Habari za Punde

Mahakimu na Mawakali Wana Mchango Mkubwa Katika Kuinua Uchumi wa Nchini -Jaji Mshibe.

Na Raya Hamad OR-KSUUUB
Mwenyekiti wa Tume ya kurekebisha Sheria Mh. Jaji Mshibe Ali Bakari, amesema mahakimu na mawakili wana mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi na kuleta maendeleo yatakayo pelekea kuwa maendeleo endelevu hapa nchini. 

Jaji Mshibe ameyesema hayo katika mkutano wa kupitia uchambuzi wa kurekebisha sheria iliowashirikisha mahakimu na mawakili wa serikali na wa kujitegemea uliofanyika katika ukumbi wa Malaria, Mwanakwerekwe katika wilaya ya Magharibi B.

Jaji Mshibe amesema wawekezaji kabla ya kuwekeza kuna vigezo wanavyovitumia ikiwa ni pamoja na kuangalia utendaji wa Mahakama  na mwenendo wa kesi inazozisimamia, uwepo wa sheria zinazoendana na hukumu wanazozitoa ,  muda wa kesi, hivyo amewataka mahakimu na mawakili kuzitumikia vyema nafasi zao kwa uadilifu na uaminifu katika kujenga Imani kwa wawekezaji. 

Amesema hakimu anatakiwa awe na upeo mkubwa na uelewa kwa kile anacho kihukumu, pia uwezo wa kuchambua kabla ya kutoa hukumu ili kujenga imani kwa jamii kwa vile sheria zinatungwa kwa maslahi ya wote na haimbagui mtu au kikundi cha watu ama taasisi fulani .

“Kitu unachokitolea hukumu ufanye jitihada zako maalum kuangalia aliyekuwepo mbele yako anahitaji hukumu ya aina gani badala ya kuangalia kitabu tu, usinyanyue kitabu kabla ya kusikiliza kesi”, alisisitiza Jaji Mshibe.

Mahakimu wanalo jukumu la kuijenga jamii bora na kuleta maendeleo kulingana na elimu walizonazo kwani mazingira yoyote wanayoyatengeneza yatachangia kuleta maendeleo ya nchi. 

Awali katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Nd. Kubingwa Mashaka Simba, amesema utafiti unaofanyika unalenga kufanya uchambuzi utakaoweza kusaidia kutengeneza sheria, pia kuangalia sheria za zamani zilizofutwa iwapo hakuna kitu kinachohitajika kwa wakati huu, pamoja na kufanya mapitio ya kina ili kuwa na sheria zinazotekelezeka.

Kubingwa amesema Tume imefanikiwa kuanzisha utaratibu wa utafiti unaongoza kazi zote za mapitio ya sheria za Zanzibar ambao umezingatia matayarisho ya awali kuhusiana na sheria iliyopendekezwa kurekebishwa, majadiliano ya  mawazo ya msingi kuhusiana na sheria husika , utafiti wa wazi, mazingatio ya wadau, pamoja na ripoti ya mapendekezo ya matukio ya utafiti 

Akitoa utangulizi juu ya uchambuzi wa baadhi ya vipengele vya sheria, Nd. Mohamed Khamis mwanasheria wa serikali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, amesema zipo sheria zilizofutwa lakini hakukuwa na maelezo na mapendekezo kwa nini zilifutwa ambazo nyingi ni zile zilizofutwa kabla ya  mapinduzi ya mwaka 1964, hivyo lengo la kukutana na kufanya mapitio hayo ni kubaini uimara na ubora wa sheria zilizopita ambazo nyingi ni zile za kabla ya mapinduzi

Mapitio ya sheria  yana  lengo la kukuza uchumi, kuweka mustakabali mwema na jamii inayobadilika kwa kasi kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknologia ambayo mara nyingi huathiri mazingira yanayotunguka  hivyo mapitio muhimu ya sheria za Zanzibar yanayoendelea yatazaa matunda katika kurahisisha utendaji mzima wa sekta ya sheria na sekta nyenginezo , na hatimae kufanikisha utoaji wa haki na kuimarisha utawala bora nchini ambao ndio msingi wa maendeleo .

Mohamed amewaomba mahakimu na mawakili hao kupitia vyema uchambuzi wa sheria tokea awali kuanzia tulikotoka ili kutoa muongozo wa sheria hata kama kuna sheria ambazo zilifutwa   na kutolea mfano kuwa zipo sheria ambazo zimefutwa lakini maendeleo makubwa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara yalifikiwa kabla ya kufutwa kwa sheria hizo hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa wahusika kuzipitia tena  sheria hizo ili ziendelee kuleta manufaa kwa nchi mbili hizi 

Nao washiriki wameiomba Tume hiyo kuangalia na kuzichambua kwa upeo mkubwa  sheria ambazo zinafanya kazi sana katika matumizi ya kawaida ili kubaini uimara na ubora wake na namna zinavyotekelezeka   

Miongoni mwa majukumu Tume ya kurekebisha sheria ni kufanya mapitio endelevu ya sheria za Zanzibar ili ziweze kukidhi haja kisiasa, kijamii, kiuchumi na kimazingira  na inawajibu wa kupendekeza mabadiliko ya sheria kwa mujibu wa mazingira ya Zanzibar, kuhakikisha sheria zinatoa haki na usawa

Kutafsiri sheria ili zifahamike kwa wanajamii ,kushauri njia mpya za utekelezaji wa sheria kuziweka pamoja  sheria za Zanzibar , kutoa elimu kwa wananchi ili wapate uwelewa wa sheria zao, kuimarisha mashirikiano na taasisi za kimataifa zenye majukumu sawa na Tume na kuchapisha makala ya sheria za kimataifa ndani ya Zanzibar  ikiwa makala hayo yanakwenda sambamba na maadili ya Mzanzibari



Tume ya Kurekebisha Sheria tayari imeshafanya mapitio hayo ya uchambuzi kwa kuwashirikisha wanasheria kutoka wizara  mbali mbali na Asasi za kiraia yaani NGO 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.