Habari za Punde

Valisha Mtoto Viatu Kupitia Mradi wa Best Of Zanzibar.“Pair for Every Child campaign”


Maofisa wa Mradi wa Best of Zanzibar wakigawa viatu kwa Watoto wa Skuli ya Msingi na Maandalizi za Kijini na Mbuyu Tende Kijiji cha Matemwe Mkoa wa Kaskazini B Unguja, uzinduzi wa uendelezaji wa kuwapitia viatu Wanafunzi, kupitia "Valisha Mtoto Viatu" hafla hiyo imefanyika katika  viwanja vya Skuli ya Kijini Matemwe. 

Best of Zanzibar inaendelea kwa mafanikio makubwa katika Kampeni yake ya “Valisha Mtoto Viatu” katika skuli ya Kijini na Mbuyu Tende. Kampeni hiyo yenye kutambuliwa kwa hashtag ya #PECcampaign ama kwa lugha ya kigeni “Pair for Every Child campaign” imeweza kuwapatia watoto zaidi ya 700 viatu kwa mwaka wa 2018. Miezi michache ya mwaka huu, Best of Zanzibar kupitia wadau mbali mbali ndani na nje ya nchi imeweza kupata pesa za kununua viatu ziada ya peya 400 ambavyo vitatolewa kwa watoto wa Skuli ya Maandalizi na Msingi katika Skuli za Kijini na Mbuyu Tende Matemwe.

Kupitia Kampeni hii ya viatu, Best of Zanzibar imeweza kupunguza idadi ya watoto wanaokwenda shule bila viatu katika vijiji hivi viwili. Watoto wadogo wa miaka minne wanatembea masafa marefu kama kilomita 5 kwenda shule na kurudi kila siku, kipindi kama hiki cha mvua, ama jua na ardhi hii yam awe na mavumbi ambapo inakuwa vigumu kwa watoto hawa kuhimili.

Kampeni ya Valisha Mtoto Viatu inatoa shukurani zake za dhati kwa wote waliofanikisha kampeni hii ndani ya Zanzibar na sehemu nyenginezo duniani ambao wamechangia kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya kwa vijiji hivi vya Kijini na Mbuyu Tende.

“Lengo letu ni kuona watoto hawa wankwenda skuli na viatu bora kwa ajili ya usalama wao na mahudhurio mazuri darsani ili kuongeza ufanisi wao na ufaulu shuleni. Waathirika zaidi ni watoto wadogo ambao ni chekechea na darasa la kwanza, ndio maana mwaka huu wa 2019 tumewalenga zaidi watoto wadogo wa miaka 4 mpaka 8” Alisema Meneja wa Best of Zanzibar, Aminata Keita. “Tunawashukuru sana wadau wetu wote na wasamaria wema kutoka Zanzibar, Afrika Kusini na hata ghuba ya mbali (Uarabuni) ambao wamewezesha watoto hawa kuvaa viatu. Natoa wito kwa NGO’s na mashirika mengine waungane nasi pamoja na kufanya Kampeni hii iwezekane kwa Zanzibar nzima” Aliongezea Aminata Keita

Mgeni Rasmi katika sherehe hiyo alikuwa ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na wageni wengine mashuhuri kutoka Serikalini na sehemu mbali mbali. Mbali na utowaji wa viatu, Best of Zanzibar ilikabidhi zawadi kwa wanafunzi 50 ambao wamefanya vizuri katika masomo yao ya Hisabu na Kingereza kwenye program ya masomo ya ziada ijulikanayo kama “After-hours Tutoring Program”

“Best of Zanzibar ilianza program yake ya masomo ya ziada kwa Kingereza na Hisabati miaka miwili iliyopita, na tunafurahi kuona mabadiliko makubwa katika matokeo na maendeleo ya wanafunzi hawa ya mwaka 2018. Leo tunawazawadia wanafunzi 50 waliofanya vizuri katika masomo haya mawili kwa kuwapa mabegi ya shule vifaa vyengine vya shule. Mwaka huu, programu yetu imeongeza walimu 6 wa masomo ya sayansi ambao nao watafanya kazi kwa kushirikiana na walimu wakuu katika Physics, Chemistry na Biology. Tunawaomba wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kuleta mabadiliko mazuri katika jamii yao, tunatarajia miaka ijayo Kijini itakuwa moja ya skuli bora visiwani” Alisema Mratibu wa Elimu na Uwezeshaji wa Best of Zanzibar, Ally Suleiman

‘Mkurugenzi wetu Bwana Brian Thomson ameahidi kuwafadhili wanafunzi katika masomo ya Uhandisi, ijapokuwa ni vigumu kuwapata wanafunzi wanaofaulu vizuri katika masomo ya sayansi ambalo ndio hitajio la kwanza ili uweze kusomea Uhandisi, hii ndio sababu ya kuongeza masomo ya sayansi kwenye program yetu” Aliongeza Ally Suleiman

“Leo tunashuhudia maadhimisho haya kwa furaha kubwa, kupokea zawadi kwa wanafunzi wetu na viatu kwa Kampeni hii ya “Valisha Mtoto Viatu.” Viatu hivi vimewasaidia sana wanafunzi wetu katika safari yao ya masomo na moyo wa kuja shule. Na kuwapatia zawadi wale ambao hawakufanya sana vizuri lakini ni wahudhuriaji wazuri zaidi na wana nidhamu nzuri, pia itachangia kuongeza ufaulu kwani itawashawishi watoto kuja shule sasa. Wazee na walimu wa Kijini wamefurahia watoto wao kuwa na viatu na vifaa vya shule kwa wanafunzi zaidi ya 600 ambao wananufaika na program hii ya Best of Zanzibar, ambayo inachangia kwa kiwango kikubwa kuleta ufanisi na matokeo mazuri kwa wanafunzi. Mafanikio yanaonekana na tunashukuru mwaka wa pili wa watoto hawa kupata viatu” Alisema, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kijini – Ulimwengu

Shughuli hiyo iliadhimishwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Mhe. Vuai Mwinyi, Wakurugenzi na Viongozi wengine wa Serikali ambao waliomba wadau wengine kuunga mkono Kampeni hiyo ya viatu sio tu kwa Kijini na Mbuyu Tende bali kwa Zanzibar nzima.

“Tunaipongeza Best of Zanzibar kwa kuendelea na juhudi zao za kukuza elimu Kijini na Mbuyu Tende. Wameweka mfano bora kwa wengine kufuata kwani hakika kuwekeza kwenye elimu ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu. Pia, natoa wito kwa wanafunzi na vijana kufanya juhudi katika masomo yao ili waweze kufaulu, Best of Zanzibar na walimu wamefanya sehemu yao hivyo basi na wanafunzi mfanye juhudi ili kupata mafanikio” Alisema, Hon. Simai Said

Best of Zanzibar inawaomba wasamaria wema kuungana nao katika Kampeni hii ya viatu na kuhakikisha watoto wote wanaenda shule na viatu. Tuwawezeshe vijana hawa kufikia malengo yao.

Tafadhali wasiliana nasi kwa mitandao ya kijamii au email: aminata@best-of-zanzibar.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.