Habari za Punde

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi Unguja Ataka Umiliki Mali za CCM

Na.Haji Mohd
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja Ndg.Mohamed Rajabu Soud ametoa agizo kwa Wabunge,Wawakilishi na Madiwani wa Mkoa huo kuhakikisha Mali zote walizonunua kwa ajili ya shughuli za Majimbo hati zake ziandikwe umiliki wa CCM na sio wa Majina yao.

Agizo hilo amelitoa katika mwendelezo wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa huo ya kukagua Utekelezaji wa Ilani katika Jimbo la Bububu Wilaya ya Mfenesini Kichama.

Alisema hatowavumilia baadhi ya viongozi wanaonunua vifaa mbali mbali kwa ajili ya Majimbo yakiwemo Gari na Mali zingine wanaoziandika majina yao badala ya jina la CCM. 

Alieleza kwamba chombo pekee kinachomiliki mali zote za Chama ni Baraza la Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi hivyo ni lazima mali zote ziwe chini ya taasisi hiyo.

"Nawaagiza Wabunge,Wawakilishi na Madiwani wote katika Mkoa wangu mali zote walizonunua kwa ajili ya CCM basi ziwe na jina la taasisi hii na sitopenda kuona Gari imenunuliwa kwa ajili ya Jimbo wakati Kadi ya umiliki inasomeka jina la aliyeinunua badala ya CCM.",alisisitiza Mwenyekiti huyo. 

Pamoja na hayo aliwataka Viongozi na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuvunja makundi  yasiyokuwa rasmi kwa mujibu wa miongozo na kanuni za Kikatiba za Taasisi hiyo.

 Alisema kuna baadhi ya Majimbo bado kuna makundi ya kufitinishana  na ugomvi hali inayokwamisha harakati za maendeleo kwani kuna baadhi ya huduma za msingi haziwafikii wananchi kwa wakati kutokana na athari makundi hayo.

 Alieleza kwamba uchaguzi unapomalizika ndani ya Chama Cha Mapinduzi makundi yote yanavunjwa na kubaki kundi moja la CCM linalotoa nafasi pana kwa viongozi wanaochaguliwa kuwatumikia wananchi wao kwa uadilifu.

Aliwataka viongozi wa Jimbo la Bububu Mbunge,Mwakilishi na madiwani kuendelea kufanya kazi kasi zaidi na kutatua changamoto za wananchi ili CCM ishinde kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Rajab alielezea kuridhishwa kwake utendaji wa viongozi hao na kuwataka wazidishe kasi ya kutekeleza Ilani ya CCM hasa katika miradi mbali mbali ya kijamii ambayo bado haijatekelezwa ipasavyo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo Mhe.Mwantakaje Haji aliwasihi wananchi kuitunza na kuithamini miradi mbali mbali ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Jimbo ili iwanufaishe wananchi wote.

Aidha aliahidi kuyafanyia kazi kwa wakati maelekezo aliyopewa na Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa huo ili kuendelea kutekeleza kutekeleza Ilani ya CCM kwa ufanisi zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.