Habari za Punde

Balozi Seif ashiriki Maonyesho ya kimataifa ya kilimo, Havana Cuba

 Balozi Seif akimpongeza Balozi wa Afrika Kusini Nchini Cuba kwa umakini wake uliopelekea kupewa nafasi hiyo muhimu ya Kidiplomasia akiwa Mwanamke pekee katika kundi hilo la Mabalozi wa Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiagana na Mabalozi wa Mataifa ya Bara la Afrika waliopo Mjini Havana Nchini Cuba baada ya kumaliza mazungumzo yao ya kubadilishana mawazo baada ya wote kushiriki Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo Mjini Havana.

Picha na – OMPR – Havana


Na Othman Khamis, Havana Cuba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisisitiza kwamba juhudi za pamoja zitaendelea kuhitajika katika kuona changamoto zinazolikabili Bara la Afrika zinakwamka kwa kutumia nguvu za pamoja za Wancnhi wa Bara hilo.

 Balozi Seif alitoa sisitizo hilo wakati akizungumza na Mabalozi wa Mataifa ya Bara la Afrika wanaoziwakilisha Nchi zao Nchini Cuba walipofika kumsalimia na kubadilishana mawazo katika Ukumbi wa Hoteli National Mjini Havana Nchini Cuba. 

Alisema Mataifa ya Afrika muda wote lazima yaendelee kushirikiana kidugu kutokana na Historia yao inayofanana ya Kiutamaduni, Kisiasa, mila na hata Kiuchumi. Balozi Seif alisema wakati umefika sasa wa Wananchi wa Afrika kuanza kubadilika na kujitegemea wenye ili kuepuka mfumo wa utegemezi unaosababisha baadhi ya wafadhili wa kigeni kulazimisha kufanywa mambo yanayokwenda kinyume na mila na Silka za Mataifa hayo. 

Alisema wakati Mataifa ya Afrika yakiendelea kushirikiana kupitia Jumuia mbali mbali za Kiuchumi katika kuelekea kwenye Maendelea, aliwakumbusha Mabalozi hao wa Afrika walioko Cuba kushikamana katika kuliona Bara lao linafunguka kiuchumi kwa kuyashawishi Makampuni na Taasisi za Uwekezaji kuelekeza miradi yao katika Nchi za Afrika.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Bara la Afrika litaendelea kuwa na matumaini makubwa kutokana na Rasilmali zake zinazopaswa kutangazwa na Mabalozi hao katika kazi zao wakizingatia pia mfumo wa kuwa na jumuiya zao za Afisi za Kibalozi ndani ya majukumu yao ya Kidiplomasia. “ Nakumbuka nikiwa Mwanadiplomasia Nchini Misri tuliwahi kuwa na Taasisi yetu ya ushirikiano wa Mabalozi tuliofanya kazi Nchini Misri tukiita Afro Asian Diplomatic Union ambayo ilisaidia kutuunganisha Wanadiplomasia tofauti”. Alisisitiza Balozi Seif. 

Aliwapongeza Mabalozi hao wa Mataifa ya Afrika waliopo Nchini Cuba kwa ukaribu wao wa uhusiano unaowapa fursa nzuri ya ushirikiano kati yao jambo ambalo litawasaidia katika kuwarahisishia kazi zao za kila siku. 

Mapema Kiongozi wa Mabalozi hao wa Mataifa ya Bara la Afrika Nchini Cuba kutoka Nchini Gabon Balozi Jean Claude Moussounda alisema ujio Balozi Seif kushiriki Maonyesho ya Kilimo utafungua ukurasa mpya wa mafungamano baina ya Cuba na Mataifa ya Afrika. 

Balozi Jean alisema Mabalozi hao Sita kwa niaba ya wenzao 26 wanaotekeleza majukumu yao ya Kidiplomasia Mjini Havana Nchini Cuba wamefarajika kushiriki Maonyesho hayo yenye kutoa mwanga wa muelekeo wa kutekeleza vyema jukumu lao la Kibalozi. 

Akitoa shukrani kwa niaba ya Mabalozi hao Balozi wa Jamuhuri ya Kenya Nchini Cuba Balozi Anthony Muchiri ameipongeza Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wake Dr. John Pombe Magufuli kwa kasi kubwa ya maendeleo ya kupigia mfano ndani ya Bara la Afrika. Balozi Anthony alisema kazi ya uimarishaji wa Miundombinu ya Mawasiliano, mapambano dhidi ya Rushwa pamoja na kuingilia zao la Korosho ni mambo ambayo Mataifa ya Bara la Afrika yana haki ya kuyaunga mkono kwa faida ya Ukombozi wa Bara zima

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.