Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Akabidhi Vifaa Kwa Uongozi wa Timu ya Muembeladu "Kubwa Lijalo"

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi msaada wa seti za Jezi Mwenyekiti wa Timu ya Soka ya Muembe Ladu Omar Zubeir katika lengo la kuendeleza Michezo Nchini.Wa kwanza kutoka Kushoto ni Kocha wa Timu ya Soka ya Muembe Ladu Ramadhan Madundo na wa kwanza kutoka Kulia ni Katibu wa Timu hiyo Mohamed Mbarouk.
 Mwenyekiti wa Timu ya Soka ya Muembe Ladu Omar Zubeir akimshukuru Balozi Seif kwa msaada huo wa Jeziutakaoleta faraja kwa Uongozi wa Klabu hiyo pamoja na Wachezaji wenyewe.
Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza umuhimu wa kudumishwa nidhamu Michezoni ili wachezaji wajijengee heshima itakayowatanulia hatma njema kimichezo ikiwemo suala la ajira mara baada ya kukabidhi msaada wa Jezi.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema suala la nidhamu michezoni ni jambo la msingi linalomjengea sifa na mafanikio mazuri mchezaji katika maisha yake Kimichezo.
Amesema mchezaji anapofikia hatua ya kutegemewa na Viongozi pamoja na walimu wake kutokana na kipaji alichojaaliwa analazimika kulinda heshima hiyo ili imfikishe daraja analokusudia kufikia hasa suala la ajira.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akiukabidhi Msaada wa seti mbili za Jezi pamoja naahadi ya Mipira Minne kwa  Timu ya Soka ya Muembe Ladu katika azma ya kuunga mkono jitihada za kuendeleza Sekta ya Michezo Nchini.
Alisema nidhamu ndio silaha pekee inayomfikisha kwenye mafanikio Mchezaji au mtu yoyote katika malengo yake akatolea mfano baadhi ya Wachezaji wa Tanzania ambao kwa sasa wanacheza mpira wa kilipwa katika Timu za Mataifa mbali mbali Duniani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Timu ya Soka ya Muembe Ladu kwa jitihada unazochukuwa wa kuwaendeleza Vijana wao Kimichezo na kuweka Historia ya Timu hiyo katika medani ya Soka.
Akipokea Msaada huo Mwenyekiti wa Klabu ya Soka ya Muembe Ladu Omar Zubeir alimshukuru Balozi Seif kwa uamuzi wake wa kuisaidia Klabu hiyo msaada utakaoleta faraja kwao na hata wachezaji wenyewe.
Omar Zubeir alisema Timu ya Soka ya Muembe Ladu na  Ujamaa zina Historia ndefu ya kuwa Timu Moja kipindi cha nyuma isiyosahaulika kwa wapenda soka Nchini kitendo ambacho Kizazi cha sasa kinapaswa kuifuatilia Historia hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.