Habari za Punde

Balozi Seif Ali Iddi Akiwa Katika Ziara Yake Mkoani Shinyanga.

Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akikaribishwa kuingia katika Mkutano wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama.
Kamisaa wa CCM Mkoa wa Shinyanga ambae pia ni Mkuu wa Mkoa huo Mh.Zainab Telak akimhakikishia Mlezi kwamba Mkoa wa Shinyanga uko salama.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi,akihutubia Wanachama wa CCM Mkoa wa Shinyanga akiwa katika ziara yake.
Mke wa Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama Mama Asha Suleiman Iddi akiwatahadharisha Wana CCM kuepuka kuwa na sura mbili katika kukitumikia Chama.
Viongozi wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga wako makini kufutia yaliyo jiri kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Mlezi wao Kichama Balozi Seif hayupo pichani.
Picha na – OMPR – ZNZ.
 Na.Othman Khmis OMPR.                        
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema wana CCM hawanabudi kuendeleza Umoja wao utaowapa nguvu za kujihakikishia kuondoza Dola ya Tanzania kwa Miaka mingi ijayo.
Alisema tabia ya baadhi ya wanachama kuhasimiana kwa sababu za tofaurti zao za kuwania uongozi wakati wamchakato wa kuwania nafasi za Uchaguzi ni kutoa mwanya kwa upinzani iwapo hawataamua kuacha makundi yaliyokuwepo wakati wa mchakato huo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo akiwa mlezi Mpya wa Mkoa wa Shinyanga Kichama alipofika kujitambulisha rasmi wakati akizungumza na Uongozi wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kahama na ile ya Mkoa wa Shinganya Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama.
Alisema udhaifu  ndani ya Uongozi wa Chama hujichomoza  pale yanapoanza makundi wakati wa mchakato jambo ambalo muongozo wa Chama huridhia hadi pale anapopatikana mgombea Mmoja anayepaswa kuungwa mkono na makundi yote yaliyokuwepo wakati wa mchakata.
Balozi Seif  aliwaeleza Viongozi hao wa Kamati za Siasa za Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga kwamba Dini zote zimekuwa zikisisitiza upendo na mshikamano unaopaswa kuendelezwa na Viongozi pamoja na wanachama wote wa Chama hicho kikongwe Barani Afrika na Ulimwengni kwa ujumla.
Akizungumzia vita dhidi ya Rushwa, Dawa za kulevya na Udhalilishaji wa Kijinsia Balozi Seif  ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Mkoa wa Serikali na Chama kushirikiana katika kuona vita hiyo inafanikiwa vyema.
Alisema kazi hiyo inapaswa kufanywa kwa pamoja na Wabunge waliomo ndani ya Mkoa huo sambamba na kutekeleza ahadi walizotoa kwa wapiga kura wao wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita.
Balozi Seif alisema wao ndio kielelezo cha Chama katika utekelezaji wa majukumu yao, kinyume na hilo utumishi wao hautaweza kuleta afya katika chama, Serikali na Jamii kwa ujumla.
Akikifungua Kikao hicho Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kahama Nd. Thomas Muyonga alimuomba Mlezi huo wa Chama Mkoa wa Shinyanga kuzifanyia kazi changamoto zinazoukabili Mkoa huo ili utekelezaji wa Ilani uende kama ilivyopangwa.
Alisema yapo masuala ambayo yanahitaji nguvu kubwa ya Chama na Serikali Taifa katika kuyatatua au kuyapatia ufumbuzi wake. Hivyo alisema Mlezi kwa sasa atakuwa na wajibu wa kulisimamia hilo akiwa kiungo kati ya ngazi zote mbili.
Akimkaribisha Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa huo Nd. Mabala Mlolwa alizipongeza Serikali zote mbili Nchini Tanzania ile ya Jamuhuri na ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Utekelezaji sahihi wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2015.
Nd. Mabala alisema utekelezaji huo umeshamiri na kuridhiwa na Wananchi walio wengi kwa vile umelenga kusimamia vyema udhibiti wa mapato ya Serikali kwa kuziba miyanya ya Rushwa jambo ambalo limeongeza kasi ya kuwatumikia vyema wananchi hasa wanyonge.
Mapema asubuhi akipokewa katika Uwanja wa ndege wa Kahama Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif  alisema uteuzi wake kwa upande mwengine utasaidia kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema Muungano huo umekuja baada ya Tanganyika kupata Uhuru wake Mwaka 1961 na Zanzibar kufanya Mapinduzi Tarehe 12 Januari Mwaka 1964 ambapo Mwezi ujao unatimiza Miaka 55 katika maadhimisho yatayofanyika Kisiwani Pemba.
Balozi Seif  alisema Wana Shinyanga wana haki ya kujivunia Mapinduzi hayo ambapo alisema Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar itazingatia kutoa mualiko kwa baadhi ya Viongozi wa Kisiasa na Serikali wa Mkoani Shinyanga kushiriki Kilele hicho.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi ameteuliwa kuwa Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga ambapo kipindi kilichopita alikuwa Mlezi wa Mkoa wa Magharibi Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.