Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein, akitowa Risala ya Kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Mfungo wa Ramadhani unaotaraji kuaza wiki ijayo. Waumini wa Dini ya Kiislamu Duniani hujumuika katika Mfugo huo ikiwa ni moja ya Ibada ya Kiislam
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein amewanasihi wafanyabiashara kuwa waadilifu katika kuwafanyia wanunuzi tahafifu za bei za bidhaa na huduma nyenginezo hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alhaj Dk. Shein aliyasema
hayo katika risala maalum aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari
katika kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika mwaka huu wa 1440 Hijria
sawa na mwaka 2019 Miladia.
Katika risala yake hiyo,
Alhaj Dk. Shein aliwataka wafanyabiashara kukumbuka kwamba kwa kufanya hivyo
hawatokula hasara bali watazidi kupata fadhila mbali mbali za Mola wao Mlezi
zinazoambatana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Aliwataka wafanyabiashara
kuzingatia ubora wa bidhaa wanazowauzia wananchi kwani wanapaswa wahakikishe
kwamba wanawauzia bidhaa ambazo hazijapita muda wake wa matumizi.
Kwa msingi huo Alhaj Dk.
Shein alieleza kuwa wanunuzi nao wanatakiwa wawe makini wanaponunua bidhaa
kwani si jambo la busara kununua bidhaa iliyokwisha muda wake wa matumizi kwa
kufuata urahisi wa bei kwa sababu urahisi huo ni gharama kubwa kwa afya zao.
Aidha, aliwataka
wakulima waendelee na ustaarabu pamoja na utamaduni wao ule ule wa ustahamilivu
na uadilifu kwa kujiepusha na tabia ya uvunaji na uuzaji wa mazao machanga.
Alhaj Dk. Shein
aliwataka wauzaji wa bidhaa mbali mbali kama vile matunda, samaki, mboga na
nyenginezo waache ile tabia ya kuuza bidhaa zao maeneo ya barabarani au
kuziweka chini bila hata ya kutandika kitu kilicho safi.
Alisisitiza kwamba
wafanyabiashara ni lazima wafahamu kwamba kufanya biashara bila ya kuzingatia
taratibu zilizowekwa kunaweza kuhatarisha usalama wa wapitao njiani, kuathiri
ubora wa bidhaa hizo pamoja na afya za watumiaji wa bidhaa hizo.
Rais Dk. Shein aliongeza
kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar si kumkomoa mtu kwa sababu
Serikali huwa haiwakomoi wananchi wake bali dhamira yake ni kuwalinda na kuona
kwamba hawafikwi na matatizo ambayo yanaweza kuepukika na kujikinga nayo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alizitaka Taasisi zinazohusika zisimamie vyema shughuli za biashara masokoni na
madukani, ili vitendo vya ghilba kwa wananchi ambao ndio wanunuzi na watumiaji
wakubwa wa bidhaa visiendelee.
Alisisitiza kuwa mwezi
wa Ramadhani ni mwezi wa kuoneana huruma na kufanyiana hisani kwa hivyo
wananchi wazidishe imani na huruma ili waweze kuitekeleza ibada ya saumu bila
ya bughudha na usumbufu.
Pamoja na hayo, Alhaj
Dk. Shein alitoa nasaha zake kwa wale ambao si Waislamu na wale ambao watakuwa
na dharura zinazowazuwia wasifunge kuwa wasifanye vitendo vitakavyoathiri
wanaofunga.
Alieleza kuwa huduma
zote muhimu pamoja na zile zinazotolewa kwa wageni hasa watalii ziendeshwe kwa
kuzingatia misingi ya kuwaheshimu ndugu zao wanaofunga na kuuheshimu Mwezi
Mtukufuwa Ramadhani,
Alhaj Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuhimizana zaidi kuisoma Qur-an kwa wingi ndani ya Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani pamoja na kujitahidi kufahamu mantiki ya maelekezo yake.
Aliwataka waumini
kuhimizana kuhudhuria darsa katika misikiti ndani ya mwezi wa Ramadhani na
kuepuka kutumia muda kwa kufanya mambo yasiyo na manufaa katika mwezi huo
ambayo yanapingana na mafunzo ya Uislamu na silka zao.
“Huu ni mwezi ambao
umepewa daraja kubwa ya utukufu na Mwenyezi Mungu (S.W) kwa sababu ndani yake
kuna mambo matukufu……ni mwezi ambao ibada za waja hulipwa fadhila nyingi kuliko
katika kiezi mingine”,alisisitiza Alhaj Dk. Shein.
Kadhalika Alhaj Dk.
Shein aliiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati na uongozi wa Mamlaka
ya Maji (ZAWA) kuhakikisha kuwa ule utaratibu wa kila mwaka wa kusambaza maji
unatekelezwa katika maeneo yenye shida ya maji na ambayo bado huduma hiyo
haijafika Unguja na Pemba.
Pia, Alhaj Dk. Shein
aliziagiza Taasisi zote zinazohusika zikiwemo Mabaraza ya Manispaa, Mabaraza ya
Miji na Halmashauri zote za Wilaya Ungua na Pemba ziyasimamie ipasavyo majukumu
yao ya kudumisha usafi katika miji na vijiji pamoja na shughuli zote za
kiuchumi na kijamiizinazofanywa katika Mwezi huo mtukufu.
Alisisitiza kuwa
utaratibu wa kufutari kwa pamoja ni vyema ukafanywa kwa kuzingatia sana masuala
ya usafi pamoja na kufuata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa afya na usafi wa
mazingira.
Alhaj Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kueleza jinsi uchumi wa Zanzibar ulivyoimarika ambapo kwa mwaka wa
fedha 2017-2018 uchumi ulikuwa kwa kasi ya asilimia 7.1 sambamba na kushuka kwa
mfumko wa bei kutoka kasi ya 5.6 mwaka 2017-2018 hadi kufikia asilimia 3.9 mwaka
2018-2019.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein aliwatakia kila la heri Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi
wakiongozwa na Spika Zubeir Ali Maulid katika Mkutano wao wa 14 wa Baraza la
Tisa la Wawakilishi utakaojadili Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha wa
2019-2020.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment