano kati yake na  Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (hayupo pichani),  Jijini Dodoma.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na  Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na  Ujumbe wa UNICEF  ukiongozwa  na Mkurugenzi wa Shirika hilo  Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika Bi. Leila Pakkala katika Mkutano Jijini Dodoma. 
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka  Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika  ukiongozwa na  Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Leila Pakkala (wa kwanza kulia) na baadhi ya maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kumalizika kwa Mkutano ulioangazia maendeleo ya mtoto, Jijini Dodoma.

Na: WFM - Dodoma
Shirika la Umoja wa Mataifa  la Kuhudumia Watoto ( UNICEF), wameonesha nia ya kuisaidia Serikali ya Tanzania kufanya tafiti mbalimbali kuhusu maendeleo ya mtoto ili kukabiliana na changamoto zinazomkabili.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, baada ya mkutano wake na Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Leila Pakkala, uliofanyika ofisi za Wizara hiyo Jijini Dodoma.
Dkt. Mpango alisema kuwa Shirika la UNICEF, lina nia yakushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ili kuweza kufanya tafiti katika mikoa mbalimbali, kuzichapisha na kuzisambaza ili kuongeza uelewa wa watu kuhusu  maendeleo ya watoto.
“Watu wengi wanajua uwekezaji kwa maana ya barabara na miundombinu mingine mikubwa lakini katika mazungumzo yetu tumesisitiza kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya watu hasa katika umri mdogo kwa kuwa usipowekeza katika umri huo na kuwekeza katika umri mkubwa matokeo yake hayawi mazuri.”, alisema Dkt. Mpango.
Alisema kuwa, maeneo ambayo ni muhimu kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na UNICEF ni pamoja na udumavu, elimu kwa ajili ya watoto hasa ambao hawajafikia umri wa kwenda shule na sheria ya mtoto katika kuhakikisha anakua salama kwa lengo la kulitumikia taifa kwa siku za usoni, hivyo alisisitiza kuwekeza  mapema kwa mtoto katika afya, lishe, elimu, uhuru wao na usalama hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kulitumikia Taifa kwa wakati ujao.
Aidha Dkt. Mpango alisema kuwa,  Serikali inafanya  jitihada kubwa kusimamia maendeleo ya uchumi kwa ujumla,  kwa kuwa Taifa lisipokuwa na uchumi imara haliwezi kuwekeza katika maendeleo ya watoto.
Alisema bajeti zinatakiwa kuweka umuhimu wa kuwekeza katika mtoto hivyo kuna Kitengo kinachohakikisha bajeti ya Serikali Kuu na Halmashauri zinazingatia mambo ya msingi ambayo yatasaidia watoto wa Tanzania kuwa na maendeleo stahiki.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika Bi. Leila Pakkala, amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika maendeleo ya mtoto jambo ambalo linastahili pongezi na pia ameipongeza Serikali kwa ukuaji wa uchumi, kupambana na rushwa, ujenzi wa miundombinu na kuongeza mapato ya ndani kupitia kodi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto- UNICEF,  kwa juhudi zinazofanywa kuhakikisha maendeleo ya mtoto nchini Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla kwa kuwekeza katika lishe na elimu ili kuwa na kizazi kijacho chenye uelewa wa kutosha ili kuleta tija katika Sekta za Maendeleo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
                                              Wizara ya Fedha ya Mipango

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.