Habari za Punde

BALOZI SEIF : MRADI WA SKULI ZA GHOROFA UTAONDOSHA CHANGAMOTO YA MADARASA KWA WANAFUNZI

   
                                     
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Mradi wa Ujenzi wa Majengo Mpya ya Skuli za Sekondari za Ghorofa unaofanywa na Serikali katika maeneo tofauti Nchini utakapokamilika utasaidia kuondosha changamoto za uhaba wa Madarasa.

Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Uongozi wa Kamati za Skuli za Sekondari za Mahonda na Fujoni pamoja na Walimu alipofanya ziara ya kukagua Kumbi mbili za kufanyia Mitihani za Skuli hizo zilizojengwa kwa nguvu za Wananchi na Walimu.

Aliwashauri Wananchi na Viongozi hao pamoja na wale wa Majimbo mengine kuendelea kubuni Miradi ya Ujenzi na kuianzisha kwa hatua ya msingi na Viongozi pamoja na Serikali itakuwa tayari kuunga mkono Miradi hiyo kwa maendeleo ya Jamii.

Akitoa maelezo kuhusiana na utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf } Mkurugenzi Uratibu Shughuli za Serikali SMT na SMZ Nd. Khalid Bakar Amrani amesema kupitia mradi huo Zanzibar tayari imeshapunguza ukali wa Umaskini kwa asilimia 12%.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Rajab Ali Rajab amesema Skuli ya Msingi na Sekondari ya Mahonda imebeba Wanafunzi wengi kuliko Skuli nyengine yoyote ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.

Nd. Rajab amesema upo umuhimu wa kujengewa mazingira bora zaidi ya kuongezewa huduma za Madarasa Wanafunzi wake kwa lengo la kupunguza  uhaba wa madarasa.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
April 21, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.