Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein. akiondoa Kipazia kuashiria kuufungua Msikiti wa Masjid Maryam Mtende kushoto Mfanyabiafhara Maaruf Zanzibar Mfadhili wa ujenzi Msikiti huo, Bw. Said Salim Bakhressa hafla hiyo imefanyika katika Kijiji cha Mtende Mkoa wa Kusini Unguja leo.5-4-2019.
Na .Abdi Shamna Ikulu.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein amewataka waumini wa Dini ya kiislamu nchini kujiepusha na
migogoro katika kusimamia uendeshaji wa huduma za misikiti na badala yake
waifanye kuwa chemchem ya kutoa elimu ya dini kwa kuzingatia misingi ya
Masheikh mashuhuri wa Zanzibar waliotangulia.
Dk. Shein amesema hayo huko Mtende, Mkoa wa Kusini Unguja,
katika hafla ya ufunguzi wa msikiti “Masjid Maryam”, uliojengwa kwa msaada wa
mhisani.
Alisema mizozo, migogoro, fujo na mapambano hayapaswi kupangwa
wala kutekelezwa kwenye misikiti, akibainisha kuwa misikiti ni nyumba ya
Mwenyezi Mungu na sehemu tukufu kwa waislamu kufanya ibada.
Alisema kwa mnasaba huo na kwa lengo la kumcha Mwenyezi Mungu,
ndio sababu wahisani huamuwa kuchangia uimarishaji wa nyumba za Mwenyezi Mungu
, hivyo akawataka waislamu wa kijiji cha Mtende kuendelea kuwa wamoja na
kupendana.
Aidha, aliutaka uongozi wa msikiti huo kupitia Ofisi ya Mufti wa Zanzibar kuchukuwa hatua za
haraka kusawazisha pamoja na kuitafutia suluhu migogoro itayojitokeza kwa mujibu wa sheria na
taratibu za dini, kupitia Quraan na hadithi za Mtume Muhammad (SAW).
“Msikiti pawe ni sehemu muhimu ya kuhimizana umuhimu wa kuitunza
amani iliyopo na kujitahidi kufuata maadili mema”, alisema.
Dk. Shein, aliwataka waumini watakaopewa dhamana ya kuusimamia
msikiti huo kufanya uadilifu na kujipambanuwa kwa sifa njema, sambamba na
kujiepusha na mambo yote ambayo Mtume ameasa kuepukwa.
“Nimefurahishwa sana na risala yenu na nakupongezeni kwa
kueleza bayana na kutuhakikishia kuwa uongozi wa msikiti huu hautakaribisha mizozo
kama inavyojitokeza katika baadhi ya misikiti”, alisema.
Rais Dk. Shein aliitaka Kamati inayosimamia msikiti huo kuweka
mikakati pamoja na mipango madhubuti
iliyo endelevu ili kuhakikisha msikiti na madrasa iliopo inakuwa
chimbuko la kuwapata maulamaa na masheikh wapya.
“Tunataka tuwapate kina marehemu Sheikh Juma Baraka wengine wa
Mtende, naamini Mwenyezi Mungu atatupa uwezo wa kuwapata masheikh wapya
watakaotokea hapa”, alisema.
Vile vile, aliwahimiza wazazi na walezi wa kijiji hicho na vyengine jirani kusimamia
vyema maendeleo ya elimu ya vijana wao, akinasibisha kauli yake na matokeo
yasioridhisha ya Skuli ya Mtende katika mitihani ya Taifa, mwaka uliopita.
“Nakuhimizeni mtumie fursa na namna mnavyoshirikiana pamoja na
umoja mlionao kuzitafutia ufumbuzi
changamoto zote zinazosababisha vijana wenu wasipate matokeo mazuri katika
mitihani yao ya Taifa”, alisema.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwataka wazee wa kijiji
hicho na vyengine jirani kutumia vyema fursa ya kufunguliwa msikiti huo wenye
madrasa kujiongezea maarifa katika masuala ya dini ili waweze kufanya ibada kwa
usahihi.
