Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud akizungumza na kutowa shukrani kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, wakati wa hafla ya futari ilioandaliwa na Benki ya Watu wa Zanzibar kwa Wateja wao na Wananchi wa Zanzibar katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein ameendelea kuwasisitiza wafanyabiashara kutowauzia wananchi bidhaa kwa bei ya juu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na miezi ijayo.
Akitoa neno la
shukurani kwa niaba ya Rais Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharii Ayoub
Mahamoud aliyasema hayo katika futari maalum iliyoandaliwa na Benki ya Watu wa
Zanzibar (PBZ), iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni, Mjini
Zanzibar.
Katika maelezo ya
shukurani hizo Rais Dk. Shein aliwataka wananchi kutokwenda kinyume na maagizo
yake aliyoyatoa katika hotuba yake aliyoitoa kwa wananchi katika kuukaribisha
mwezi wa Ramadhani mwaka huu kwa kuwanasihi kutouza bidhaa zao kwa bei ya juu
hasa mwezi huu wa Ramadhani.
Aliongeza kuwa kuuza
bidhaa kwa bei ya juu kutawapelekea wananchi kupata usumbufu mkubwa katika
kutekeleza ibada yao ya funga hivyo, aliwataka wafanyabiashara kutofanya
vitendo hivyo kwa mwezi huu wa Ramadhani na miezi ijayo hasa ikizingatia pia,
mwezi ujao kuna Sikukuu ya Idd Fitr ndani yake.
Aidha, Rais Dk. Shein aliendelea
kuwasisitiza wafanyabiashara kutowauzia wananchi bidhaa zilizopitwa na muda
pamoja na bidhaa ambazo hazijafika muda wa kuliwa hasa mazao ya chakula ili
kuendelea kuupa heshima mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein aliwataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuitumia hiyo Benki ya Watu
wa Zanzibar (PBZ) kwani ni benki ya Serikali pamoja na kuendelea kufungua
hesabu zao kwa huduma za Kiislamu na zisizo za Kiislamu.
Rais Dk. Sheim pia,
alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa wale wote waliopata athari za mafuriko ya
mvua za masika zinazoendelea hapa nchini.
Pia, aliwataka wananchi
wa Zanzibar kuendeleza umoja na mshikamano ambao utadumisha amani na utulivu uliopo
nchini ili maendeleo zaidi yazidi kupatikana.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alitoa pongezi kwa Benki hiyo kwa juhudi zake kubwa inazoendelea
kuzichukua katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kusisitiza haja ya
kuziendeleza zaidi ili zizidi kuleta
tija na maendeleo kwa nchi na wananchi wake.
Mapema, Mjumbe wa
Kamati ya Sheria ya Benki hiyo ambaye pia, ni Katibu wa Kamisheni ya Wakfu na
Mali ya Amana Sheikh Abdallah Talib alitoa shukurani kwa Benki hiyo kwa
kuendeleza utamaduni wa kuwafutarisha wananchi wakiwemo wateja wao na kueleza
kuwa kitendo hicho cha heri kinaleta mapenzi makubwa ndani yake.
Sheikh Abdallah Talib
alieleza kuwa kitendo hicho cha kufutarisha kilichofanywa na Benki hiyo ya Watu
wa Zanzibar kinaonesha alama ya watu walio wema sambamba na kuonesha jinsi
Benki hiyo ilivyokuwa karibu na inavyowajali wateja wake.
Katika hafla hiyo ya
futari viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid
na viongozi wengine wa dini na Serikali pamoja na wananchi mbali mbali wakiwemo
wateja wa Benki hiyo.
Leo Alhaj Dk. Shein anatarajia
kuungana pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja katika futari maalum
aliyowaandalia.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment