Habari za Punde

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Yazindua Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Walimu wa Sayansi na Kiingereza Madarasa ya Tano na Sita Zanzibar.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mmanga Mjengo Mjawiri akizungumza na walimu, Maafisa Elimu na Wakurugenzi wa Halmashauri katika uzinduzi wa Mradi wa Mafunzo ya kutoa msaada kwa wanafunzi wa Skuli za Msingi (TESS) katika Kempasi ya SUZA Nkrumah
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Maalim Abdulla Mzee akiwaeleza walimu wa Skuli za Sekondari walioshiriki uzinduzi wa Mradi wa Mafunzo ya kutoa msaada kwa wanafunzi wa Skuli za Msingi (TESS) katika Kempasi ya SUZA Nkrumah.
Baadhi ya Walimu, Maafisa Elimu na Wakurugenzi wa Halmashauri walioshiriki Mafunzo ya kutoa msaada kwa wanafunzi wa Skuli za Msingi (TESS) wakifuatilia uzinduzi wa Mradi huo katika Kempasi ya SUZA Nkrumah.
Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Amali Mmanga Mjengo Mjawiri na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya kutoa msaada kwa wanafunzi wa Skuli za Msingi (TESS) katika Kempasi ya SUZA Nkrumah.

Na Ramadhani Ali   -Maelezo -Zanzibar.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mmanga Mjengo Mjawiri amesema ili kupata matokeo mazuri ya wanafunzi katika mitihani ya elimu ya juu na vyuo, juhudi kubwa inahitajika katika kuimarisha elimu ya maandalizi na msingi.

Amesema Maafisa Elimu na Walimu wakuu wa skuli za msingi wanapaswa kuwa wasimamizi na wafuatiliaji wa karibu wa kazi za kila siku za walimu wao ili malengo yaliyowekwa ya elimu yaweze kufikiwa. 

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali alieleza hayo alipokuwa akizindua Mradi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu wa masomo ya Sayansi, Kiingereza na Hesabu wa darasa la tano na sita wa skuli za Unguja ili waweze kutoa msaada kwa wanafunzi na kuongeza ufaulu wao.

Alisema imebainika kuwa pamoja na juhudi zinazochukuliwa za kuwapatia walimu mafunzo ya mara kwa mara suala la ufuatiliaji na ufuatiliaji limekuwa ni tatizo kubwa kwa skuli nyingi za Zanzibar.

Aliweka wazi kuwa msimamo wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuwa kuanzia sasa inataka kuona mafunzo yanayotolewa kwa walimu wa skuli yanaleta mabadiliko na kuongeza ufanisi  katika skuli zao 

Aliwataka walimu wakuu kuwa wabunifu katika kuongoza na kushirikiana na Maafisa Elimu na viongozi wa Halmashauri, hasa wakati huu wa wa ugatuzi, kubuni mbinu mpya za kuendeleza mbele skuli zao
.
 Aidha aliwataka walimu wakuu kujitambua na kuthamini nafasi waliyopata huku wakijenga upendo kwa walimu, wanafunzi na kujiepusha kufanya makosa ambayo yanaweza kuwavunjia heshma mbele ya jamii.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mradi huo katika Kempasi ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar Kempasi ya Nkrumah, Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Walimu Maimuna Fadhil Abass alisema kwa vile  elimu ya msingi imeingizwa katika ugatuzi, viongozi wa Wilaya wanatakiwa kuipokea na kuifanyia kazi huku Wizara ya elimu ikiendelea na wajibu wa kusimamia sera.

Akimkaribisha Naibu Waziri kuzindua Mradi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Maalim Abdulla Mzee alisema zipo baadhi ya skuli zinawalimu wazuri lakini zimeshindwa kutoa mwanafunzi hata mmoja kwenda michepuo jambo linaloashiria uwajibika mdogo kwa skuli hizo.

Alisema lengo la Wizara ya Elimu ni kuona kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa michepuo kinaongeza kila mwaka na wameandaa zawadi maalum  kwa skuli itakayo ongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wao kwa kila mwaka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.