Alisema ujenzi wa Msikiti huo na hatua ya maendeleo yake
umezingatia suala zima la kuendeleza elimu, ikiwa ndio msingi wa mambo yote
sambamba na kumuongoza binadamu kupata mafanikio na maisha mema.
“Elimu ndio nyenzo inayomuwezesha muumini kutekeleza vyema
ibada zake na kuishi katika uchamungu”, alisema.
Dk Shein alieleza kuwa kitendo cha waumini kutowa sadaka ni miongoni
mwa ibada muhimu zilizohimizwa katika Qoraan na hadithi za Mtume Muhammad
(SAW), ambapo Mwenyezi Mungu amewahakikishia malipo makubwa waumini
wanaotekeleza ibada hiyo.
Alisema kupitia Aya za Suratul Hadyd Mwenyezi Mungu
amebainisha kumuongeza baraka zaidi mja anaetowa, ambapo faida zake huonekana
duniani na kesho mbele ya haki, hivyo akamuombea malipo mema mhisani
aliefadhili ujenzi huo.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa kijiji
cha Mtende kwa kuwa wamoja na kuendeleza ushirikiano na Serikali, hatua iliyowawezesha
kupata maendeleo makubwa katika huduma mbali mbali za kijamii, ikiwemo miundombinu bora ya barabara.
“Mtende hivi sasa inafikika kirahisi kwa kuwa na barabara
nzuri ya lami na watu wanafaidika na huduma za umeme, huduma za Afya na elimu
ya maandalizi”, alisema.
Kuhusiana na changamoto za upatikanaji wa huduma za maji safi
na salama , Dk. Shein alisema changamoto hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na
ongezeko la kiwango cha chumvi katika pango la Chau ambalo ni tegemeo la huduma
hiyo kwa muda mrefu.
Alisema kupitia mradi wa uchimbaji wa visima wa Ras Al Khaimah
, tayari kisima kimoja kipya kimechimbwa katika kijiji hicho.
Aidha, alisema Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imejenga tangi jipya la maji lenye uwezo wa
kuhifadhi lita 120,000 kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa shehiya hiyo na
kubainisha kuwa miundombinu ya umeme na mabomba inatarajiwa kuungwa hivi
karibuni.
“Nakuombeni muendelee kuwa na subira, kwani wazee walisema ‘subira
huvuta kheir’, nina imani jitihada zetu zitafanikiwa na kheri itapatikana kwa
uwezo wa Mwenyezi Mungu kabla ya kumalizika mwaka huu”, alisema.
Mapema, Sheikh Khamis
Ramadhan, akisoma risala ya wananchi wa Mtende, alisema ujenzi wa msikiti huo umewapunguzia masafa ya
kufuata eneo la ibada waumini wa karibu na kitongoji hicho na hivyo kupata
fursa nzuri ya kufanikisha ibada zao.
Alimpongeza mfadhili wa ujenzi wa msikiti huo Sheikh Said
Salim Bakhresa kwa imani na mapenzi makubwa aliyonayo kwa wananchi wa kijiji
hicho na kufadhili ujenzi huo.
Katika hatua nyengine, wananchi wa Mtende wamepongeza
mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii
yaliofikiwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba chini ya
uongozi wa Dk. Shein.
Aidha, walipongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali katika
kuitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto ya maji safi na salama inayokabili
kijiji hicho.
Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi, aliwataka
waumini wa msikiti huo kuutunza, sambamba na kuwaendeleza watoto kitaaluma,
akibainisha hatua hiyo yaweza kuwa sababu ya kupatikana imani na upendo
miongoni mwao.
Aidha, alisema ni fahari kubwa kwa watu wa Mtende kupata
msikiti huo na kufunguliwa na kiongozi mkuu wa nchi, hivyo akawataka waumini
hao kuutumia kwa ajili ya kuwaunganisha.
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment