Habari za Punde

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayuob Mohammed Azungumzia Kipindi Hichi Cha Mwezi wa Ramadhani

Na  Mwashungi Tahir - Maelezo Zanzibar.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud  ametoa onyo kwa kipindi hichi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa  Ramadhani ambao unatarajiwa kuanza kesho tarehe 7-5-2019  kufungwa baa zote za mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na mashehe wa dini zote wakiwemo na viongozi wa Chama cha Mapinduzi huko ofisini kwake Vuga wakati alipokuwa akitoa taarifa kuhusu mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema katika kipindi chote cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi inapiga  marufuku kuwa wazi baa zote pamoja na maduka yanayouza pombe mziki kwa nyakati zote ikiwa usiku au mchana.
"Napiga marufuku kwa kipindi hichi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani  mambo yote ya starehe ikiwemo vilevi, muziki ,mikahawa na vioski vyote kufungwa mara moja"alitoa msisitizo Ayoub.
Pia Ayoub alisema anapiga marufuku mikahawa, vioski na maeneo yote yanayouzwa yanayouzwa vyakula na mama lishe na baba lishe kuuza biashara zao wakati wa mchana na badala yake wauze wakati wa magharibi.
Aidha alitoa indhari kwa wale wenye nyumba za kulala wageni na nyumba zinazokodishwa watu kufanywa madanguro kuwa Serikali ya Mkoa itachukuwa hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kuzitumia nyumba hizo katika kipindi hichi cha Ramadhani.
Aliwataka viongozi wote wakiwemo wakuu wa Wilaya , Masheha na Mabaraza ya manispaa katika Mkoa huu kuhakikisha amri hizi zinatekelezwa na kwa yeyote atakaepinga amri hizo sheria zitafata mkondo wake.
Hivyo alitoa wito kwa wakaazi wa Mkoa wa     Mjini katika kipindi hichi kuzingatia mavazi ya heshima  kama ilivyo desturi yetu na kuwataka wale wanaongoza watalii wawakumbushe kuvaa mavazi ya stara yanayozingatia maadili ya Kizanzibar.
"Nawaomba wale wanaotembeza watalii wawahimize kuvaa mavazi ya kiheshima kwa kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani kwa kufuata mila na desturi zetu", alisema Mkuu wa Mkoa.
Ayoub alisema katika mwezi huu shughuli za biashara , ibada  na matukio mengi ya kidini  huongezeka hivyo Serikali ya Mkoa itahakikisha hali ya Ulinzi na Usalama itaimarika zaidi kwa kuweka doria katika maeneo yote lengo ni waumini wa dini ya kiislam wanapata kutekeleza nguzo hii kwa hali ya amani na utulivu.
Alisema katika kuhakikisha wito wa        Muheshimiwa Rais wa Zanzibar Ali Mohamed Shein unatekelezwa naomba sekta husika inayosimamia biashara kuimarisha ukaguzi katika masoko na maduka ndani ya Mkoa wa Mjini kuhakikisha bei za bidhaa hazipandi na watakaobainika kwenda kinyume hatua za sheria zitafuata.
Na kwa upande wa usafiri wa dala dala amewataka wawe makini ili kupunguza ajali zinazoweza kutokea kwa vile harakati zinaongezeka msongamano hasa inapokaribia karibu ya wakati wa magharibi .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.