Habari za Punde

Ubaya wa Rushwa Unaposhamiri Ndani ya Jamii Hupelekea Nchi Kutofikia Malengo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akiizindua Rasmi Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Mkakati Shirikishi wa Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar akiwa Mwenyekiti wake, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi yake uliopo Vuga Mjini Zanzibar.


Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  alisema kwamba ubaya wa Rushwa  unaposhamiri ndani ya jamii mara nyingi hupelekea Nchi kutofikia malengo yake iliyojipangia ya Maendeleo.
Alisema kinga na dawa pekee ya kukabiliana na Rushwa ni kuhakikisha kwamba kila Mwana Jamii anatekeleza Sheria ipasavyo inayoambatana na shughuli za uelimishwaji kufanywa kwa kiwango kikubwa.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiizindua Rasmi Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Mkakati Shirikishi wa Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar akiwa Mwenyekiti wake, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi yake uliopo Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema vitendo vya Rushwa mara kadhaa huchochea Umaskini, Ukosefu wa Ajira, upatikanaji finyu wa huduma za Kijamii ambapo Wananchi wake hushindwa kufikia Malengo ya Kisiasa pamoja na Kiuchumi.
Balozi Seif alisema kwamba Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mipango, Sera, Sheria na Maazimio tofauti na kuchukuwa hatua mbali mbali katika kuona haki na Ustawi wa Wananchi wake unakuwa na kulindwa na kufikia hatua ya kutunga Sheria ya kwanza ya kuzuia Rushwa Mnamo Mwaka 1975.
Alisema Sheria hiyo ilikwenda sambamba na uundwaji wa Tume mbili ili kusimamia udhitibi wa Vitendo vya Rushwa Nchini zilizodumu hadi Mwaka 1985 ambapo ilifutwa na makosa yote ya Rushwa yakaingizwa katika Sheria ya Adhabu { yaani Penal act }.
Balozi Seif  alifahamisha kwamba Sera ya Utawala Bora Zanzibar ya Mwaka 2011 iliyoweka mifumo madhubuti ya Kuzuia Rushwa inaendelea kutekelezwa kwa umahiri wa hali ya juu ambapo Mwaka 2012 Sheria nambari 1 ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Zanzibar ilipitishwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo kwamba hatua iliyofuata ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar {ZAECA } yenye lengo la kusimamia Sheria hiyo iliyoanza mara baada ya kuteuliwa kwa Mkurugenzi wake Mkuu.
Alisema Serikali imefikia hatua ya kuwa na Mkakati Shirikishi wa Kuzui Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar akiwaomba Wananchi wafahamu kwamba Mkakati huo unahitaji kutekelezwa kwa misingi ya Umoja na Mshikamano wa pamoja.
Balozi Seif alisema Taifa limelazimika kuwa na Taasisi hiyo ili kuzidisha kasi ya kufikia malengo yake ya kutokomeza vitendo vya Rushwa na Uhujumu Uchumi hali itakayokuza Utawala Bora Nchini kwa kuwa na Ushiriki wa kila mdau ambao ni Serikali, Sekta za Umma pamoja na zile Binafsi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa kuondosha aina zote za Rushwa kwa njia ya kujenga uadilifu katika kusimamia Sheria za Nchi zilizopo sambamba na uchukuaji wa hatua dhidi ya Vitendo vyote vya Rushwa.
“ Naamini kuwa tukiwa wamoja Visiwa vya Zanzibar bila ya Rushwa inawezekama”. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Mkakati Shirikishi wa Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar.
Aidha Balozi Seif  alisema Jamii lazima ishirikishwe kikamilifu katika kuzuia, kutoa habari na kukataa vitendo hivyo katika maeneo yote ya huduma ili sambamba na kujpatiwa Elimu juu ya madhara ya Vitendo hivyo kwa Maendeleo ya Taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.