Habari za Punde

Tamasha la Wasanii wa muziki wa kizazi kipya kufanyika kesho

 Rais wa Kikundi cha Sanaa Zanzibar ( Zanzibar Fleva Unit ) Mohamed Abdallah Laki (katikati) akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo kuhusu Uzinduzi wa Tamasha la Mapinduzi Safari la Miaka 55 kuanzia kesho.
  Msemaji Mkuu wa Kikundi cha Sanaa  Zanzibar ( Zanzibar  Fleva Unit )  Rashid Msabaha akiwaelezea  Waandishi wa habari lengo la Uzinduzi wa Tamasha la Mapinduzi Safari la Miaka  55 katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Muandishi wa habari wa Zanzibar leo Mwinyimvua akiuliza Suali juu ya  Uzinduzi wa Tamasha la Mapinduzi Safari la Miaka 55 katika  Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Picha na Maryam Kidiko .
Na Mwashungi Tahir    Maelezo                    
Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Mjini Unguja Khatib Abraham Khatib anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Wasanii wa  muziki Zanzibar  kizazi kipya linalotarajiwa kufanyika hapo kesho tarehe 15-12-2018 huko katika Shehia ya  Mpendae.
Hayo ameyazungumza Rais wa Kikundi cha Sanaa Zanzibar ( Zanzibar Flever Unit )   Mohamed Abdullah Laki  huko katika ukumbi mdogo wa Studio Rahaleo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tamasha hilo ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra ya Miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu.
Alisema lengo la Tamasha hilo ni kuijulisha jamii kwa kupitia  wasanii wa  muziki  umuhimu wa Mapinduzi  Matukufu yaliyofanyika 1964 Visiwa vya Zanzibar na kufanya  vizazi  kuwa huru na kujitapa kwenye Nchi yao.
“Lengo kubwa la Tamasha hilo ni Wananchi kupatiwa elimu na  kuelimishana juu ya Mapinduzi yetu na kuzithamini nguvu za wazazi wetu waliopindua Nchi hii kuwa na amani hadi sasa hapa tulipo”, alisema Rais huyo.
Pia alisema kazi kubwa ya Wasanii ni kuburudisha na kuelimisha jamii katika matukio mbali mbali na jukumu la kufanya kazi katika Taifa   na kuwashukuru viongozi wao wote walioko madarakani  katika kuyaendeleza  Mapinduzi Matukufu.
Aidha Tamasha hilo litahudhuria na  Wasanii na kutumia Sanaa hio kwa kuchochea fikra kwa jamii kujua kwamba muziki sio uhuni  ni ajira  na  kazi yake kubwa ni  kutoa elimu  kwa kutumia usanii wa  nyimbo au michezo ya kuigiza kwa nia ya kupatikana uelewa kwa wale watizamaji au wasikilizaji.
Vile vile alisema wanaringa kwa kupatikanwa Mapinduzi na kukumbushana katika Tamasha hilo  ili wawe na huruma kwa roho za wazee wao waliopotea kwani kufanya Mapinduzi hayo ndiko kulikosababisha watembee kifua mbele.
Nae Msemaji Mkuu wa  Kikundi cha Sanaa Zanzibar ( Zanzibar Flever Unit )    Rashid Mustafa aliviomba vyombo vya habari kuwa na mashirikiyano na wasanii ili kuzitangaza kazi zinazofanyika kwa jamii na  kupata uelewa  wa mambo yanayotokea katika nchi yao.
Alisema Tamasha hilo linatarajiwa kuwa kubwa na  kujulikanwa wasanii wa  Zanzibar ambao wana    nafasi kubwa sana katika fani ya muziki.
“Tamasha hili linatarajiwa kuwa kubwa sana na kuweza kuwakutanisha wasanii mbali mbali wa kizazi kipya kutoka sehemu mbali mbali ya Zanzibar wakiwemo Unguja na Pemba tunaiomba jamii ijitokeze kwa wingi  hapo kesho kuanzia saa 6 za mchana hadi saa kumi na mbili jioni”, alisema Msemaji mkuu huyo.
Pia alisema  ndani ya Tamasha hilo ndilo litaloweza kuibua Wasanii wa kila aina na  kutambulika vipaji vyao  kwa kujulikanwa kwa urahisi  katika jamii,nchi au Taifa kwa ujumla.
Akielezea Katibu wa Kikundi cha Sanaa Zanzibar ( Zanzibar Flever Unit )    Salum Dharafi   alisema  Tamasha hilo litahusisha zaidi Wasanii wa Zanzibar  ambao wanahusika na Mapinduzi yaliyotokea katika Nchi yao kwa lengo la kushirikishwa wasanii hao.
Wasanii wanaotarajiwa kushiriki Tamasha hilo ni pamoja na  Chabi 6 , Hemedi Music , Honey ela , Ismail na lady Blach pia na wasanii wengine mbali mbali watashiriki na linatarajiwa kuendelea Kaskazini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.