Habari za Punde

Wiziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Azungumza na Waziri wa Afya na Viongozi wa Taasisi ya Aga Khan Jijini Dodoma leo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongoza mazungumzo kati yake, na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (wa pili kushoto) pamoja na Viongozi wa Taasisi ya Aga Khan, Ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Mei 28, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) ukamilishe majadiliano yao na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhusu matumizi ya kadi za NHIF kwenye hospitali zao ili Watanzania wengi zaidi waweze kunufaika.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Mei 28, 2019) alipokutana na viongozi kadhaa wa taasisi hiyo pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango unaotolewa na taasisi ya AKDN katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya.

“Nilijionea kazi kazi kubwa inayofanyika pale Hospitali ya Aga Khan Machi, mwaka huu, niliongea na wagonjwa na kupata maoni yao, lakini kikubwa tu mpunguze gharama na muimarishe huduma zenu,” amesema.

Amewapongeza viongozi hao kwa utoaji wao wa huduma kwenye sekta nyingine kama elimu, maji na kilimo. “Tunategemea mtaendelea kuimarisha huduma hizo ili ziwasaidie Watanzania wengi zaidi,” amesisitiza.

Viongozi hao walikutana na Waziri Mkuu ili kumuarifu juu ya mpango wa taasisi hiyo wa kuanzisha kituo maalum cha matibabu ya saratani nchini (Specialised Cancer Care Facility) ambao unatarajiwa kugharimu dola za marekani milioni 15. Kituo hicho kitaendeshwa kwa ubia baina ya hospitali za Ocean Road, Muhimbili, Bugando na Aga Khan.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alimweleza Waziri Mkuu kwamba hospitali za Ocean Road na Bugando zinatoa huduma za radiotherapy na chemotherapy, wakati hospitali ya KCMC inatoa huduma ya chemotherapy tu. “Hospitali ya Rufaa ya Mbeya bado huduma hizo zinaadaliwa ili ziweze kutolewa,” alisema.

Hata hivyo, Waziri Ummy alisema hivi sasa kwa nchi nzima, kuna vituo zaidi ya 120 ambavyo vinatoa huduma ya utambuzi wa saratani (cancer screening).

Mapema, akitoa maelezo kuhusu mpango wa kujenga kituo hicho, Mwakilishi Mkazi wa AKDN, Bw. Amin Kurji, alisema wameshawasiliana na hiospitali zote tajwa na sasa wanashirikiana na wataalamu wa wizara ya afya ili kukamilisha suala hilo.

“Tatizo la saratani hapa nchini ni kubwa kwa sasa. Lakini tunataka watu watambue kwamba ukiugua saratani haimaanishi kwamba utakufa mara moja (it’s not a death sentence). Inaweza kutibika endapo mgonjwa atawahi kupata matibabu,” alisema Bw. Kurji.

Alisema kwa sasa hivi hapa nchini hakuna kituo maalum cha matibabu ya saratani nchini lakini kitu cha pekee kuhusu kituo hicho ni uwepo wa huduma zinazotembea za upimaji na utoaji tiba hadi mikoani. “Huduma hizi zitakuwa zinatolewa kwenye mikoa yote kupitia njia ya mtandao, ilhali vituo vikuu vya Dar es Salaam na Mwanza vitakuwa vikitoa majibu kwa madaktari husika,” alisema.

Alisema lengo lao pia ni kutoa elimu juu ya kuzuia, upimaji wa mapema na upatikanaji wa tiba (prevention, early diagnosis and cure).

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA.        
JUMANNE, MEI 28, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.